May 27, 2023 05:34 UTC
  • Sura ya al-Fat-h Aya ya 14-16 (Darsa ya 940)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahi Rahmani Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 940 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 48 ya al-Fat-h. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 14 ya sura hiyo ambayo inasema:

وَلِلَّهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ يَغْفِرُ لِمَن يَشَاءُ وَيُعَذِّبُ مَن يَشَاءُ ۚ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا

Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi. Humsamehe amtakaye, na humuadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghufira, Mwenye kurehemu. 

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizowazungumzia wanafiki, ambao katika batini na ndani ya nafsi zao ni makafiri, lakini nje na katika dhahiri yao wanajionyesha kuwa ni Waislamu. Katika mwendelezo wa maudhui hiyo, aya tuliyosoma inasema: hapana shaka Mwenyezi Mungu ni msamehevu na mrehemevu; na yeyote anayetubia na akajutia matendo maovu aliyoyafanya huko nyuma, atapata maghufira na msamaha wake. Lakini kwa wale wanaoshupalia na kushikilia kufuata njia ya upotofu na wakaamua kuendeleza inadi na ukaidi dhidi ya haki, hao kwa hakika wameamua kujikosesha rehma za Allah SWT na hapana shaka watalipwa malipo ya adhabu kwa matendo yao maovu waliyofanya. Aya hii inatilia mkazo pia mamlaka mutlaki ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ulimwengu wote ili asije mtu yeyote yule akapitikiwa na dhana kwamba anaweza kutoka nje ya utawala na mamlaka yake Mola Muumba au kuishinda irada yake na alitakalo Yeye Mola. Baadhi ya tunayojifunza kutokana na aya hii ni kwamba, rehma, upole na uraufu wa Mwenyezi Mungu umeizidi ghadhabu yake. Ikiwa mwanadamu hatojifungia mwenyewe mlango wa rehma za Mwenyezi Mungu kutokana na matendo yake, awe na hakika kwamba endapo atatubia kwa mabaya aliyofanya atarehemewa na Yeye Mola aliye mwingi wa rehma na huruma. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, ili mtu aweze kupata uokovu Siku ya Kiyama inalazimu aambatanishe pamoja hofu na matumaini kwa Allah. Na ndio maana tunaona katika mfumo wa malezi ya kidini, watu wanatakiwa wawe kwenye hali ya hofu na matarajio ili wasifikie hatua ya kukata tamaa moja kwa moja ya kupata msamaha wa Mola, wala kuingiwa na ghururi ya kujihisi wameshafuzu kikamilifu, bali wawe na matumaini na matarajio ya kupata za Mwenyezi Mungu na wakati huohuo wawe na woga na hofu ya kufikwa na ghadhabu na adhabu yake Mola.

Ifuatayo sasa ni aya ya 15 ya sura yetu ya al-Fat-h ambayo inasema:

سَيَقُولُ الْمُخَلَّفُونَ إِذَا انطَلَقْتُمْ إِلَىٰ مَغَانِمَ لِتَأْخُذُوهَا ذَرُونَا نَتَّبِعْكُمْ ۖ يُرِيدُونَ أَن يُبَدِّلُوا كَلَامَ اللَّهِ ۚ قُل لَّن تَتَّبِعُونَا كَذَٰلِكُمْ قَالَ اللَّهُ مِن قَبْلُ ۖ فَسَيَقُولُونَ بَلْ تَحْسُدُونَنَا ۚ بَلْ كَانُوا لَا يَفْقَهُونَ إِلَّا قَلِيلًا

Walio baki nyuma watasema: Mtapo kwenda kuchukua ngawira, tuacheni tufuatane nanyi! Wanataka kuyabadili maneno ya Mwenyezi Mungu. Sema: Hamtatufuata kabisa. Mwenyezi Mungu alikwisha sema kama hivi zamani. Hapo watasema: Bali nyinyi mnatuhusudu. Siyo, bali walikuwa hawafahamu ila kidogo.

