Mar 26, 2023 02:41 UTC
  • Jumapili, 26 Machi, 2023

Leo ni Jumapili tarehe 4 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1444 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 26 Machi 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 867 iliyopita, alifariki dunia Muhammad bin Muhammad maarufu kwa jina la Ibn Khorasani, mtaalamu wa lugha, malenga na mwandishi wa Baghdad. Ibn Khurasani alizaliwa mwaka 494 Hijria huko Khurasan, kaskazini mashariki mwa Iran. Msomi huyo baadaye alielekea Baghdad, Iraq na kuishi katika mji huo. Muhammad bin Muhammad alihitimu masomo kwa walimu mashuhuri wa zama hizo. Ibn Khurasan ameandika mashairi mengi ambayo mengi kati ya hayo yamepotea. ***

Ibn Khorasani

 

Katika siku kama hii ya leo miaka 112 iliyopita alizaliwa mwandishi mashuhuri wa michezo ya kuigiza wa Marekani, Tennessee Williams. Alivutiwa sana na fasihi na mvuto huo ulikolea na kuimarika zaidi wakati alipokuwa masomoni katika chuo kikuu na hatimaye alifanikiwa kuwa mwandishi mkubwa. Tennessee Williams alitumia uhodari wake kueleza fikra zake kwa lugha ya michezo ya kuigiza. Kazi zake nyingi zilieleza hali ya watu wa tabaka la chini na wanaosumbuliwa na ukata katika jamii ya Marekani. Miongoni mwa kazi za mwandishi huyo mashuhuri ni Cat on a Hot Tin Roof, Sweet Bird of Youth na The Glass Menagerie. ***

Tennessee Williams.

 

Miaka 71 iliyopita katika siku kama ya leo, yalianza mapambano ya Mau-Mau yakiongozwa na Mzee Jomo Kenyatta, mwasisi wa nchi huru ya Kenya, dhidi ya wakoloni wa Kiingereza. Katika kipindi cha vita viwili vikubwa vya dunia, Kenya ilikumbwa na machafuko na vurugu nyingi. Hata hivyo baada ya Vita vya Pili vya Dunia, wananchi wa nchi hiyo waliamua kupambana kufa na kupona ili kuikomboa nchi yao kutoka mikononi mwa wakoloni wa Ulaya. Wakoloni wa Kiingereza waliweka sheria kali katika maeneo tofauti ya Kenya hasa katika maeneo ya Wakikuyu lakini hilo halikuzuia kuasisiwa harakati ya Mau-Mau. Kaulimbiu kuu ya wapiganaji wa Mau-Mau ilikuwa ni kuweko usawa na uadilifu katika masuala ya kijamii na kisiasa baina ya wenyeji wa Kenya na Wazungu. Hatimaye harakati hiyo ya Mau-Mau kwa uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta ilifanikiwa kuikomboa Kenya kutoka mikononi mwa wakoloni wa Kiingereza mwanzoni mwa muongo wa 60. ***

Mzee Jomo Kenyatta

 

Tarehe 26 Machi mwaka 1971 katika siku kama hii ya leo, Pakistan Mashariki ambayo hivi sasa inajulikana kwa jina la Bangladesh iliamua kujitenga na Pakistan baada ya kuzuka mivutano mikubwa ya kisiasa na uasi nchini humo. Pakistan Mashariki na ile ya Magharibi ilikuwa nchi moja, iliyoamua kujitenga na India mwaka 1947. Wabangladeshi waliokuwa wakiishi Pakistan Mashariki na kuunda jumla ya asilimia 98 ya watu wa eneo hilo, hawakuridhishwa na vitendo vya kibaguzi vilivyokuwa vikifanywa na serikali kuu huko Pakistan Magharibi na kwa msingi huo awali walitaka kupewa mamlaka ya kujiendeshea mambo yao wenyewe. Baadaye walianzisha mapambano ya silaha na kufanikiwa kulifukuza jeshi la Pakistan Magharibi wakisaidiwa na jeshi la India. Pakistani Mashariki ilipewa jina la Bangladesh. ***

Bendera ya Bangladesh

 

 Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Ahmad Sekou Toure kiongozi mkubwa wa nchi ya Kiafrika ya Guinea. Sekou Toure alizaliwa Januari 9 mwaka 1922 katika moja ya miji ya katikati mwa Guinea. Aliingia katika harakati za kisiasa akiwa katika rika la ujana na alikuwa akitaka uhuru wa  chi yake kutoka kwa wakoloni wa Kifaransa. Hatimaye mwaka 1958 nchi hiyo ilipata uhuru na mwaka mmoja baadaye Touré akateuliwa kuwa rais na kusalia madarakani hadi mwaka 1984 alipofariki dunia. ***

Ahmad Sekou Toure

 

Tags