Dec 29, 2022 14:16 UTC

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 9 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya Tisa.

إِذَا أَقْبَلَتِ الدُّنْیَا عَلَى أَحَدٍ أَعَارَتْهُ مَحَاسِنَ غَیْرِهِ وَ إِذَا أَدْبَرَتْ عَنْهُ سَلَبَتْهُ مَحَاسِنَ نَفْسِهِ

Ulimwengu ukimpa mtu uso humkopesha mazuri ya wengine na ukimpa kisogo humpoka mazuri hayo.

Moja ya kazi nzuri na za kuvutia mno za Amirul-Mu'minin, Imam Ali (AS) katika kitabu cha Nahjul Balagha, ni maelezo na ufafanuzi wake kuhusu dunia. Dunia ina majukumu mawili, chanya na hasi, au kwa maneno mengine, jukumu la kujenga au jukumu la uharibifu. Dunia inaweza kuwa chanzo cha elimu na ujenzi, na pia inaweza kuwa chanzo cha upofu na upotofu. Ikiwa mtu anaitazama dunia kwa jicho la welewa na ufahamu, itakukpa mafunzo na ushauri mzuri, na kuyafanya maisha yako kuwa ya furaha. Lakini dunia hii hii inaweza kuwa njia ya uzembe wa mwanadamu na kuweka pazia juu ya macho yake ashindwe kuona ukweli na hatimaye kusababisha maafa na uharibifu.

Mawalii wa Mwenyezi Mungu wanaichukulia dunia kuwa ni njia ya muda na ya mpito ya kufikia Akhera na wanatumia neema na suhula za dunia kupata radhi za Mwenyezi Mungu kujijenga kinafsi na kujikurubisha kwa Mola wa Ulimwengu. Wanaichukulia furaha na kutokuwa na furaha, fedha na upungufu wa mali kuwa ni mitihani tu ya Mwenyezi Mungu na wanatumia subira na uchamungu kuipatia suluhisho mitihani hiyo, mmoja baada ya mwingine ili kuboresha maisha yao na kufikia furaha ya milele katika maisha ya baada ya hapa duniani. Lakini kwa baadhi ya watu, dunia si njia ya kufikia Akhera, bali kwao dunia ndio malengo yao ya mwisho na wanafanya juhudi zao zote kwa ajili ya mambo ya kidunia. Anasa na mapumbao ya dunia yamewaziba macho na hawazingatii maonyo na mafunzo yote ya ulimwengu. Kigezo cha hukumu zao kuhusu watu si maadili mema, wala imani na uchamungu, bali ni kiwango cha kipato chao na jaha na utajiri wao duniani. Kwa hivyo, kila mtu anapokuwa na mali na cheo, watu hao husema, dunia imempa uso na kumkubali na ikiwa mtu atakosa mali na utajiri wa kimaada, wanasema kwamba dunia imempa kisogo.

Katika hikima hii ya 9 iliyomo kwenye kitabu cha Nahjul Balagha, Imam Ali AS anavuta mazingatio yetu juu ya mabadiliko ya hali ya watu mbele ya wale ambao dunia inawakubali na wakati dunia inapowapa kisogo. Anasema: Dunia inapomkubali mtu hukopesha mazuri ya wengine na huona mambo yanamnyookea lakini wakati inapompa kisogo, humpoka na kumpokonya neema hizo ikawa kila anachokigusa hakinyooki. Hii kwa hakika ndiyo dunia.

Kauli hii ya Imam AS ina ushahidi mwingi wa kihistoria. Wapo watu wengi sana ambao wamekuwa maarufu katika serikali na siasa au katika masuala ya kijamii na kiuchumi au hata katika masuala ya kielimu na mengineyo. Lakini baada ya muda kupita, wanasahaulika kabisa huku uchunguzi na utafiti ukionesha kuwa, kazi za wengine ndizo zilizojaa kwenye faili la mtu huyo. Mmoja wa wafasiri mashuhuri wa Nahj al-Balagha, Ibn Abi al-Hadid Muutazili, katika ufafanuzi wake wa hekima hii, anasema: “Tumeona mashairi mengi mazuri ambayo kwa vile mzungumzaji wake alikuwa hajulikani, watu walimnyima haki yake na mashairi yake hayo mazuri kunasibishwa na watu mashuhuri katika tungo za kishairi. Hata katika utuungaji wa vitabu n.k, kumekuwa kukifanyika makosa ya kuwapa wengine, sifa za watu wengine. Ni hivyo hivyo katika masuala ya sanaa, sayansi, teknolojia, uvumbuzi wa vitu n.k, tumeona kazi za watu ambao si mashuhuri, wanapokwa haki hizo na kupewa watu mashuhuri imma kwa makusudi au kwa kughafilika. 

Naam! Tusitarajie kitu kingine ghairi ya hicho. Kwani wakati vigezo vikuu katika jamii vinapokuwa ni pesa, utajiri na urembo katika kuwatathmini watu, mtu ambaye ana vitu hivyo vingi zaidi yeye ndiye huonekana kuwa na mafanikio zaidi na ndiye anayependwa zaidi na wengine. Watu kama hao hawafaidiki tu na vitu vyao na vya wenzao, lakini hata watu huwafikiria kimakosa kuwa na ukamilifu wa maadili. Mfano bora ni wa watu mashuhuri wa kila jamii, ambao dunia inapowakubai , si tu historia yao mbaya haionekani na mtu yeyote, bali hata matendo yao yote watu huyaona ni mema. Pia wananasibishiwa wao kazi bora za wengine na hugeuzwa kuwa kioo na vigezo vya kimaadili na kiakili. Katika jamii kama hiyo, ikiwa mtu wa namna hiiyo mambo yatamuharibikia na kupoteza mali na hadhi na dunia ikampa kisogo, watu watamchukulia kuwa ni fedheha. Hata kama aliwatendea mema, wema wake hautakumbukwa na wengi na hata ikitokezea akawa amefanya kazi nzuri ya kisanii kwa mfano, basi kazi hiyo anaweza kunasibishwa nayo mtu mwingine mashuhuri. Ikiwa mtu huyo atazidi kupoteza utajiri wake wa mali, anaweza pia kupoteza hata marafiki na mashabiki wake. Hii ndiyo hali ya jamii ambayo kipaumbele chake kikuu ni mambo ya kidunia na ambayo inaihesabu dunia kuwa ndio kila kitu. Wakati katika jamii ambayo thamani ya mtu ni kuwa na maadili mema, akhlaki nzuri, kujitolea, uchamungu, ujuzi, nk, hali yoyote ya kimaada na kidunia inayomtokea mtu huyo huwa haiathiri kabisa heshima na hadhi yake.