May 27, 2023 03:41 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 927 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 46 ya al Ah'qaaf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 29 ya sura hiyo ambayo inasema:

وَإِذْ صَرَفْنَا إِلَيْكَ نَفَرًا مِّنَ الْجِنِّ يَسْتَمِعُونَ الْقُرْآنَ فَلَمَّا حَضَرُوهُ قَالُوا أَنصِتُوا ۖ فَلَمَّا قُضِيَ وَلَّوْا إِلَىٰ قَوْمِهِم مُّنذِرِينَ

Na tulipokuletea kundi la majini kusikiliza Qur'ani. Basi walipo ihudhuria walisema: Nyamazeni! Na ilipo kwisha somwa, walirudi kwa kaumu yao kwenda kuwaonya.

Katika darsa zilizopita tulisoma aya zilizowahutubu washirikina wa Makka, ambao kwa sababu ya ukaidi na utoaji visingizio tu hawakuwa tayari kusilimu na kuiamini haki. Aya tuliyosoma inaendeleza maudhui hiyo kwa kusema: japokuwa nyinyi hamjaikubali na kuiamini haki, lakini kundi moja la majini, na ambao nyinyi wenyewe mnaamini kuwa wapo na hata mnawaitakidi kwamba wana taathira katika maisha yenu, wakati walipozisikia aya za Qur'ani walimwamini Mtume na hata wakawalingania na kuwafikishia wenzao pia wito wa Uislamu. Kuwepo viumbe waitwao majini ni moja ya maudhui zilizobainishwa kwa uwazi kabisa ndani ya Qur'ani tukufu. Sura moja ya kitabu hicho cha mbinguni inaitwa Suratul-Jin, ambayo ndani yake imeelezwa kwamba, wao majini wanamwamini Mungu pekee wa haki, Qur'ani na kufufuliwa viumbe; na kwamba katika viumbe hao, wako walio waumini na wako makafiri pia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, majini ni viumbe pia kama walivyo wanadamu; wana akili, hisia na wajibu wa kutekeleza maamrisho ya Allah na kujiepusha na makatazo yake; na wamepewa pia irada na uwezo wa kuchagua njia ya kufuata. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kuamini tu peke yake hakutoshi; bali inalazimu mtu awalinganie na kuwaongoza wenzake pia katika njia ya haki.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 30 hadi 32 ambazo zinasema:

قَالُوا يَا قَوْمَنَا إِنَّا سَمِعْنَا كِتَابًا أُنزِلَ مِن بَعْدِ مُوسَىٰ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ وَإِلَىٰ طَرِيقٍ مُّسْتَقِيمٍ

Wakasema: Enyi kaumu yetu! Sisi tumesikia Kitabu kilicho teremshwa baada ya Musa, kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake, na kinacho ongoza kwenye Haki na kwenye Njia Iliyo Nyooka.

يَا قَوْمَنَا أَجِيبُوا دَاعِيَ اللَّهِ وَآمِنُوا بِهِ يَغْفِرْ لَكُم مِّن ذُنُوبِكُمْ وَيُجِرْكُم مِّنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ

Enyi kaumu yetu! Muitikieni Mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu, na muaminini, Mwenyezi Mungu atakughufirieni madhambi yenu, na atakukingeni na adhabu iumizayo. 

وَمَن لَّا يُجِبْ دَاعِيَ اللَّهِ فَلَيْسَ بِمُعْجِزٍ فِي الْأَرْضِ وَلَيْسَ لَهُ مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءُ ۚ أُولَٰئِكَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ

Na asiyemwitikia Mwitaji wa Mwenyezi Mungu basi hatashinda katika ardhi, wala hatakuwa na walinzi mbele yake. Hao wamo katika upotovu ulio dhaahiri. 

