Alkhamisi tarehe 29 Disemba 2022
Leo ni Alkhamisi tarehe 5 Jumadithani 1444 Hijria inayosadifiiana na tarehe 29 Disemba 2022.
Miaka 772 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 5 Jumadithani mwaka 672 Hijria alifariki dunia Jalaluddin Muhammad Balkhi maarufu kwa jina la Maulawi, mshairi mkubwa wa Iran katika mji wa Kunya ambao ni moja kati ya miji ya zamani ya Iran ulioko kusini mwa Uturuki ya leo.
Maulawi alihesabiwa kuwa mshairi mkubwa na maarufu zaidi katika karne ya 9 Hijria Shamsia na miongoni mwa wanafikra na wachamungu wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu.
Maulawi alizaliwa mwaka 604 Hijria Shamsia katika mji wa Balkhi kaskazini mwa Afghanistan ya sasa na baada ya muda akahamia katika mji wa Konya akiandamana na baba yake.
Baadaye alielekea Syria kwa ajili ya masomo ya juu.
Miongoni mwa vitabu muhimu zaidi vya Maulawi ni Mathnawi Maanawi, Fihi ma Fihi, Maktubat Maulana na Rubaiyyat.

Siku kama ya leo miaka 116 iliyopita, katiba ya Iran iliyokuwa imeandikwa na kuandaliwa na Bunge la kwanza la taifa ilitiwa saini na kupasishwa na mfalme wa wakati huo wa Iran Mozaffar ad-Din Shah Qajar.
Katiba hiyo ilikuwa na vipengee 51 ambapo baadaye viliongezwa vipengee 107 kama vikamilisho.
Katika kipindi cha miaka iliyofuata na katika zama za tawala mbalimbali hususan katika kipindi cha utawala wa kidikteta wa Kipahlavi, katiba hiyo ilifanyiwa marekebisho ya kimsingi. Akthari ya marekebisho hayo yalikuwa ni9 kwa madhara ya mamlaka ya wananchi na Uislamu.

Katika siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, mkataba wa kupata uhuru Jamhuri ya Ireland ulitiwa saini baina ya viongozi wa wapigania jamhuri wa Ireland na utawala wa wakati huo wa Uingereza.
Hata hivyo kutokana na kuanza Vita vya Pili vya Dunia, serikali ya Uingereza ilikataa kutekeleza mkataba huo. Baada ya vita hivyo, mnamo mwaka 1949, Jamhuri ya Ireland ya Kusini ilijitangazia rasmi uhuru wake toka kwa mkoloni Muingereza.
Uhuru wa Ireland ulikuwa matokeo ya mapambano ya karne nane ya wapigania Jamhuri wa Ireland dhidi ya Uingereza.

Miaka 92 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Theodor Nöldeke msomi wa Kijerumani na mtaalamu wa mambo ya nchi za mashariki.
Alihitimu masomo yake katika taaluma ya teolojia, falsafa pamoja na lugha mbalimbali na kutunukiwa shahada ya uzamivu. Theodor Nöldeke alianza kufundisha Chuo Kikuu akiwa na umri wa miaka 25 na kuifanya kazi hiyo kwa miaka mingi.
Theodor Nöldeke alikuwa amebobea katika lugha za Kiarabu, KIifarsi, Kituruuki, Kigiriki, Kihispania na Kitaliano.
