Sura ya Ghaafir, aya ya 53-56 (Darsa ya 867)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 867 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 53 na 54 za sura hiyo ambazo zinasema:
وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْهُدَىٰ وَأَوْرَثْنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ الْكِتَابَ
Na kwa hakika tulimpa Musa uwongofu, na tukawarithisha Wana wa Israili Kitabu,
هُدًى وَذِكْرَىٰ لِأُولِي الْأَلْبَابِ
Ambacho ni Uwongofu na Ukumbusho kwa wenye akili.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya iliyozungumzia ahadi ya Allah SWT ya kuwapa auni na msaada na kuwanusuru Mitume wake na wafuasi wao. Aya hizi tulizosoma zinaashiria moja ya mifano hai ya msaada huo wa Allah na kueleza kwamba, wakati tulipomchagua Musa kumpa Utume tulimuongoza katika njia ya kumlingania tauhidi Firauni na Bani Israil na ya kumuabudu Mungu pekee wa haki pamoja na kutekeleza jukumu lake la Utume. Tuliteremsha pia kitabu cha Taurati ili baada ya kuondoka Musa pia, kiwe muongozo kwa Bani Israil wa kuufikia uongofu; na kwa kuisoma Taurati, waondokane na mghafala na kuyatambua majukumu na masuulia yao. Kwa watu wanaozitumia akili zao, Kitabu cha mbinguni ni wenzo wa ukumbusho na uongofu. Lakini Kitabu hicho hakiwafaidishi chochote watu wakaidi na wenye taasubi, wasiotumia akili zao. Kwa hakika wanaofaidika hasa na Kitabu cha mbinguni ni watu wanaofanya mambo yao kwa kutumia akili na mantiki na si kwa kufuata hawaa na matamanio ya nafsi zao. Ijapokuwa wanadamu wote wamepewa neema ya akili, lakini wengi wao wanatawaliwa na matashi na matamanio ya nafsi, badala ya kuongozwa na akili na hekima. Na kama inavyoeleza Qur’ani, mungu wa watu wengi ni hawaa na matamanio ya nafsi zao. Wanachofikiria watu kama hao ni kuweza kujistarehesha na kuzidi kujinufaisha kwa kila njia inayowezekana. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, sisi wanadamu wote, wakiwemo hata Mitume, tunahitajia uongofu wa Mwenyezi Mungu. Tab’an Mitume, wao hufikiwa na uongofu huo moja kwa moja kutoka kwa Allah, na sisi tuliosalia unatufikia kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia kwa Mitume. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, urithi ulioachwa na Mitume haukuwa ni mali, makasri wala mashamba; urithi muhimu zaidi ulioachwa na wajumbe hao wa Allah ni vitabu vya mbinguni kwa ajili ya uongofu wa watu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, mwanadamu anahitaji ukumbusho katika hali yoyote ile aliyo. Kwa sababu uongofu pia, kama hautaandamana na ukumbusho, baada ya muda husahaulika. Aya hizi zinatutaka tuelewe pia kuwa, akili humuelekeza mtu kwenye wahyi; na viwili hivyo kwa pamoja humfikisha mtu kwenye saada na ukamilifu wa kiutu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 55 ambayo inasema:
فَاصْبِرْ إِنَّ وَعْدَ اللَّهِ حَقٌّ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ بِالْعَشِيِّ وَالْإِبْكَارِ
Basi subiri. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Na omba maghufira kwa dhambi zako, na umtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi jioni na asubuhi.
Ijapokuwa inayemhutubu aya hii ni Bwana Mtume Muhammad SAW, lakini maamrisho yaliyomo ndani yake yanawahusu watu wote. Kuna nukta kadhaa ambazo zimeashiriwa katika aya hii: Ya kwanza ni kwamba, kwa kuwa imeshakuthibitikia wewe Mtume kuwa ahadi za Allah za kuwaongoza na kuwasaidia Mitume waliotangulia ni za kweli, basi na wewe pia kuwa na subira na vumilia katika njia ya kuwalingania watu uongofu na kuwaelekeza kwenye haki; na wala usidhoofishwe na kuvunjwa moyo na uafriti, inadi na ukaidi wa maadui. Kwa sababu siri kuu ya ushindi wako katika medani zote ni kuwa na subira na istikama ya kuvumilia shida na vizuizi unavyokabiliana navyo; na bila shaka kama utakuwa thabiti na mwenye subira ahadi ya Allah ya kukupa ushindi itathibiti tu. Hapana shaka, kuwa na imani kuhusu ukweli wa ahadi ya Allah humpa moyo mtu katika njia ya haki anayoifuata na anayoilingania na huweza kwa wepesi kuvumilia misukosuko inayomkabili. Nukta ya pili ni kuwa, kama hujatekeleza itakiwavyo jukumu lako katika njia hii, basi usafishe na uutakase moyo wako na kutu za madhambi kwa kumwomba maghufira Mola wako. Ni wazi kwamba Mitume wa Mwenyezi Mungu, wao ni waja maasumu na wala hawafanyi dhambi yoyote, kwa sababu kama wangekuwa wanamuasi Allah wangewezaje kuwakataza watu wasifanye maasi na madhambi na wawe tayari kuwatii wao kikamilifu! Kwa hiyo kuwa maasumu na kutofanya dhambi ni sharti la lazima la Utume. Na kama tunaona katika baadhi ya aya za Qur’ani limetumiwa neno