Hikma za Nahjul Balagha (2) + SAUTI
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu ya pili ya mfululizo wa makala fupi fupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo tutazungumzia madhara ya tamaa.
Wasikilizaji wapenzi, tunakianza kipindi chetu leo kwa moja ya semi muhimu za Imam AS aliposema:
أَزْرَى بِنَفْسِهِ مَنِ اسْتَشْعَرَ الطَّمَعَ، وَ رَضِیَ بِالذُّلِّ مَنْ کَشَفَ عَنْ ضُرِّهِ، وَ هَانَتْ عَلَیْهِ نَفْسُهُ مَنْ أَمَّرَ عَلَیْهَا لِسَانَه
Ameidhalilisha nafsi yake anayetanguliza mbele tamaa. Na ameridhia kudhalilishwa anayetangaza kiholela shida zake. Na amejidunisha nafsi yake kila anayeongozwa na ulimi wake.
*******
Mwanadamu amepewa heshima kubwa na Mwenyezi Mungu kutokana na kwamba yeye ni khalifa wa Allah katika ardhi. Ni kwa sababu hiyo ndio maana hana ruhusa kivyovyote vile kujidhalilisha na kujidunisha. Mtu yeyote hana haki ya kuitia majaribuni heshima ya wenzake kwa ajili ya kufikia maisha chapwa na dhalili ya kidunia. Haruhusiwi yeyote kusema uongo, kuwachongea wafanyakazi wenzake, kuhodhi mali ili wenziwe wasipate, kuiba na kufanya ubadhirifu wa mali ya umma, kufanya ubaguzi wa kikaumu na kikabila, ubakhili na kuzuia kuwafikia wengine neema aliyo nayo, kuacha kutenda uafilifu kwa uluwa na nguvu za kiutawala na maovu mengine yote yanayokanyaga heshima yake na ya wengine. Ni kwa sababu ya umuhimu mkubwa wa suala hili ndipo leo tumeamua kunukuu usemi huu wa Imam Ali Bin Abi Talib AS katika kitabu cha Nahjul Balagha ambapo amesema:
أَزْرَى بِنَفْسِهِ مَنِ اسْتَشْعَرَ الطَّمَعَ، وَ رَضِیَ بِالذُّلِّ مَنْ کَشَفَ عَنْ ضُرِّهِ، وَ هَانَتْ عَلَیْهِ نَفْسُهُ مَنْ أَمَّرَ عَلَیْهَا لِسَانَه
Ameidhalilisha nafsi yake anayetanguliza mbele tamaa. Na ameridhia kudhalilishwa anayetangaza kiholela shida zake. Na amejidunisha nafsi yake kila anayeongozwa na ulimi wake.
Katika hikma yake hii iliyojaa nuru, Imam Ali AS amegusia magonjwa matatu ya nafsi ambayo ni tamaa, kukosa subira na kuropoka, magonjwa ambayo mara zote hushusha hadhi ya mtu.
Tamaa maana yake ni kupenda makuu na kutamani kuwa na kitu zaidi ya mtu anavyostahiki. Mtu anayependa mali kupindukia, cheo na anasa za kidunia, hutekwa na ladha za kupita za dunia kiasi kwamba, huwa yuko tayari kufanya chochote kwa ajili ya kufikia japo kiasi kidogo tu cha ladha za dunia. Wakati kwa cheo alichopewa mwanadamu na Muumba wake, anachotakiwa kufanya mja huyo ni kutegemea moja kwa moja kwenye chanzo hicho kikuu cha kheri na ladha zote na kutoiruhusu nafsi yake kujidhalilisha mbele ya ladha za kupita za kidunia.
Baadhi ya wakati ni wajibu kwa mtu kufumba mdomo wake na kutabasamu tu mbele ya watu wanaomsemeza. Mara nyingi mtu anapoelezea matatizo yake kwa kila mtu, huishia kudharauliwa na watu hao kwani ni wachache wanaoweza kuonesha angalau nia ya kumsaidia. Tab'an hapa hatusemi kuwa mtu asimueleze yeyote matatizo yake. Kwa mfano mtu anapokwenda kwa daktari, ni wajibu wake kumueleza kiundani matatizo aliyo nayo ili aweze kumpa dawa za kumuondolea matatizo hayo. Baadhi ya wakati mtu ana wajibu wa kumueleza rafiki yake mwaminifu matatizo yake ili kupata ushauri. Lakini mtu kuifanya ndio tabia yake kutangaza matatizo yake kwa kila mtu, hilo halikubaliki kabisa na ndio ugonjwa uliokemewa hapa na Imam Ali AS.
Baadhi ya wakati neno moja tu lisilo la mahala pale, linaweza kusababisha maafa makubwa. Hivyo inabidi mtu awe macho katika maneno yake. Katika dunia yetu ya leo, adui amekaa tayari tayari kutumia vibaya udhaifu wa mtu. Hivyo katika sehemu ya mwisho ya usemi wake uliojaa hikma, Imam Ali AS anasema: Na ameidunisha nafsi yake kila anayeongozwa na ulimi wake. Lengo la Imam Ali AS hapa ni ule ulimi ambao haudhibitiwi na akili. Ulimi usio na breki. Historia imenukuu matukio mengi yaliyoishia kwenye mauaji na umwagaji damu za watu wasio na hatia kutokana na kutamkwa neno moja.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.