Akhlaqi Katika Uislamu (34)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 34 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitazungumzia ulazima wa elimu kuambatana na imani katika akhlaqi za Kiislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.
Katika kipindi kilichopita tulieleza kwamba Bwana Mtume Muhammad SAW alianzisha mapinduzi yake ya kiutamaduni katika zama ambapo ardhi ya Bara Arabu ilikuwa na watu wachache waliokuwa wakijua kusoma na kuandika huku akthari ya watu wake wakiwa wameghariki kwenye lindi la ujinga na ujahilia.
Ilikuwa ni katika anga na mazingira hayo Mwenyezi Mungu Mola mwenye hekima alimteremshia aya ya kwanza ya Qur'ani iliyozungumzia kusoma na kalamu, kalamu ambayo alikuja kuiapia pia katika aya nyingine ya kitabu hicho cha mbinguni na akaitangaza risala na ujumbe wa Nabii wake huyo wa mwisho kuwa ni kuwafundisha watu kitabu na hikma; watu ambao waliishi kwenye ulimwengu wa ujinga na upotofu, lakini muda si mrefu baadaye, wakaweza kuasisi utamaduni na ustaarabu adhimu wa Kiislamu uliong'ara duniani.
Tukiendelea na maudhui ya akhlaqi za kiutamaduni za Uislamu, sifa nyingine inayozipambanua na kuzipa hadhi ya kipekee akhlaqi hizo ni kuambatanisha pamoja elimu na imani.
Katika sehemu ya mwisho ya aya ya 11 ya Suratul-Mujaadalah Qur'ani tukufu inasema: "…Mwenyezi Mungu atawainua walio amini miongoni mwenu, na walio pewa ilimu daraja za juu. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda".
Kutokana na aya hii tunaweza kubaini kwa uwazi, jinsi elimu na imani zisivyoweza kutenganika.
Tajiriba na uzoefu wa historia pamoja na matukio yanayojiri katika zama zetu hizi vimeonyesha kuwa, kutenganishwa elimu na imani kunasababisha hasara na madhara yasiyoweza kufidika. Lakini mbali na hilo, imani inapotokana na elimu na utambuzi husalimika na khurafa na mambo ya uzushi. Wakati elimu inapotenganishwa na kuwekwa mbali na imani, imani huwa kitu cha ukereketwa, taasubi na fikra mgando; na kumuelekeza mtu kwenye upotofu na njia isiyo na lengo. Kwa upande mwingine, elimu isipoandamana na imani huwa ni sawa na kumkabidhi silaha mtu mwovu; au huwa ni sawa na taa inayokabidhiwa kwa mwizi stadi katika usiku wa giza, ili akaitumie kuporea vitu vyenye thamani kubwa.
Mwanafikra na mwanafalsafa mkubwa wa Kiislamu, Shahidi Ayatullah Murtadha Mutahhari ametupa mtazamo mwingine wa taswira ya hekima kubwa kuhusu mchango wa pamoja wa elimu na imani, alipoeleza yafuatayo katika moja ya maandiko yake: "Elimu inatupatia mwangaza na uwezo; na imani inatoa upendo na matumaini. Elimu inatengeneza wenzo; na imani inatufikisha tuendako. Elimu inaongeza kasi; na imani inaonyesha muelekeo. Elimu ni kuweza; na imani ni kutaka mazuri…Elimu ni mapinduzi ya nje na imani ni mapinduzi ya ndani ya nafsi. Elimu inaifanya dunia iwe ya wanadamu na imani inaifanya iwe ya utu…Elimu inayatengeneza maumbile na imani inamtengeneza mtu…Elimu ni jamali ya akili na imani ni uzuri wa roho. Elimu ni uzuri wa fikra na imani ni uzuri wa hisia…Elimu ni usalama wa nje na imani ni usalama wa ndani ya nafsi. Elimu inatoa kinga dhidi ya hujuma za maradhi, mafuriko, matetemeko ya ardhi na vimbunga; na imani inatuhifadhi na misongo ya mawazo, upweke, kujiinamia, hofu ya kukosa pa kukimbilia na kuhisi maisha hayana maana yoyote."
