Jumatatu Juni 13, 2016
Leo ni Jumatatu tarehe 7 Ramadhani 1437 Hijria sawa na Juni 13, 2016.
Siku kama ya leo miaka 1440 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Abu Twalib ami ya Mtume Muhammad (SAW) na baba wa Imam Ali (A.S) alifariki dunia. Abu Twalib alikuwa pamoja na Waislamu wengine huko katika Shiibi Abi Twalib akimlinda na kumhami mtukufu huyo mbele ya adha za washirikina. Mtume Muhammad (SAW) alikuwa chini ya uangalizi wa Abu Twalib tangu alipokuwa na umri wa miaka minane, baada ya kuaga dunia babu yake, Abdul Muttalib. Abu Twalib alisilimu baada ya kubaathiwa Mtume na alikuwa muungaji mkono na mtetezi mkubwa wa Mtume Mtukufu dhidi ya washirikina wa Kikuraishi.
Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita sawa na tarehe 13 Juni mwaka 1944, kombora la kwanza la ardhi kwa ardhi la Ujerumani ya Kinazi lililojulikana kwa jina la V-1 lilishambulia ardhi ya Uingereza, katika Vita vya Pili vya Dunia. Kabla ya hapo Ujerumani ilikuwa ikiishambulia ardhi ya Uingereza kwa njia ya anga. Baada ya vita hivyo, nchi nyingine duniani zilitengeneza makombora ya aina hiyo kwa teknolojia ya kisasa zaidi.
Miaka 110 iliyopita katika siku kama hii ya leo, chama cha Sinn Féin kilianzishwa kama tawi la kisiasa la jeshi la Warepublican wa Ireland katika kisiwa cha Ireland, magharibi mwa Uingereza. Ireland ilikuwa koloni la Uingereza na chama hicho kiliasisiwa kwa lengo la kupigania uhuru wa kisiwa hicho na mwandishi wa habari maarufu wa eneo hilo aliyeitwa Arthur Griffith. Baada ya kuendesha mapambano na mashinikizo mengi dhidi ya serikali ya Uingereza mwaka 1921 Ireland ya Kusini ilipata uhuru.
Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, mwafaka na tarehe 13 Juni 1921 katika miaka ya mwanzo ya usimamizi wa Uingereza huko Palestina, kulianzishwa harakati kubwa ya wananchi katika ardhi yote ya Palestina dhidi ya Wazayuni. Harakati ya wananchi hao wa Palestina ilibainisha upinzani wao dhidi ya siasa za kikoloni za Uingereza pamoja na uungaji mkono wa nchi hiyo kwa Wazayuni waliokuwa wakiishi Palestina. Katika fremu ya sera hizo za Uingereza mwaka 1923 kulikuwa na Wazayuni 35 elfu huko Palestina na kabla ya kuundwa utawala bandia wa Israel mwaka 1948 idadi hiyo ilikuwa zaidi ya laki sita.