dhambi kuhusu Bwana Mtume SAW au Mitume wengine, si kwa maana iliyo sawa na ya madhambi wanayofanya watu wengine. Ufanyaji dhambi wa watu ni wa kumuasi Mwenyezi Mungu, lakini kwa upande wa Mitume, ambao wana daraja za juu na upeo wa juu wa elimu ya kumjua Allah, haifai wao kughafilika na Mola wao hata lahadha ndogo au kuacha yale ambayo ni bora wao kuyafanya. Ukweli ni kwamba kufanya dhambi Mitume si kwa maana ya kumuasi Mwenyezi Mungu, bali ni kule kuhisi kwao kwamba hawajaweza kutekeleza wajibu wao kwa Allah SWT kwa namna inayomstahikia Yeye Mola Mwenye Enzi. Mfano wake, ni kama inavyokuwa kwa mtu anayemualika ugeni nyumbani kwake mtu mkubwa mwenye kuheshimika na akajaribu kumkirimu mgeni wake huyo ukomo wa uwezo wake, lakini baada ya ukarimu wote huo akamuomba radhi kwa mapungufu yaliyokuwepo. Sababu yake, ni kutokana na kuhisi kwamba, ijapokuwa amejitahidi kadiri ya uwezo wake, lakini ukarimu aliofanya haukukidhi hadhi na daraja ya mgeni wake huyo anayeheshimika. Na nukta ya mwisho iliyoashiriwa katika aya hii ni kwamba, tuimarishe imani zetu kwa kumdhukuru, kumhimidi na kumsabihi Allah SWT kila siku na tunapoanza kufanya kila jambo. Hapana shaka kuwa, kumhimidi na kumsabihi Mwenyezi Mungu, kumtakasa na kila kasoro na nuksani na kumshukuru Muumba huyo aliyetukuka na asiye na mwenza huijenga roho na moyo wa mtu na kumfanya apambike kwa sifa tukufu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kama tunaziamni kweli ahadi za Mwenyezi Mungu, basi tuwe imara na thabiti katika kutekeleza majukumu ya kidini; na wala tabu na matatizo yanayotukabili katika njia hiyo yasituzuie kufikia lengo letu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, watu wote, wakiwemo Mitume wana wajibu wa kuomba maghufira, kwa sababu taksiri na makosa wanayofanya watu wa kawaida au mpaka maalumu wa uwezo na suhula walizonazo Mitume havitoi kwa fursa kwao ya kutekeleza wajibu na majukumu yao kwa Allah kama inavyopasa na inavyomstahikia Yeye Mola. Aidha aya hii inatuelimisha kwamba, kumdhukuru na kumsabihi Mwenyezi Mungu inapasa kufanyike kila siku na kwa kudumu asubuhi na jioni ili kuweza kumuinua mtu daraja yake na kuimarisha misingi ya imani yake. Na pia aya hii inatutaka tuelewe kuwa, kuhimidi na kusabihi inapasa yote mawili yafuatane pamoja ili tumshukuru Allah kwa neema zake na pia tumtakase na ufanyaji dhulma au uonevu wa aina yoyote ile kwa waja wake.
Tunaihitimisha darsa yetu hii kwa aya ya 56 ambayo inasema:
إِنَّ الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِ اللَّهِ بِغَيْرِ سُلْطَانٍ أَتَاهُمْ ۙ إِن فِي صُدُورِهِمْ إِلَّا كِبْرٌ مَّا هُم بِبَالِغِيهِ ۚ فَاسْتَعِذْ بِاللَّهِ ۖ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ
Hakika hao wanao bishana katika Ishara za Mwenyezi Mungu bila ya dalili yoyote iliyowafikia, hawana vifuani mwao ila kutaka ukubwa tu, na wala huo hawaufikii. Basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.
Aya hii inaashiria chimbuko la kuikana na kuipiga vita dini kwa kueleza kwamba, watu wanaokadhibisha na kuzipinga aya za Qur’ani na miujiza ya Mitume bila hoja wala burhani na kuanzisha mijadala na mabishano yasiyo na mantiki ili kuwazuia watu wengine wasiifuate dini, huwa wanachochewa na kiburi na ghururi waliyonayo ndani ya nafsi zao. Wao hujikweza na kuwadunisha waumini. Kwa hiyo sio wao wenyewe tu wasio tayari kuuamini wito wa Mitume lakini wanatumia mijadala na mabishano marefu ili kuwazuia watu wengine pia wasiifuate njia ya haki; na kwa dhana yao, kufanya hivyo kutawazuia Mitume wasipate hadhi katika jamii na kuwanyang'anya wao nafasi na hadhi yao ya juu waliyonayo. Lakini Mwenyezi Mungu ameahidi kuwa, ataviondoa vizuizi hivyo vinavyowekwa na watu hao na hatoruhusu wapinzani wa haki wafikie malengo yao maovu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, ukafiri na ukanushaji unaofanywa na watu wengi chimbuko lake ni kujikweza na kutakabari mbele ya haki, na si kwamba hawabainikiwi na ukweli wa maneno ya Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, mtu anayetakabari anatafuta ukubwa na mamlaka ya kuitawala jamii, lakini hawezi kufikia lengo lake hilo; na hata kama ataonekana kidhahiri kuwa amelifikia, hufedheheka na kudunika na mwisho wake hukataliwa na jamii. Vilevile aya hii inatutaka tujikinge na kuomba hifadhi kwa Allah katika kila hali, hususan tunapoandamwa na kila aina ya njama na hila za maadui wa dini. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 867 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atunusuru na shari za maadui zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../