Moja ya sifa walizonazo wanafiki, ni kuwa kwao watu wasioacha kujinufaisha kwa fursa yoyote itokeayo. Wakati itokeapo hatari hujiweka mbali kwa visingizio hivi na vile na kukwepa kutekeleza majukumu na wajibu walionao, lakini popote pale na wakati wowote ule wanapohisi kuwepo kwao kwenye jambo kuna manufaa na wao, hawachelewi kujitokeza mbele. Wakati Waislamu walipokuwa njiani wanarudi Madina wakitoka Hudaibiyah, Mwenyezi Mungu Mtukufu alimpa Bwana Mtume Muhammad SAW bishara ya ushindi wa Khaybar na akawazuilia kushiriki vita vya Khaybar wale waliokataa kwenda Hudaibiyah. Lakini wakati Waislamu walipokuwa wanaelekea Khaybar, kundi la watu hao lilimtaka Bwana Mtume awaruhusu waungane na msafara wa Waislamu kuelekea huko kwa kisingizio cha kufidia uzembeaji wa kubaki kwao nyuma na kusalia Madina katika kadhia ya Hudaibiyah, lengo likiwa ni kutaka na wao pia wakanufaike na ngawira zitakazopatikana huko. Lakini Bwana Mtume SAW aliwasomea amri iliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu na kuwazuia wasishiriki katika vita vya Khaybar. Ajabu ni kwamba, badala ya kundi la watu hao wajalimaslahi kukiri kwamba wao wenyewe ndio wa kulaumiwa kwa hilo, waliwabebesha dhima ya lawama watu wengine na kusema: wao hawataki sisi tushiriki katika Jihadi hii kwa sababu ya husuda waliyonayo juu yetu, na wanataka ngawira zote za huko wapate wao! Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, wale ambao wakati wa dhiki na hatari wanakwepa kutekeleza wajibu na majukumu yao ya kijamii, inapasa wanyimwe baadhi ya suhula na huduma za ustawi wa jamii ili usipatikane mwanya wa kujitokeza na kuenea watu wajalimaslahi tu ndani ya jamii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kila Muislamu hudai kwamba ameamini na anafuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu SWT. Lakini waumini wa kweli na wanafiki hupambanuka pale matukio ya shida, dhiki na misukosuko inapowafika Waislamu. Halikadhalika tunajifunza kutokana na aya hii kwamba, waumini wasishtushwe wala kuingiwa na hofu kutokana na tuhuma na uzushi wa wanafiki, ambao huwavurumizia tuhuma ili wao waweze kujivua na dhima ya makosa waliyofanya.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 16 ambayo inasema:

قُل لِّلْمُخَلَّفِينَ مِنَ الْأَعْرَابِ سَتُدْعَوْنَ إِلَىٰ قَوْمٍ أُولِي بَأْسٍ شَدِيدٍ تُقَاتِلُونَهُمْ أَوْ يُسْلِمُونَ ۖ فَإِن تُطِيعُوا يُؤْتِكُمُ اللَّهُ أَجْرًا حَسَنًا ۖ وَإِن تَتَوَلَّوْا كَمَا تَوَلَّيْتُم مِّن قَبْلُ يُعَذِّبْكُمْ عَذَابًا أَلِيمًا

Waambie walio achwa nyuma katika watu wa majangwani: Karibuni hivi mtaitwa kwenda kupigana na watu wakali kwa vita, mpigane nao au wasalimu amri. Basi mkit'ii, Mwenyezi Mungu atakupeni ujira mzuri. Na mkigeuka kama mlivyo geuka kwanza, atakuadhibuni kwa adhabu iumizayo.

Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia ya kukataliwa ombi la wanafiki la kutaka waruhusiwe kushiriki katika vita vya Khaybar na kueleza kwamba, kama nyinyi kweli mnajuta kwa kosa mlilofanya huko nyuma, basi thibitisheni ukweli wa maneno yenu katika medani ya Jihadi ngumu iliyoko mbele yenu; na hii ni njia ambayo Mwenyezi Mungu amekufungulieni ili akusameheni kwa mliyofanya huko nyuma. Hata hivyo msitarajie kupata ngawira za vitu katika vita hivyo, wala msijitose kwenye medani ya mapigano kwa tamaa ya kupata ngawira. Pamoja na hayo mtapata malipo ya thawabu kwa Mwenyezi Mungu wanayopata wanaopigana katika njia ya haki. Lakini kama mtakaidi kwenda kwenye medani ya vita hivyo pia na mkahalifu amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, jueni kwamba adhabu kali ya Moto inakusubirini. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, katika mfumo wa kijamii tuwafungulie njia ya kutubia makosa yao wale waliokosea, ambako wako tayari kujirekebisha; na si kuwasusia moja kwa moja. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, tusimdharau na kumdogesha adui kwa namna yoyote ile, wala ushindi tuliopata huko nyuma tusiuchukulie kuwa hoja ya kupata ushindi tena katika vita vijavyo, kwa sababu inawezekana naye pia akajizatiti na kujiimarisha na kuingia kwenye medani ya mapambano akiwa na nguvu zaidi ya alivyokuwa hapo kabla. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, nguvu na uwezo wa kujilinda na kujihami Waislamu inapasa ufikie kiwango cha kumfanya adui alazimike kusalimu amri na kukubali kushindwa. Vilevile aya hii inatutaka tuelewe kuwa, lengo la kupigana Jihadi ni kutii amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, si kutwaa na kujiongezea maeneo ya ardhi wala kuwahodhi na kuwatawala watu wengine. Kwa hivyo wanaochopigania wanajihadi wa kweli huwa ni kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kuepukana na ghadhabu zake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 940 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/