Mchango wa Maulamaa (64)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha kila juma cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu. Kipindi chetu cha juma lililopita kilitupia jicho kwa mukhtasari historia na maisha ya Sayyid Ali Akbar Fal Asiri, alimu na mwanazuoni mwengine mahiri na mashuhuri wa Kishia ambaye mchango wake una nafasi muhimu mno katika ulimwengu wa Kiislamu.
Tulisema kuwa, Sayyid Ali Akbar Fal Asiri alizaliwa 1256 Hijria katika kijiji cha Asir kilichoko katika viunga vya mji wa Lamerd. Tuliona jinsi alivyoongoza harakati ya kupinga ughali wa mkate na jinsi alivyofanikiwa katika harakati hiyo pamoja na mchango wake mkubwa huko Shiraz kama ambavyo alikuwa na nafasi muhimu katika harakati ya kupinga kuhodhiwa sekta ya tumbaku nchini Iran. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 64 ya mfululizo huu kitamzungumzia Mirza Ashtiyani. Nina wingi wa matumaini kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi.
Muhammad Hassan Ashtiyani au Mirza Ashtiyani alizaliwa 1248 Hijria katika eneo la Ashtiyan liililo jirani na mji mtakatifu wa Qom Iran. Muhammad Hassan kama alivyokuwa Mirza Shirazi naye alimpoteza baba yake aliyefariki dunia wakati yeye ana umri wa miaka mitatu na hivyo kuonja ladha chungu ya maisha ya uyatima. Muhammad Hassan alilelewa na mama yake aliyesifika kwa uchamungu na aliyekuwa na mapenzi makubwa na watu wa nyumba ya Bwana Mtume (saw) na hivyo maisha yake kupitia katika mkondo wa maariifa ya dini. Mama yake alimpeleka katika walimu wa dini huko Ashtiyan na Muhammad Hassan akashiriki masomo katika eneo alilozaliwa mpaka alipofikisha umri wa miaka 13. Baada ya hapo alifunga safari na kuelekea Borujerd kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Katika zama hizo, Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Borujerd kilikuwa chuo amilifu, hai zaidi na mashuhuri zaidi miongoni mwa vyuo vya Kishia. Akiwa katika chuo hicho Muhammad Hassan au Mkirza Ashtiyan kama anavyojulikana pia, alisoma fasihi, fikihi na Usul mpaka akafikia daraja ya kuwa mwalimu na kuanza kufundisha huku akiwa hajafikisha miaka 17. Hii ni katika hali ambayo, wanafunzi wake walikuwa wamemzidi umri huku wengine wakiwa ni watu wazima.

Hata hivyo shauku na hamu ya kuwa jirani na Imam Ali bin Abi Twalib (as) vilimfanya afunge safari na kuelekea katika mji wa Najaf huko Iraq kwa ajili ya kujiimarisah zaidi kielimu na kimaarifa. Safari yake iliambatana na mashaka na taabu nyingi, kwani akiwa njiani alipata maradhi na kuugua sana. Hata shauku ya kujifunza na kuhudumia maktaba ya Ahlul-Beiti (as) ilimzuia kukatisha safari yake na kurejea. Mirza Ashtiyani aliwasili katika Haram ya Imam Ali bin Abi Twaliib (as) akiwa na homa kali. Baada ya kufanya ziara na kuomba dua, aliondoka katika Haram hiyo takatifu na hivyo kuanza kukata masafa katika njia ngumu ya kutafuta elimu akiwa mbali na kwao na familia yake.
Ukiacha Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as), Mirza aliyekuwa kijana wakati huo alikuwa akihisi ugeni katika maeneo mengine yote ya mji wa Najaf. Maradhi aliyokuwa akiigua yaliongeza maradufu upweke wa ugenini. Wakati anatoka katika Haram ile kwa bahati njema na kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu alikutana na mmoja wa marafiki wakongwe wa marehemu baba yake ambaye kwa miaka mingi alikuwa kiishi katika mji wa Najaf. Bwana yule alimchukua Muhammad Hassan hadi nyumbani kwake na kumuandalia mazingira ya kuishi pamoja na masomo. Kinyume na matarajio, baada ya muda mfupi tu, Mirza Ashtiyan alipona maradhi yake na kuanza ukurasa mpya wa kusoma na kutafuta elimu katika mji wa Najaf. Alianza kushiriki masomo ya Sheikh Murtadha Ansari. Sheikh Murtadha Ansari ni mmoja wa Maulamaa mahiri na watajika na mafakihi stadi katika karne ya 13 Hijria.
Katika Hawza ya Najaf, wanafunzi wote wa Sheikh Murtadha Ansari walikuwa wamemzidi umri, kiasi kwamba, kutokana na haya na soni alikuwa akilazimika kukaa nyuma ya pazia wakati wa kusoma na kumsikiliza mwalimu. Siku moja Muhammad Hassan aliuliza swali. Sheikh Murtadha Ansari alihamisika mno na swali la mwanafunzi wake huyu lililokuwa limejaa tafakuri na hivyo akagundua kipaji kikubwa na maarifa ya hali ya juu aliyokuwa nayo mwanafunzi wake huyu. Ni kuanzia hapo ambapo Sheikh Murtadha Ansari akawa akimpa umuhimu mwanafunzi huyo kijana.

