Jan 29, 2023 02:34 UTC
  • Jumapili, 29 Januari, 2023

Leo ni Jumapili tarehe 7 Rajab, 1444 Hijria sawa na tarehe 29 Januari, 2023 Miladia

Miaka 1139 iliyopita katika siku kama hii, yaani mwezi saba Rajab mwaka 305 Hijria alizaliwa Ibn T'arrar, mwanafasihi Muislamu na alimu wa fani ya Hadithi. Abul Fat'h Muafi bin Zakariya bin Yahya, maarufu kama Ibn T'arrar, alikuwa mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kishafi aliyebobea katika fiqhi, fasihi, Hadithi, nahau na misamiati. Alimu huyo wa Kiislamu alialifu athari kadhaa za fiqhi. Kwa upande wa fasihi, miongoni mwa vitabu muhimu vya Ibn T'arrar ni "Al Jaliis wal Aniis" chenye majalada mia moja, baadhi yao yakianza kwa kunukuu na kusherehesha Hadithi za Mtume SAW. Ibn T'arrar aliaga dunia mwaka 390 Hijria mjini Baghdad akiwa na umri wa miaka 85.

Ibn T'arrar

Miaka 286 iliyopita, mnamo Januari 29, 1737 alizaliwa Thomas Paine, mwanasiasa na mwandishi mwanamapinduzi wa Uingereza. Baada ya kumaliza masomo yake ya elimu ya kati Paine aliamua kujishughulisha na kazi mbalimbali lakini hakufanikiwa katika yoyote kati ya hizo. Hatimaye mnamo mwaka 1774, yaani mwaka mmoja kabla ya kuanza vita vya uhuru wa Marekani aliwasili nchini humo na kuanza kazi ya uandishi. Tasnifu yake iliyoitwa "Akili Timamu" iliwaathiri mno wananchi na viongozi wa Marekani na kuimarisha azma yao ya kujikomboa kutoka kwenye makucha ya Uingereza. Baada ya uhuru wa Marekani, Thomas Paine alirejea kwao Uingereza ambako aliandika kitabu "Haki za Mtu" kutetea Mapinduzi ya Ufaransa. Kwa sababu huko Uingereza alitambuliwa kama haini, Paine alilazimika kuelekea Ufaransa ambako alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Taifa. Alifia Marekani mwaka 1809 katika hali ya simanzi na ufakiri.

Thomas Paine

Miaka 97 iliyopita, mnamo tarehe 29 Januari 1926, alizaliwa Profesa Muhammad Abdussalam, mwanafizikia mbobezi wa Pakistan katika mji wa Punjab mashariki ya nchi hiyo. Abdussalam, ambaye alizaliwa katika familia ya kidini alianza kudhihirisha mapema kipawa kikubwa alichokuwa nacho kwa kufanikiwa kuingia chuo kikuu cha Punjab akiwa na umri wa miaka 14. Na baada ya kuhitimu shahada ya pili ya Uzamili akiwa na umri wa miaka 20 alielekea chuo kikuu cha Cambridge nchini Uingereza. Baada ya kuhitimu shahada ya kwanza ya Hisabati na Fizikia, mwaka 1951, Abdussalam alihitimu shahada yake ya Uzamivu au PhD ya Fizikia na kutunukiwa tuzo ya Adams. Mwaka 1979, Profesa Muhammad Abdussalam pamoja na watafiti wengine wawili, alitunikiwa tuzo ya amani ya Nobeli na kuwa mwanasayansi wa kwanza katika Ulimwengu wa Kiislamu kushinda tuzo hiyo. Mwanasayansi huyo aliteuliwa kuwa mshauri wa masuala ya sayansi na elimu wa rais wa Pakistan kuanzia mwaka 1961 hadi 1974. Katika uhai wake, Muhammad Abdussalam alivumbua vitu kadhaa wa kadhaa na aliaga dunia mwaka 1996.

Profesa Muhammad Abdussalam

Miaka 81 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 29 Januari 1942, baada ya majeshi ya Uingereza na Urusi kuivamia ardhi ya Iran na kuuhalifu msimamo wa Iran wa kutopendelea upande wowote katika Vita vya Pili vya Dunia, makubaliano baina ya pande hizo tatu yalisainiwa. Kwa makubaliano hayo, serikali ya wakati huo ya Iran ililazimika kufungua njia na nyenzo za mawasiliano ya nchi kavu, angani na baharini kwa ajili ya kambi ya Waitifaki, yaani Allies katika vita hivyo, ili kwa kuitumia njia ya Iran kupitishia silaha na zana za kivita, iweze kuimarisha vikosi vyake vya upande wa Urusi dhidi ya Ujerumani ya Manazi. Kwa upande wao, Urusi na Uingereza ziliyatambua mamlaka kamili ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya Iran na kuahidi kwamba, katika muda usiozidi miezi sita baada ya kumalizika vita, zitaondoa majeshi yao katika ardhi ya Iran. Lakini mbali na kuisababishia nchi hii hasara zisizofidika wakati yalipokuwepo majeshi yao, pale vita vilipomalizika, sio tu Urusi haikuwa tayari kuwaondoa askari wake, lakini pia ilijaribu kufanya kila mbinu kuunda serikali kibaraka kaskazini magharibi ya Iran kwa ajili ya kuandaa mazingira ya eneo hilo kujitenga. Hata hivyo njama hiyo iligonga mwamba na jeshi la Urusi likalazimika kuondoka katika ardhi ya Iran.

Vita vya Pili vya Dunia

Na miaka 44 iliyopita, yaani tarehe 29 Januari 1979, wakati mashekhe mashuhuri wa Iran walipofanya mgomo wa kuketi ndani ya msikiti wa chuo kikuu cha Tehran kupinga na kulalamikia hatua ya utawala wa Shah kumzuia Imam Khomeni (MA) asiingie nchini, umati mkubwa wa wananchi ulimiminika mabarabarani kuelekea msikiti huko. Katika miji mingine ya Iran pia waandamanaji waliokuwa wakitoa nara na kaulimbiu za “Allahu Akbar, Khomeini Kiongozi”, walitaka utawala wa kidikteta wa Shah uangushwe na Imam Khomeini arejee nchini. Askari wa utawala wa Shah waliingilia kati tena kuwatawanya wananchi mjini Tehran ambapo katika makabiliano hayo, Waislamu wanamapambano wengi wa Iran waliuliwa shahidi na kujeruhiwa.

Mgomo wa kitako wa Mashekhe katika msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran

 

 

Tags