May 27, 2023 04:58 UTC
  • Sura ya Muhammad, aya ya 36-38 (Darsa ya 936)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 936 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 47 ya Muhammad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 36 na 37 za sura hiyo ambazo zinasema:

إِنَّمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا لَعِبٌ وَلَهْوٌ ۚ وَإِن تُؤْمِنُوا وَتَتَّقُوا يُؤْتِكُمْ أُجُورَكُمْ وَلَا يَسْأَلْكُمْ أَمْوَالَكُمْ

Hakika maisha ya dunia ni mchezo na pumbao. Na kama mkiamini na mkawa na takua, Mwenyezi Mungu atakupeni ujira wenu, wala hakutakeni mali zenu.

إِن يَسْأَلْكُمُوهَا فَيُحْفِكُمْ تَبْخَلُوا وَيُخْرِجْ أَضْغَانَكُمْ

Na akikutakeni hayo na kukushikilieni mtafanya ubakhili, na atatoa undani wa chuki zenu.

Mojawapo ya mambo yanayomfanya mtu awe na mapenzi ya dunia, ni kuwa na mtazamo potofu juu ya maisha haya ya ulimwenguni. Mtu anayedhani kwamba mali na utajiri wake na nguvu za madaraka na mamlaka alizonazo vitadumu na kubaki naye milele, huvikumbatia hivyo na huwa na mapenzi navyo laisal kiasi. Mtu kama huyo, huwa hawi tayari kutoa mali na alivyonavyo katika njia ya Mwenyezi Mungu au kuyatumia madaraka na mamlaka yake katika njia ya kuitia nguvu dini ya Allah. Lakini kwa mtu anayemwamini Mwenyezi Mungu, yeye huichukulia dunia kuwa ni sawa na njia ya mapito, ambayo kandokando yake kuna misitu ya kupendeza na uwanda wa kuvutia. Waliowengi, miongoni mwa wanaoipita njia hiyo, hughafilika na kule wanakoelekea, wakasimama kando yake kwenye vivuli vya miti na pembeni ya mito ili kujiburudisha na kujistarehesha tu. Lakini kwa wale wanaomwamini Allah SWT, hawaghafiliki na wanakoelekea katika uliko mwisho wa safari yao. Kama walivyo watu wengine, wao pia husimama kando ya njia hiyo, kadiri inavyolazimu ili kubeba wanayohitajia. Lakini pamoja na hayo, kisimamo hicho hakiwachukulii muda wao mrefu, bali huendelea, tena kwa mwendo wa kasi, na safari yao ya kule wanakoelekea. Mbali na hayo, waliomwamini Allah, wanaipita njia ya maisha kwa kumcha Mola wao na kuichunga taqwa, ili wasije wakakhalifu sharia za Mwenyezi Mungu wakati wakiwa njiani, na hivyo kuweza kufika wanakoelekea salama usalimini. Ni wazi kwamba awezaye kuyakata masafa kwa kasi katika njia ya maisha ya dunia na kufika haraka anakoelekea, ni yule asiyejibebesha mizigo na masurufu mengi yatakayomtia wasiwasi na wahaka muda wote kufikiria namna ya kuyahifadhi na kuyalinda. Ni yule ambaye afikapo kwenye kila kituo, huchukua kile anachohitaji tu hadi atakapofika kituo kingine, na kuwaachia wenzake wanaohitajia, vingine vilivyosalia. Na naam! kinachozuia mwendo, harakati na hatua za mwanadamu katika njia ya maisha ni uchu na ubakhili, ambavyo humfanya asiwe na mzigo mwepesi wa kumfikisha haraka anakoelekea. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kushughulishwa na anasa za dunia, kuikumbatia na kuwa na mapenzi nayo kupindukia mpaka ikatusahaulisha akhera, haviendani na kumwamini na kumcha Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, dunia ya watu wasiomwamini Mwenyezi Mungu ni mithili ya dunia ya watoto, ambao mapenzi yao yote wameyaelekeza kwenye vitu vyao vya kuchezea na hivyo hupitisha siku na maisha yao kwa kujipumbaza na kujifurahisha na vitu hivyo. Wa aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba, kuwa na fedha na mali ni jambo la lazima kwa ajili ya kujikimu katika maisha ya hapa duniani, lakini iwe ni kwa kiwango cha kumtoshelezea mtu mahitaji yake ili asiwe mhitaji kwa wengine; na si kwamba lengo pekee la maisha kwake yeye, likawa ni kukusanya na kujilimbikizia mali na utajiri. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kuwa, uchu na ubakhili humzuia mtu kutekeleza majukumu yake ya kidini yanayohusiana na utoaji na kuwafanyia watu wema na ihsani.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 38 ambayo inasema:

