Jun 19, 2016 01:25 UTC
  • Jumapili, Juni 19, 2016

Leo ni Jumapili tarehe 13 Ramadhan 1437 Hijiria, sawa na tarehe 19 Juni 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1342 iliyopita inayosadifiana na tarehe 13 Ramadhani mwaka 95 Hijria, alifariki dunia Hajjaj bin Yussuf Thaqafi liwali katili na dhalimu wa Iraq katika kipindi cha utawala wa Bani Umayyah. Hajjaj bin Yussuf Thaqafi aliyeishi katika kipindi cha wafalme wa Bani Umayyah, Abdul Malik Marwan na Hisham bin Marwan, alikuwa katili na mashuhuri kwa kuwatesa na kuwaua wapinzani wa utawala wa Bani Umayyah, na hasa wafuasi wa Imam Ali bin Abi Talib AS na watu wa familia ya Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Baadhi ya wanahistoria wameandika kuwa, zaidi ya watu 120,000 waliuawa kutokana na amri iliyotolewa moja kwa moja na Hajjaj bin Yussuf Thaqafi. Miongoni mwa jinai zilizowahi kufanywa na Hajjaj bin Yusuf Thaqafi ni kuushambulia mji mtakatifu wa Makka na kuharibu al Kaaba mwaka 74 Hijria.
Siku kama ya leo miaka 149 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Juni 1867, Maximilian mwana wa mfalme wa Austria ambaye aliikalia kwa mabavu Mexico, alinyongwa na wapigania uhuru wa nchi hiyo. Baada ya Benito Juarez kuchukua urais wa Mexico mwaka 1855, aliwakata mikono wazungu na kupunguza nguvu za Kanisa nchini Mexico. Hatua hiyo iliwakasirisha mno wazungu na wakoloni wa Ulaya waliokuwa wakiongozwa na Ufaransa, na kulazimika kutuma jeshi nchini Mexico kwa shabaha ya kulihami Kanisa pamoja na mabepari wa Ulaya nchini humo.
Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita, Enrico Forlanini mhandisi wa Kiitalia alifanikiwa kufanya majaribio ya kwanza ya kurusha angani helikopta katika mji wa bandari wa Alexandria nchini Misri. Helikopta hiyo iliboreshwa zaidi na mtaalamu Mpoland, na ubunifu huo ukaandikwa kwa jina lake.
Siku kama ya leo miaka 109 iliyopita, alifariki dunia Jahangir Khan Qashqai, faqihi, mwanafalsafa na mtaalamu wa elimu ya irfani wa Iran. Qashqai alizaliwa katika jimbo la Qashqai, katikati mwa Iran na kuanza kujifunza elimu ya dini katika jimbo hilo ambapo alifikia daraja za juu. Baadaye alielekea mjini Isfahan, moja ya miji mikubwa ya Iran ambapo alijishughulisha na masomo ya akhlaqi na kuondokea kuwa kuwa alimu mkubwa ambaye baada ya hapo alianza kazi ya kulea wanafunzi. Msomi huyo alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 85 na akazikwa katika mji huo wa Isfahan.
Na siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, Houari Boumediene, makamu wa rais na waziri wa ulinzi wa wakati huo wa Algeria, aliongoza mapinduzi ya kijeshi yasiyo ya umwagikaji wa damu na kumuondoa madarakani Rais Ahmed Ben Bella na kutwaa uongozi wa nchi hiyo kwa nguvu. Boumediene alikuwa akiongoza jeshi la kupigania uhuru la Algeria katika harakati za mapinduzi za nchi hiyo dhidi ya wakoloni Wafaransa. Baada ya mapinduzi na uongozi wa nchi kuchukuliwa na Ben Bella, pole pole kuliibuka tofauti baina ya marafiki hao wa zamani, tofauti ambazo ziliishia kwenye mapinduzi ya kijeshi dhidi ya muitifaki wake huyo.