Akhlaqi Katika Uislamu (32)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 32 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitazungumzia masuala ya uchumi na nafasi yake katika Akhlaqi za Kiislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.
Mpendwa msikilizaji, moja ya mambo ya msingi na yenye taathira kubwa ya kuifanya familia iwe thabiti na imara ni suala la uchumi. Pamoja na hayo kinachopasa kuzingatiwa zaidi juu ya suala hili ni namna sisi wenyewe tunavyoyaangalia masuala ya uchumi. Japokuwa masuala ya kifedha yana taathira kubwa katika mipango na uendeshaji wa familia lakini kwa mtazamo wa Uislamu haifai kuyafanya kuwa ndio lengo halisi la maisha kama yanavyoangaliwa na mfumo wa Ubepari wa Magharibi. Kwa sababu tutakapokuwa hivyo, utamaduni wa Umaada, yaani akhlaqi za kujali vitu tu ndio utakaoshika nafasi katika malengo na mipango ya maisha yetu; na matokeo yake, familia zetu zitakuwa zikijali na kufikiria maslahi yao zenyewe tu ya kiuchumi na kughafilika na shida na dhiki walizonazo watu wanyonge. Katika hali hiyo, moyo wa utu utaanza kutoweka kidogo kidogo na sumu ya sifa chafu kama za kujilimbikizia mali, matumizi ya israfu na kuishi maisha ya kifakhari itapenya na kusambaa ndani ya mwili wa familia. Lakini kama mke na mume wataliangalia suala la uchumi kwa jicho la wenzo na suhula tu ya kuendeshea maisha yao, katika hali hiyo wataweza kwa wakati mmoja kunufaika na wenzo wa uchumi kwa ajili ya kujikimu kwa mahitaji ya lazima ya maisha yao, kwa namna itakayoimarisha hisia za upendo kwa watu wa familia yao; na wakati huohuo kuwa na raghaba na shauku ya kutekeleza jihadi ya mali, kwa kuwa tayari kujihini na kujitolea ili kuwasaidia wanyonge na wahitaji. Katika hali hiyo, haitakuwa rahisi katu kunasa kwenye mtego wa ubinafsi na uchoyo, israfu na ufakhari. Hata hivyo, ili kuweza kufanikisha lengo hilo inapasa mke na mume wawe na fikra na mtazamo unaofanana; ili mbali na kusimamia ipasavyo masuala ya kifedha na kiuchumi ya familia yao, watekeleze pia jukumu na masuulia ya kiutu na kibinadamu waliyonayo kwa ajili tu ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu.
Kwa mtazamo wa kiujumla, kuna watu wa aina tatu katika suala la namna mume anavyosimamia jukumu lake la uendeshaji masuala ya kifedha na kiuchumi ya familia yake. Aina ya kwanza ni ya mume aliye maridhia wa kila kitu katika kutii na kutekeleza kila akitakacho mkewe. Yeye huwa hana sauti, uamuzi wala mamlaka ya jambo lolote katika ndoa yake, zaidi ya kuridhisha matashi na matakwa ya mkewe. Matokeo yake ni kuwa mtu wa kusahau majukumu na masuulia yake yote ya kidini na kiutu; na hima yake yote kuwa ni kufanya yale yatakayompendeza mkewe. Aina ya pili ya mume ni yule asiyejali wala kuwajibika kwa namna yoyote kuhusiana na masuulia ya kiuchumi aliyonayo kwa familia yake. Yeye huwa na mtazamo wa kuendesha familia yake kimfumo dume wa kumburuza mke, kuwa na kauli ya mwisho katika kila jambo na kufanya lolote lile atakalo bila kujali mahitaji ya mke na familia yake. Lakini kinyume na makundi hayo mawili, kuna aina ya tatu ya mume aendeshaye masuala ya kiuchumi ya familia yake kwa mtazamo wa kadiri na wastani, kwa kufuata miongozo na mafunzo ya aya za Kitabu cha Mwenyezi Mungu na sira za viongozi wa dini. Aya ya 29 ya Suratul-Israa inalibainisha hilo kama ifuatavyo: "Wala usiufanye mkono wako kama ulio fungwa shingoni mwako, wala usiukunjue wote kabisa, utabaki ukilaumiwa muflisi."
