Jumatatu, Juni 2, 2025
Leo ni Jumatatu tarehe 06 Mfunguo Tatu Dhulhija 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe Pili Juni mwaka 2025 Milaadia.
Katika siku kama ya leo miaka 1188 iliyopita, alizaliwa Abu Ali Muhammad ibn Hammam, mmoja wa maulama mashuhuri wa Iran.
Ibn Hammam alikuwa akiishi mjini Baghdad, Iraq ambapo alifanikiwa kusoma elimu ya hadithi kutoka kwa maulama wakubwa wa enzi zake. Msomi huyo pia alikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao walijifunza kwake elimu ya Hadithi na elimu nyingine za Kiislamu. Abu Ali Muhammad ibn Hammam ameacha vitabu kadhaa katika taaluma ya Hadithi.

Katika siku kama hii ya leo miaka 143 iliyopita alifariki dunia Giuseppe Garibaldi kamanda mzalendo na kiongozi wa harakati ya umoja wa Italia.
Giuseppe alizaliwa mwaka 180 na wakati wa ujana wake alifanya kazi mbalimbali na mwishowe kujiunga na jeshi. Baadaye alichaguliwa kuwa kamanda wa wanaharakati wa kupigania uhuru wa Italia na alifanya jitihada nyingi za kuleta umoja nchini humo.
Kwa ajili hiyo alijulikana katika historia ya Italia kama shujaa wa taifa.

Siku kama ya leo Miaka 55 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim, mkuu wa kituo cha kidini cha Najaf aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92.
Baada ya kuaga dunia Ayatullah Burujerdi ambaye alikuwa mar'ja' mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, Ayatulah Hakim alichukua nafasi yake na kufuatwa na Waislamu wengi na hasa wa Iraq, kuhusiana na masuala ya kifik'hi. Alipambana vikali na kila kundi au watu waliojaribu kuharibu jina la Uislamu.
Fatua yake mashuhuri ya kupinga fikra ya ukomunisti dhidi ya mafundisho ya dini ilileta mabadiliko makubwa nchin Iraq. Fatua hiyo pia ilimpelekea kutoa amri ya kupigana jihadi dhidi ya utawala haramu wa Israel.
Ujenzi wa maktaba, shule na vituo vya kidini na kiutamaduni pamoja na uandishi wa vitabu kama vile Mustamsak Urwat al-Wuthqah na Nahjul Faqaha ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vilivyoandikwa na mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu. *

Miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 12 Khordad mwaka 1379 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Hujjatul Islam Sayyid Ali Akbar Abuturabi, mwanzuoni mwenye mwamko na mwanaharakati wa Iran katika ajali ya gari pamoja na baba yake Ayatullah Sayyid Abbas Abuturabi.
Hujjatul Islam Sayyid Ali Akbar Abuturabi alizaliwa mwaka 1318, kwa mujibu wa kalenda ya Iran, katika mji wa kidini wa Qum. Alijifunza elimu ya dini kutoka kwa maulamama wakubwa akiwemo Imam Khomeini (M.A). Hujjatul Islam Abuturabi katika mapambano ya kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu mara kadhaa alikamatwa na kuteswa na vibaraka wa Shah.
Wakati vya vita vya Iran na Iraq mwaka 1359 alikamatwa mateka na askari wa utawala wa Baath wa Iraq na kufungwa kwa miaka 10 katika jela zenye mateso makali za Iraq. Lakini alivumilia kiasi cha kuwa mashuhuri miongoni mwa mateka wa Iran kwenye jela hizo. Alipoachiliwa huru aliteuliwa kuwa mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya mateka na walioachiliwa huru.
