Sura ya H'ujuraat, aya ya 13-18 (Darsa ya 947)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 947 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 49 ya H'ujuraat. Tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya yake ya 13 ambayo inasema:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا ۚ إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ
Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekufanyeni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye khabari.
Kama tutajaalia wapenzi wasikilizaji kwamba watu wote duniani wana asili na rangi moja na wanazungumza lugha moja na wanafanana kimaumbile na kulingana katika mambo yao yote, hapo itabidi tujiulize, katika hali kama hiyo itawezekana kweli kuwatambua na kuwapambanua watu? Kwa kweli mojawapo ya neema za Mwenyezi Mungu inayobainisha hekima na uwezo wake mutlaki usio na mpaka ni kutafautiana wanadamu katika hali mbalimbali, ambako kumekuwa sababu ya kupatikana aina kwa aina za watu, wa rangi, asili na lugha tofauti. Lakini mbali na hayo, katika kila kaumu ya watu wa rangi na asili fulani, kila mtu ana hali za namna ya peke yake zinazomtafautisha na mwenzake, kiasi kwamba hata mapacha wawili waliofanana kupita kiasi, hawawi sawa katika kila kitu. Kwani wazazi wao na jamaa zao wa karibu huweza kuwapambanua na kuwatambua. Katika aya hii tuliyosoma, Qur'ani tukufu imeashiria msingi huo wa kutofautiana watu katika maumbile ya kimwili pamoja na mbari zao na kusema: siri ya kuwepo tofauti hizi ni kuwawezesha watu kutambuana ili wasipatwe na matatizo katika mahusiano yao ya kijamii na katika kuamiliana kwao. Hapana shaka kwamba, kuna watu wa asili, rangi na wa baadhi ya kaumu na makabila wanaozichukulia tofauti hizo kuwa ni alama ya ubora. Hali ya kuwa aya hii inaeleza kinagaubaga kwamba: nyinyi nyote mnatokana na baba mmoja na mama mmoja, na asili yenu nyote ni Adam na Hawa. Kwa hiyo hakuna sababu yoyote ya kujitukuza na kujiona bora, kwani watakaokirimiwa na kupewa heshima maalumu mbele ya Mwenyezi Mungu ni wale tu watakojijenga kiroho na kinafsi na kufikia daraja ya juu ya ukamilifu wa kiutu na kidini. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, si mwarabu kwa asiye mwarabu, wala mweupe kwa mweusi, aliye na ubora wa aina yoyote ile. Wote hao ni watu na watoto wa baba mmoja na mama mmoja. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kwamba, kuwa mwanamme au mwanamke au watu kuwa na tofauti zinazoonekana za maumbo, sura, rangi na asili kumefanywa kwa hekima, na ili waweze kujuana na kutambuana, si kwa ajili ya kujivuna na kujiona bora. Wa aidha aya hii inatutaka tujue kuwa, Qur'ani imetupilia mbali aina zote za ubaguzi, kuanzia wa rangi, kaumu, kabila, wa kijamii au mwingine wowote ule; na kipimo pekee ulichoweka cha kuwafadhilisha na kuwatukuza watu, ni usafi na utakasifu wa nafsi zao na uchamungu wao.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 14 na 15 za sura yetu ya H'ujuraat ambazo zinasema:
قَالَتِ الْأَعْرَابُ آمَنَّا ۖ قُل لَّمْ تُؤْمِنُوا وَلَٰكِن قُولُوا أَسْلَمْنَا وَلَمَّا يَدْخُلِ الْإِيمَانُ فِي قُلُوبِكُمْ ۖ وَإِن تُطِيعُوا اللَّهَ وَرَسُولَهُ لَا يَلِتْكُم مِّنْ أَعْمَالِكُمْ شَيْئًا ۚ إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ
Mabedui wamesema: Tumeamini. Sema: Hamjaamini, lakini semeni: Tumesilimu; maana Imani haijaingia bado katika nyoyo zenu. Na mkimt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hatakupunguzieni chochote katika (malipo) ya amali zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْتَابُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ ۚ أُولَٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ
Hakika Waumini ni wale tu walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake tena wasitie shaka, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao. Hao ndio wakweli.