Kwa mujibu wa aya hizi, wakati majini waumini waliporejea kwa kaumu yao, waliwalingania kwa kuwaambia: Mungu yuleyule aliyemtuma Musa na Kitabu, sasa amemtuma Mtume mwengine na kitabu chengine kiitwacho Qur'ani. Leo sisi tumesikia aya za kitabu hicho na tumebaini kuwa, kama kilivyokuwa Kitabu cha Musa kinawalingania watu kufuata njia ya haki. Kila mwenye kumwamini Mtume huyo, ambaye anawalingania watu dini ya Mwenyezi Mungu, ataepukana na madhambi na maovu na kuokoka na adhabu ya Mola. Lakini asiyeamini na akaikadhibisha haki ajue kwamba hataweza kukabiliana na irada ya Mwenyezi Mungu na kusalimika na adhabu yake, kwa sababu hakuna awezaye kumnusuru mtu na adhabu ghairi ya Yeye Mola. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, majini, nao pia wanazo habari kuhusu historia za Mitume waliopita na yaliyomo kwenye vitabu vya mbinguni. Kundi moja katika wao ni waumini; na kundi jengine ni makafiri. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, njia ya haki ndio njia iliyonyooka. Ni njia inayomuepusha mtu na kila aina ya upotofu na kufurutu mpaka na inaongoza kwa uadilifu, kadiri na wastani. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Mitume wanawalingania watu njia ya Mwenyezi Mungu, si kuwafuata wao. Wanawabainishia watu hukumu na sharia tukufu za Mwenyezi Mungu; na si chochote kile kinachotokana na wao. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa, kukufuru na kumkanusha Mwenyezi Mungu, mwishowe humfikisha mtu kwenye mkwamo; mkwamo ambao si yeye mtu mwenyewe anaweza kujikwamua; wala si watu wengine wanao uwezo wa kumtoa.

Ifuatayo sasa ni aya ya 33 na 34 ambazo zinasema:

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّهَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَلَمْ يَعْيَ بِخَلْقِهِنَّ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَن يُحْيِيَ الْمَوْتَىٰ ۚ بَلَىٰ إِنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

Je! Hawaoni ya kwamba Mwenyezi Mungu, aliye ziumba mbingu na ardhi, na hakuchoka kwa kuziumba, kuwa ni Muweza wa kuwafufua wafu? Naam! Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.

وَيَوْمَ يُعْرَضُ الَّذِينَ كَفَرُوا عَلَى النَّارِ أَلَيْسَ هَٰذَا بِالْحَقِّ ۖ قَالُوا بَلَىٰ وَرَبِّنَا ۚ قَالَ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ

Na siku watakapo letwa makafiri Motoni wakaambiwa: Je! Haya si kweli? Watasema: Naam! Tunaapa kwa Mola wetu Mlezi, (ni kweli)! Atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu ya kule kukufuru kwenu.

Aya hizi ambazo ni miongoni mwa aya za mwisho za Suratul-Ah'qaaf, kwa mara nyingine tena zinagusia maudhui ya maadi, yaani kufufuliwa viumbe na kuwahutubu washirikina ya kwamba: Mwenyezi Mungu ambaye ameumba mbingu na ardhi na hajachoka wala kushindwa kuviumba viwili hivyo, ni mweza wa kuwafufua waliokufa. Bila shaka uumbaji wa ulimwengu huu mkubwa na mpana, wenye anuai za viumbe wa kila sura, maumbo na rangi ni ishara ya uwezo usio na ukomo alionao Muumba wa kufanya kitu chochote kile. Na kama ni hivyo itawezekanaje Mola kama huyo ashindwe kuwafufua na kuwaumba tena wanadamu? Hii yenyewe ni hoja na ishara ya wazi kabisa kuhusu uwezekano wa kutokea maadi. Kwa hiyo tatizo si uwezo wa Mwenyezi Mungu unaokufanyeni msiamini kufufuliwa; tatizo ni nyinyi wenyewe; na chanzo chake ni kutaka mfanye kila mtakacho kulingana na matamanio na matashi ya nafsi zenu, kisha msalimike na wala msifikwe na hatima inayoendana na mliyoyafanya. Ukweli ni kwamba, mtakapoyaona wenyewe macheche ya kutisha ya moto Siku ya Kiyama, hamtakuwa na la kufanya isipokuwa kuungama na kukiri ukweli wa mliyoelezwa na mliyoahidiwa, lakini kukiri huko kutakuwa na faida gani, ikiwa wakati huo hakutakuwa na njia ya kukuwezesheni kurudi tena duniani kufidia mliyoyaacha! Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, uwezo wa Mwenyezi Mungu hauna mwisho, ukomo wala mpaka. Uwezo wa Allah SWT katika uumbaji wa ulimwengu huu wenye adhama ni hoja ya wazi zaidi ya kuthibitisha uwezekano wa kuumbwa tena mwanadamu Siku ya Kiyama. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ndimi za makafiri zitafunguka kuiungama haki Siku ya Kiyama. Watamkiri Allah kuwa ni Mola na Mlezi wao, kwamba Kiyama ni kweli na malipo ya thawabu na ikabu yapo kama yalivyoahidiwa, lakini kukiri na kuungama huko hakutawafalia kitu wala kuwa na faida yoyote kwao wakati huo.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 35 ambayo inasema:

