Sura ya H'ujuraat, aya ya 10-12 (Darsa ya 946)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 946 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 49 ya H'ujuraat. Tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya yake ya 10 ambayo inasema:
إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ
Kwa hakika Waislamu wote ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe.
Katika ubora ulionao Uislamu ni kuweka msingi wa kuwepo uhusiano wa kiudugu baina ya waumini wote. Kwa kawaida, ndugu wawili katika familia moja huwa wanajichukulia kuwa na hadhi na nafasi sawa katika familia yao pasi na mmoja kujihisi au kujifanya bora kuliko mwenzake na kujipa cheo na nafasi ya juu zaidi. Na namna hivyo pia Uislamu unawausia waumini kwamba, pamoja na kutafautiana kwao kwa makabila, asili na lugha wajione wote wako sawa; wala asitokee yeyote kati yao akajiona mbora kuliko wenzake. Bwana Mtume Muhammad SAW aliwafungisha masahaba zake mkataba wa udugu, ili mfungamano huo wa kidini uendelee kuwepo daima kati ya Waislamu katika zama zote za historia. Katika hotuba alizotoa katika nyakati, mwahala na mazingira tofauti, Nabii huyo wa rehma alikuwa akisisitiza kwa kusema: "mwarabu hana ubora kwa asiye mwarabu, wala mweupe hana ubora kwa mweusi, bali wote ni ndugu na waja wa Mwenyezi Mungu". Kwa hivyo kila zinapotokea tofauti na mizozo baina ya Waislamu wawili au makundi mawili ya Waislamu, jukumu wanalokuwa nalo Waislamu wengine ni kuwasuluhisha na kuwapatanisha wenzao kwa msingi wa udugu na kutekeleza haki na uadilifu baina ya Waislamu hao waliogombana. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, haijuzu kwa mtu yeyote kujikweza na kujiona bora kuliko wengine, kwa sababu waumini wote wanalingana na wana hali na hadhi sawa. Kinyume na uhusiano wa wazazi kwa watoto wao, ambao unaanzia juu kushuka chini, uhusiano baina ya ndugu huwa na mlingano wa usawa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kama ambavyo familia huchukua hatua kutatua tofauti zitokeazo kati ya ndugu wawili, jamii ya Kiislamu pia inapaswa kufanya juhudi za kuondoa tofauti zinazozuka baina ya waumini na kuleta suluhu na mapatano kati yao. Wa aidha aya hii inatutaka tujue kwamba amani, upendo na masikilizano yanayokuwepo baina ya waumini, huwa sababu ya wao kuteremkiwa na rehma za Mwenyezi Mungu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 11 ya sura yetu ya H'ujuraat ambayo inasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَسْخَرْ قَوْمٌ مِّن قَوْمٍ عَسَىٰ أَن يَكُونُوا خَيْرًا مِّنْهُمْ وَلَا نِسَاءٌ مِّن نِّسَاءٍ عَسَىٰ أَن يَكُنَّ خَيْرًا مِّنْهُنَّ ۖ وَلَا تَلْمِزُوا أَنفُسَكُمْ وَلَا تَنَابَزُوا بِالْأَلْقَابِ ۖ بِئْسَ الِاسْمُ الْفُسُوقُ بَعْدَ الْإِيمَانِ ۚ وَمَن لَّمْ يَتُبْ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ
Enyi mlio amini! Wanaume wasiwadharau wanaume wengine, huenda wakawa bora kuliko wao; wala wanawake (wasiwadharau) wanawake wengine, huenda hao wakawa bora kuliko wao. Wala msitiane kasoro, wala msiitane kwa majina (mabaya) ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwisha amini. Na wasio tubu, hao ndio madhalimu.