Baada ya ushindi na kumalizika kwa vita vya Jamal, Imam Ali (AS) alifika katika mji wa Basra. Siku moja alikwenda kumtembelea mmoja wa wafuasi wake aitwaye A’laa bin Ziyad Haarithi, ambaye alikuwa na nyumba kubwa. Alipoitupia jicho nyumba ya A’laa na ukubwa iliokuwa nao, Imam Ali alisema: “Kuna haja gani ya kuwa na nyumba kubwa kama hii wakati unahitajia zaidi kuwa na makazi makubwa akhera?” Kisha baada ya kusema hayo, mtukufu huyo alimuelekea A’laa na kumwambia: “Bila shaka kama utataka, unaweza kuifanya nyumba hiihii kubwa wasila na wenzo wa kujistawishia nyumba na makazi yako ya akhera. Ni pale utakapoifanya mahala pa kupokelea wageni, kuunganishia udugu na ujamaa na kuifanya kituo cha kushughulikia na kutatua shida na matatizo ya wahitaji na kuwatimizia haki zao zinazokuwajibikia na kutoitumia kwa manufaa yako binafsi tu na familia.”
Baada ya kupewa nasaha na miongozo hiyo yenye thamani kubwa, A’laa kwa upande wake, alimsikitikia na kumshtakia Imam Ali (AS) kuhusu ndugu yake aitwaye A’sim kwa kusema: “Ameitelekeza aila yake, amekhitari kuvaa nguo chakavu, ameacha kujituma kufanya kazi na ameamua kujitenga na kujiweka mbali na watu." Aliposikia vile, Imam Ali (AS) aliamuru palepale akaitwe A'sim aje mbele yake. Alipomwona alimwambia: "Ewe adui wa nafsi yako, ni wazi kwamba shetani ameiteka akili yako. Kwa nini umewatelekeza mke na watoto wako? Unadhani Mwenyezi Mungu aliyekuhalalishia na kukujaalia neema chungu nzima za dunia yuko radhi na anafurahia tabia na mwenendo wako huu potofu? Acha ndugu yangu mwenendo huu usio sahihi na ifaidishe nafsi yako na aila yako na neema za Mwenyezi Mungu". (Sehemu ya hotuba ya 207 ya Nahjul-Balaghah).
Pamoja na yote tuliyoeleza mpendwa msikilizaji kuhusu nafasi na wajibu wa mume wa kushughulikia mahitaji ya kifedha ya familia yake, baadhi ya wakati changamoto za kiuchumi huyatikisa maisha ya familia mpaka mke na mume wakalazimika kufanya kazi pamoja nje ya familia ili kumudu na kuweza kukimu mahitaji ya kiuchumi ya aila yao. Lakini hata kama itawalazimu kufanya hivyo, kwa vyovyote vile haifai kwa mke kughafilika na jukumu na masuulia yake makuu ya umama na malezi ya watoto na mustakabali wao, bali muda wote ajitahidi kuhakikisha anailinda nafasi hiyo ili isije ikadhurika au kulegalega kwa namna yoyote ile. Inasikitisha kuona wananadharia na watetezi wa fikra ya Ufeministi wanapinga mtazamo huu kwa kisingizio cha kutetea haki za wanawake na usawa baina yao na wanaume; na hawako tayari katu kuitambua nafasi ya mwanamke kama mama katika ndoa na familia. Miongoni mwa taathira hasi za mtazamo huo ni kudhoofika hisia safi za upendo na huruma za mama kwa watoto, kuwakosesha watoto joto la huba, huruma na mapenzi ya kuwa karibu na mama yao, kudhoofisha mahusiano ya kifamilia na mwishowe kuporomoka na kusambaratika nguzo za jengo takatifu la ndoa. Kwa hiyo, pamoja na umuhimu na nafasi ambayo mke anaweza kuwa nayo ya kuchangia masuala ya kifedha kwa ajili ya uendeshaji wa familia, lakini hilo lisiwe sababu ya kumghafilisha yeye na nafasi yake kuu na hasasi ya umama na ya malezi ya watoto na vizazi vijavyo na ambayo ni muhimu mno kwa ajili ya kudumu na kuwa imara zaidi familia. Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji niseme pia kuwa, sehemu ya 32 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 33 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/