فَاصْبِرْ كَمَا صَبَرَ أُولُو الْعَزْمِ مِنَ الرُّسُلِ وَلَا تَسْتَعْجِل لَّهُمْ ۚ كَأَنَّهُمْ يَوْمَ يَرَوْنَ مَا يُوعَدُونَ لَمْ يَلْبَثُوا إِلَّا سَاعَةً مِّن نَّهَارٍ ۚ بَلَاغٌ ۚ فَهَلْ يُهْلَكُ إِلَّا الْقَوْمُ الْفَاسِقُونَ

Basi subiri, kama walivyo subiri Mitume wenye ustahmilivu mkubwa, wala usiwahimizie (adhabu). Siku watakapo yaona waliyo ahidiwa itakuwa kama kwamba hawakukaa (ulimwenguni) ila saa moja ya mchana. Huu ndio ufikisho! Kwani huangamizwa isipo kuwa walio watu mafasiki? 

Aya hii, ambayo ndiyo aya ya mwisho ya Suratul-Ah'qaaf inamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW ya kwamba, kuwa na subira na vumilia idhilali na maudhi ya washirikina pamoja na inadi na ukaidi wao; wala usiwe na haraka ya kuona adhabu itakayowafika. Sababu ni kwamba, Allah SWT atawapa malipo ya adhabu Siku ya Kiyama kwa amali na matendo yao maovu na machafu waliyofanya. Jukumu na wajibu wako wewe ni kufikisha wito wa Mola wako, huwajibiki kwa matokeo ya kazi yako. Ikiwa watu wataamini au watakufuru, jaza na malipo ya kuamini au kukufuru kwao watayakuta kwake Yeye Allah SWT. Aya hii inaashiria pia jinsi umri na uhai ulivyo mfupi. Namna uhai wa duniani ulivyo mfupi kulinganisha na maisha ya milele ya akhera, watu siku hiyo watahisi kama kwamba hawakukaa hapa duniani zaidi ya saa moja tu ya siku nzima. Hapo ndipo watakapopatwa na majuto na huzuni kubwa, kwa nini hawakuchagua kufuata njia ya haki; lakini majuto yao hayatawafalia kitu, kwa sababu hakutakuwa na njia yoyote ya kufidia makosa waliyoyatanguliza. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, jukumu la Mitume ni kufikisha wito wa Mwenyezi Mungu; haiwajuzii kuwalazimisha watu waamini au kutoa adhabu kwa makafiri. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kwamba, kuwa na kifua kipana na kuwastahamilia wapinzani, ni sifa mojawapo ya Mitume wa Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo wafuasi wao, inapasa wawe namna hivyo pia. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa, moja ya taratibu alizoweka Allah ni kutoa muhula na fursa kwa makafiri na wafanya madhambi hapa duniani. Vilevile aya hii inatutaka tuelewe kwamba uhai wa duniani ni mfupi sana kulinganisha na wa akhera; kwa sababu ni mithili ya saa moja tu ya siku nzima. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 927 ya Qur'ani imefikia tamati. Na ndiyo inayotuhitimishia pia tarjumi na maelezo ya sura hii ya 46 ya Al Ahq’aaf. In shaa Allah tuwe tumeaidhika, kuelimika na kufaidika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka na atujaalie kuwa miongoni mwa atakaowarehemu kwa kuwaingiza katika Pepo yake ya milele huko akhera, amin. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/