Baada ya aya iliyotangulia kutilia mkazo uhusiano wa kiudugu kati ya waumini, aya hii inagusia mifano mitatu ya madhambi ya ulimi yanayoudhuru na kuutia doa uhusiano huo wa kiudugu kwa kueleza kwamba: si mwanamme wala mwanamke yeyote au watu wa kabila na rangi yoyote ile wenye haki ya kumdharau na kumkejeli mtu au watu wa kabila, mbari na rangi nyingine. Kwa sababu hakuna mtu au kaumu yoyote iliyo bora na iliyo juu kuliko nyingine, hata ijipe haki ya kuwadharau na kuwadunisha watu wengine. Halikadhalika, kuwapa watu au kaumu zao lakabu na majina yasiyopendeza na kuwaita watu kwa lakabu na majina machafu husababisha vinyongo, chuki na uadui kati ya pande mbili. Kwa sababu hiyo Allah SWT ameyaeleza hayo kuwa ni madhambi na kwamba kutotubia na kutoacha tabia hiyo chafu ni alama na kielelezo cha dhulma ambayo mtu anawafanyia wenzake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kumwamini Mwenyezi Mungu hakuendani na kuwadharau na kuwadunisha waja wa Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kuwadharau na kuwadunisha watu na kaumu zingine ni alama ya kujikweza na kujiona bora. Qur'ani tukufu inakabiliana na tabia hii chafu kwa kusema: haifai kujiona bora kuliko wengine, huenda wale mnaowadharau wakawa wabora kuliko nyinyi. Vilevile aya hii inatubainishia kuwa, kufichua aibu za watu na kuwasema kwa ubaya kutawachochea na wao pia kufichua aibu zetu na kuanika ila na kasoro zetu. Kwa maneno mengine ni kwamba, kuwasema watu wengine kwa ubaya si barabara ya upande mmoja. Kwani kama si leo ni kesho, suala hilo litageuka kuwa la pande mbili kwa watu wengine kutangaza aibu zetu na kutusema na sisi pia kwa ubaya. Halikadhalika aya hii inatutaka tuelewe kwamba moja ya malengo ya kimkakati na ya uono wa mbali ya Uislamu ni kuyafanya mazingira ya jamii yasalimike na tabia mbaya na chafu na kuepusha mivutano na mapigano ya kijamii.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 12 ambayo inasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ ۖ وَلَا تَجَسَّسُوا وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا ۚ أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَن يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ ۚ وَاتَّقُوا اللَّهَ ۚ إِنَّ اللَّهَ تَوَّابٌ رَّحِيمٌ
Enyi mlio amini! Jiepusheni na dhana nyingi, hakika baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipeleleze, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! anapenda mmoja wenu kuila nyama ya nduguye aliye kufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba, Mwenye kurehemu.
Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyopita kwa kuzungumzia mifano mitatu mingine ya madhambi, yanayodhoofisha uhusiano wa kiudugu baina ya wanajamii. Japokuwa Qur'ani inawausia Waislamu kila mmoja kuwa na dhana njema kwa mwenzake, lakini kwa masikitiko, baadhi ya watu huwa na dhana mbaya kwa wenzao. Kwa kutegemea tetesi, shaka na dhana tu, na bila ya kuwa na hoja wala ushahidi, watu hao hupeleleza na kuchunguza mambo ya wenzao na kuishia kuwazushia tuhuma bila ya kisa wala sababu. Kusengenya ni kuwaeleza kitu watu wasichokijua kuhusu mtu, bila mtu huyo mwenyewe kuwepo, kitu ambacho kama atakuja kusikia ataudhika. Katika aya hii ya 12 ya Suratul-H'ujuraat, kusengenya kumefananishwa na kula nyama ya mtu aliyekufa. Kwa sababu wakati msengenyaji anapomchafulia mtu heshima yake mbele za watu, kwa kuwa mtu huyo huwa hayupo kwenye hadhara hiyo na hawezi kujitetea nafsi yake, heshima yake aliyoharibiwa huwa haiwezi kurudi tena kama ilivyokuwa. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, katika jamii ya Kiislamu, msingi na asili huwa ni kutowatia watu hatiani, kuaminiana na kudhaniana dhana njema. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kuwatilia shaka watu ndio chanzo cha kupeleleza mambo yao na hatimaye kuwasengenya na kuanika aibu zao. Aidha, aya hii inatuelimisha kwamba, moja ya mbinu za kuwahadharisha watu na mambo maovu ni kutumia hisia za kiutu. Kwa mfano katika aya hii, mtu anayesengenywa na kusemwa kwa ubaya ametajwa kuwa ni ndugu aliyekwisha fariki na asiye na uwezo wa kujitetea. Vilevile aya hii inatutaka tufahamu kuwa, hakuna mkwamo wowote katika dini tukufu ya Uislamu. Hata kama madhambi ya mtu yatakuwa makubwa kiasi gani, yanaweza kusamehewa na kufidiwa kwa toba ya kweli, kwa sababu Allah SWT anapokea sana toba, Naye ni mrehemevu na mwenye huruma kwa waja wake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 946 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atutakase na maradhi mbalimbali mabaya na machafu ya nafsi, yakiwemo ya kusengenya, ambayo yanatuhilikisha wengi miongoni mwetu kwa kututeketezea thawabu za amali zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/