هَا أَنتُمْ هَٰؤُلَاءِ تُدْعَوْنَ لِتُنفِقُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَمِنكُم مَّن يَبْخَلُ ۖ وَمَن يَبْخَلْ فَإِنَّمَا يَبْخَلُ عَن نَّفْسِهِ ۚ وَاللَّهُ الْغَنِيُّ وَأَنتُمُ الْفُقَرَاءُ ۚ وَإِن تَتَوَلَّوْا يَسْتَبْدِلْ قَوْمًا غَيْرَكُمْ ثُمَّ لَا يَكُونُوا أَمْثَالَكُم

Angalieni! Nyinyi ndio mnaitwa ili mtoe (mali) katika njia ya Mwenyezi Mungu, lakini wapo katika nyinyi wanao fanya ubakhili. Na afanyaye ubakhili, basi anajifanyia ubakhili mwenyewe. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, na nyinyi ndio wahitaji. Na mkigeuka atawaleta watu wengine badala yenu, nao hawatakuwa kama nyinyi. 

Aya hii, ambayo ndiyo aya ya mwisho ya Suratu-Muhammad inaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kwa kuashiria baadhi ya Waislamu wenye mapenzi ya mali na utajiri wa kidunia na kuacha kutoa mali na utajiri wao huo katika njia ya Mwenyezi Mungu; na kuwaambia: kama nyinyi mnamwamini kweli Mwenyezi Mungu, imani yenu haihusiani na kusali na kufunga tu, ibada ambazo hazishurutishi kutumia mtu mali yake; lakini sharti jengine la imani ya kweli juu ya Allah, ni kutoa sehemu ya mali kwa njia ya Zaka au kwa ajili ya Jihadi katika njia ya kuipa nguvu dini yake. Bila shaka watu wanaofanya ubakhili katika mambo hayo, wasidhani kwamba Allah SWT ni mhitaji kwao, ndio maana anawaamuru kufanya hivyo, bali wao ndio wanaomhitaji Yeye Mola; na kadiri wanavyofanya ubakhili, kwa hakika wanajikosesha malipo ya thawabu na rehma za Allah za hapa duniani na akhera. Sehemu ya mwisho ya aya inatumia lugha kali na ya kutishia kwa kusema: msidhani kwamba, kwa kuwa ni waumini, mtapata rehma na uraufu wa Mola kila mara hapa duniani. Kama nyinyi mtazembea katika kutekeleza wajibu wenu wa kuilinda dini ya Mwenyezi Mungu na kupambana na maadui wa dini, nguvu na nafasi yenu itadhofu na kupungua hatua kwa hatua, na mwishowe mtatoweka. Na katika hali kama hiyo, Allah SWT atawaleta badala yenu watu wengine, ambao wana juhudi na bidii katika kuilinda dini yake, na ambao hawatokuwa na ubakhili wa kutoa sehemu ya mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, ubakhili katika kutoa, hauendani na kumwamini Mwenyezi Mungu; na mtu muumini wa kweli hawezi kuwa bakhili. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, jambo lisilo na shaka ni kwamba, Muislamu inampasa atoe katika njia ya Mwenyezi Mungu kulingana na uwezo wa mali na fedha alionao; na atambue pia kuwa Allah SWT ni mkwasi mutlaki asiye na uhitaji wa chochote, lakini yeye mja, hata akijikusanyia na kujilimbikizia mali kwa kiwango chochote kile, atabaki kuwa mhitaji kwake Yeye Mola. Vilevile aya hii inatutaka tuelewe kwamba, waumini wanapata nusra na msaada wa Mwenyezi Mungu pale wanapotekeleza sawasawa na kwa usahihi majukumu yao; na Yeye Mola hajatoa dhamana ya kumpa mtu nusra na msaada wake vyovyote vile iwavyo. Wa aidha aya inatutaka tutambue kuwa, kujitolea roho na mali katika njia ya Allah ndiko kunakodhamini kuendelea kubaki na kuwepo kwa jamii; na kuacha kufanya hivyo kwa sababu ya kuikumbatia dunia hupelekea kuporomoka jamii na kuletwa mahala pake jamii na kaumu nyengine. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 936 ya Qur'ani imefikia tamati na ndiyo inayotuhitimishia tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 47 ya Muhammad. Inshallah tuwe tumenufaika na kuaidhika na yote tuliyojifunza kutokana na sura hii. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waumini wa kweli, tunaoyashika yote aliyotuamrisha na kuyaepuka yote aliyotukataza; na si kufanya yaliyo mepesi tu kwetu na kuyaacha yasiyopendeza nafsi zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/