Kwa hiyo kutokana na yote haya, kuna ulazima wa elimu na imani kuwa bega kwa bega na kuchangia kwa pamoja pande zote za maisha. Umuhimu wa jambo hili ni mkubwa kiasi kwamba Imam Sajjad (AS) alikuwa akisema: "Laiti kama watu wangekuwa wanajua kuna thamani gani katika kujifunza elimu na ujuzi, basi wangefanya juhudi kwa ajili ya hilo, hata kama ni kwa kumwaga damu zao au kwa kulazimika kuzamia kwenye vina vya bahari". (Al Kafi, Kitaabu Fadhlil-ilm)
Moja ya matunda yanayopatikana kwa kuungana elimu na imani katika utamaduni wa Kiislamu ni kuifanya elimu iwe na jukumu na masuulia. Mwanasayansi au alimu ambaye hainufaishi jamii yake kwa elimu aliyonayo kwa kuwataalamisha na kuwaelimisha watu, au akawa hafanyi juhudi za kuitoa jamii hiyo kwenye lindi la ujinga; kwa mtazamo wa mfumo wa akhlaqi za kiutamaduni za Uislamu, si tu elimu ya mtu kama huyo haina thamani yoyote, lakini pia inakemewa na kukosolewa vikali.
Kuhusu tabia waliyokuwa nayo baadhi ya maulamaa wa Kiyahudi ya kutotekeleza itakiwavyo masuulia yao ya kielimu, aya ya tano ya Suratul-Jumu'a inasema: "Mfano wa walio bebeshwa Taurati kisha wasiibebe, ni mfano wa punda, anaye beba vitabu vikubwa vikubwa."
Kwa mujibu wa Hadithi, sababu hasa inayowafanya maulamaa na wataalamu kama hao kuwa na sifa hiyo chafu ni kutekwa na vivutio na mapambo ya dunia kunakowafanya waitumie elimu yao kama wenzo wa kujidhaminia maslahi yao.
Imam Jaafar Sadiq (AS) ambaye alikuwa ruwaza na kigezo kilichokamilika cha elimu na imani amelizungumzia hilo kama ifuatavyo: "Mumuonapo alimu mpenda dunia msimpe thamani katika jamii (na jueni kwamba anajionyesha tu kuwa mtu wa dini) kwa sababu kila mtu hushughulishwa na kile akipendacho". Kisha mtukufu huyo akaongezea kwa kusema: "Mwenyezi Mungu alimteremshia wahyi Nabii Daud ya kwamba, usimweke baina yangu na wewe mwanazuoni mpenda dunia, atakuweka mbali na waliojikurubisha na Mimi; kwa sababu wanazuoni hao ni maharamia wanaowateka waja wanaonitafuta Mimi". Al Kafi- Kitabu Fadhaailul-Ilm)
Sababu nyingine inayowafanya baadhi ya maulamaa waache kutekeleza masuulia yao ya kielimu ni kujikumbatisha na wenye madaraka katika ulimwengu wa siasa. Maulamaa kama hao huzitumia elimu zao kama bidhaa na nyenzo za kuwatumikia wenye uchu wa madaraka na kugeuzwa vikaragosi na vibaraka wa watu hao. Huwa tayari kutii na kutekeleza amri yoyote wanayopewa na wenye madaraka hata kama itakuwa na madhara kwa jamii, kwa sababu wameshajisabilia kuwa watumwa wa watu hao.
Bwana Mtume Muhammad SAW amesema: "maulamaa wa dini ni waaminiwa wa Mitume madamu hawajapenda dunia". Akaulizwa Bwana Mtume. Yaa RasulaAllah, nini maana ya wao kupenda dunia? Akasema: Ishara yake ni pale watakapowatii watawala (katika ulimwengu wa madaraka na siasa). Basi mtakapowaona wamejiweka karibu na wenye madaraka ziwekeni mbali safu zenu na wao". Na kwa Hadithi hiyo ya Bwana Mtume SAW, niseme pia kuwa, sehemu ya 34 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 35 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/