Aya hizi zinawazungumzia watu wanaojinasibu kuwa wameamini kwa kusema: "Sisi tumemwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake" na kulifanya hilo kuwa jambo la kujivunia na kujifakharisha kwa wengine. Lakini Qur'ani inasema: wao wanatamka kwa ndimi zao tu kuwa ni Waislamu na wameamini, lakini katika amali na matendo hawajajisalimisha kwa kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hali ya kuwa imani na matendo yamefungamana na yanategemeana; kwani kila moja bila ya mwenzake huwa halina thamani. Sehemu inayofuatia ya aya inaashiria alama mbili za kuthibitisha kuwa imani imepenya kweli ndani ya nafsi za watu kwa kusema: muumini wa kweli ni yule asiye na chembe ya shaka ndani ya nafsi yake wala kusuasua juu ya ukweli wa njia ya Mwenyezi Mungu. Jengine ni kwamba, huwa tayari kuitoa mhanga roho yake na mali zake katika njia ya dini na kuisabilia nafsi yake katika medani hiyo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mtu anayejidai kuwa ameshika dini wakati matendo yake hayaendani na mafundisho ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hapa duniani ataendelea kupata upendeleo wa kuhesabika kuwa Muislamu; lakini Uislamu huo hautamfalia kitu huko akhera. Funzo jengine tunalopata katika aya hizi ni kuwa, kitovu cha imani kiko moyoni mwa mtu si kwenye ulimi wake; na njia ya kuifikia imani, ni utiifu wa kimatendo; si matamshi matupu yatamkwayo na ulimi. Kwa maneno mengine ni kuwa, amali ndiyo uthibitisho wa imani ya moyoni mwa mtu. Aidha aya hizi zinatutaka tufahamu kwamba, mbali na Qur'ani, ambayo ni maneno ya Allah, amri na mafundisho ya Bwana Mtume SAW, nayo pia ni sehemu ya dini na ni wajibu kuyafuata. Halikadhalika aya hizi zinatuonyesha kuwa, medani ya Jihadi na kuihami dini ya Mwenyezi Mungu ndio njia ya kupambanua ukweli wa walioishika dini kikwelikweli na uongo wa wale wanaojidai na kujigamba tu.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 16 hadi 18 za sura hii ya al-H'ujuraat ambazo zinasema:
قُلْ أَتُعَلِّمُونَ اللَّهَ بِدِينِكُمْ وَاللَّهُ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۚ وَاللَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ
Sema: Ati ndio mnamjulisha Mwenyezi Mungu Dini yenu, na ilhali Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na ardhini, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu?
يَمُنُّونَ عَلَيْكَ أَنْ أَسْلَمُوا ۖ قُل لَّا تَمُنُّوا عَلَيَّ إِسْلَامَكُم ۖ بَلِ اللَّهُ يَمُنُّ عَلَيْكُمْ أَنْ هَدَاكُمْ لِلْإِيمَانِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ
Wanakusimbulia kuwa wamesilimu! Sema: Msinisimbulie kwa kusilimu kwenu. Bali Mwenyezi Mungu ndiye aliye kufanyieni ihsani kwa kukuongozeni kwenye Imani, ikiwa nyinyi ni wakweli.
إِنَّ اللَّهَ يَعْلَمُ غَيْبَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَاللَّهُ بَصِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ
Hakika Mwenyezi Mungu anajua yaliyofichikana mbinguni na ardhini. Na Mwenyezi Mungu anayaona myatendayo.
Katika zama za Bwana Mtume SAW, baadhi ya watu walikuwa wakimfanyia masimango mtukufu huyo kwa kumwambia: Sisi ndio tuliosilimu, tukakuamini na kukusaidia. Qur'ani tukufu ikawahutubu watu hao kwa kuwaambia: maneno gani hayo yasiyo na maana mnayosema? Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio waliokufanyieni nyinyi ihsani kwa kukuleteeni uongofu, wakakutoeni kwenye giza la ujinga na ujahili na kukuongozeni kwenye njia ya nuru. Isitoshe, kama nyinyi ni wakweli kwa hayo mnayodai hakuna haja ya kueleza hayo na kumfanyia masimango Mtume, kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mjuzi na mwenye habari ya mambo yote ya mbinguni na ardhini; na anaijua pia batini na yaliyomo ndani ya nafsi zenu na anatambua vyema ni kwa kiwango gani mumeamini na kushikamana na dini yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tusione tumemfanyia ihsani Allah SWT na Mtume wake kwa sababu ya kuamini kwetu na kwa amali tunazofanya, kwa sababu wao si wahitaji wa imani wala amali zetu. Kutolewa kwenye giza la ujinga na upotofu na kuonyeshwa na kuelekezwa kwenye njia ya haki na uongofu ni neema kubwa ya Mwenyezi Mungu na ihsani isiyo na kifani ya Yeye Mola kwetu sisi. Basi Yeye Allah na Mtume wake ndio wa kutusimanga kwa ihsani yao hiyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, katika jamii ya Kiislamu tujihadhari tusije tukahadaiwa na kauli za wanaodai kwa dhahiri zao kuwa ni waumini, kwa sababu baadhi yao si wakweli kwa wanayodai. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, mbinguni na ardhini kuna siri nyingi zilizofichika na ambazo bado hazijagundulika, lakini zote hizo Allah SWT anazijua vyema. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 947 ya Qur'ani imefikia tamati, na ndiyo inatukamilishia pia tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 49 ya al-H'ujuraat. Inshallah tuwe tumeaidhika na kuelimika kwa yote tuliyojifunza katika sura hii. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuwa washukurivu wa kila neema aliyotupa, ikiwemo neema tukufu na isiyo na kifani ya Uislamu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/