Muhammad akawa na safari za kwenda na kurudi katika nyumba ya Sheikh Murtadha Ansari akiwa mwanafunzi wake maalumu. Ikafikia wakati Sheikh Murtadha Ansari akawa akiwatuma wanafunzi wengine kwa Mirza Ashtiyani ili wakaulize maswali na kupatiwa ufumbuzi mahali walipokwama na ambapo hawajaelewa wakati mwalimu akifundisha. Kutokana na Muhammad Hassan kuwa na lugha nzuri ya ubainishaji na kunukuu vyema yaliyokuwa yakifundishwa na Sheikh Murtadha Ansari akaondekea kuwa mashuhuri kwa jina la msemaji na mfafanuzi wa Sheikh.
Mwaka 1281 Hijria, baada ya kufariki dunia Sheikh Murtadha Ansari, Mirza Ashtiyani na wanafunzi wengine wa alimu huyo walishauriana na kufikia natija ya kumchagua Mirza Ashtiyani kuwa Marjaa na kiongozi wa Mashia ulimwenguni. Ni baada ya tukio hilo ndipo Mirza Ashtiyani akawa amekusudia kurejea Iran na hiki ndicho kile kipindi ambacho, Naser al-Din Shah mfalme wa nne katika ukoo wa Qajar Iran alikuwa amewapatia upendeleo mwingi Wamagharibi na alikuwa akitambua vyema kwamba, kuwa na welewa na kuweko na umoja na mshikamano baina ya wananchi ni jambo hatari kwake. Naser al-Din Shah alikuwa akihofia mno nguvu ya kijamii ya Maulamaa kwani alikuwa akitambua vyema kwamba, Maulamaa ndio mhimili mkuu wa umoja na mshikamano wa watu katika jamii.
Kinyume na matakwa ya Shah, Mirza Ashtiyani ambaye alikuwa tayari ni Mujtahidi mashuhuri na aliyekuwa na heshima ya hali ya juu miongoni mwa watu, aliingia Tehran kwa mapokezi makubwa na yaliyojaa hamasa. Kisha akaanzisha Chuo Kikuu cha Kidini mjini Tehran na akaanza kujishughulisha na kazi ya kufundisha na kulea wanafunzi. Kila siku idadi ya wanafunzi waliokuwa wakihudhuria masomo yake ilikuwa ikiongezeka sambamba na mapenzi makubwa ya watu kwa alimu na mwanazuoni huyu. Mbali na kuwa mahiri na makini mno katika ufundishaji alifahamika vyema kama mtu mwenye kipaji cha hali ya juu cha kuzungumza kilichoambatana na ufasaha na ubainishaji mzuri. Ni kutokana na hilo, ndio maana hakuwa na mithili katika zama hizo katika kuwafikishia wanafunzi maudhui mbalimbali za masomo.

Moja ya sifa maalumu ya Mirza Ashtiyani ni uzingatiaji wake wa hali ya juu kuhusiana na masuala ya kijami ya Waislamu. Alikuwa akiamini kuwa, kuleta mageuzi katika jamii na kushughulikia matatizo ya watu ni jukumu la alimu na msomi wa dini na hakusita kutoa gharama ya hali na mali na hata heshima katika njia hii.
Mirza Muhammad Ashtiyani alikuwa mwanzisghi wa harakati ya kuharamishwa tumbaku. Baada ya mtawala Naser al-Din Shah kulipatia shirika moja la Uingereza haki ya kuhodhi sekta yote ya tumbaku, Mirza Muhammad Ashtiyani alimuandikia barua kadhaa mtawala huyo na hata kubainisha upinzani wake katika vikao mbali na kiongozi huyo, lakini Shah alipuuza yote hayo.
Mirza Ashitayni ambaye alisoma pamoja na Mirza Shirazi kwa Sheikh Murtadha Ansari, alimuandikia barua Marjaa huyo wa Kishia ambapo sambamba na kubainisha hali ya mambo alimtaka aingilie suala hilo akiwa Marjaa wa Kishia.
Mbali na barua hiyo, Miirza Shirazi alikuwa amepokkea pia barua nyingine zikimtaka achukue hatua.
Hatimaye mwaka 1308 Hijria, Mirza Shirazi alitoa fatuwa ya kuharamisha matumizi ya tumbaku kwa namna yoyote ile.
Kufuatia fatuwa hiyo ambayo maneno yake hayakuwa yakizidi hata mstari mmoja, wananchi wote Waislamu wa Iran, wake kwa waume, wakubwa kwa wadogo, wasomi, wafanyabiashara, wananchi wa kawaida na hata wasiokuwa Waislamu walitii fatwa hiyo kwa kutotumia tumbaku kwa njia yoyote ile na hivyo wakawa wamesimama dhidi ya mkoloni Muingereza na kuanzisha harakati ya pamoja dhidi ya mkataba wa tumbaku au mkataba wa Talbot.
Mbali na harakati za kijamii na kisiasa, Mirza Muhammad Ashtiyani hakuwa nyuma pia katika kualifu na kuandika vitabu. Kitabu chake muhimu zaidi ni Bahrul-Fawaid. Wanahistoria wanasema kuwa, Ashtiyani ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kueneza fikra na mitazamo ya mwalimu wake nchini Iran yaani Sheikh Murtadha Ansari.
Katika upande wa ibada na uchaji Mungu, Ayatulllah Ashtiyani alikuwa na hima na bidi kubwa na katu hakuwa akiacha kusoma Ziyart Ashura, Swala ya usiku na sunna nyingine. Hatimaye baada ya miaka mingi ya hima na huduma alimu huyo aliaga dunia mjini Tehran na kwenda kuzikwa huko Najaf Iraq.
Kwa leo tunakomea hapa kutokana na kumalizika muda wa kipindi chetu. Msisite kujiunga nami wiki ijayo.
Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.