May 27, 2023 06:41 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 949 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 50 ya Qaaf. Tunaianza darsa yetu kwa aya yake ya tisa hadi ya 11 ambazo zinasema:

وَنَزَّلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً مُّبَارَكًا فَأَنبَتْنَا بِهِ جَنَّاتٍ وَحَبَّ الْحَصِيدِ

Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji yaliyo barikiwa, na kwa hayo tukaotesha mabustani na nafaka zivunwazo.

وَالنَّخْلَ بَاسِقَاتٍ لَّهَا طَلْعٌ نَّضِيدٌ

Na mitende mirefu yenye makole yaliyo zaa kwa wingi, 

رِّزْقًا لِّلْعِبَادِ ۖ وَأَحْيَيْنَا بِهِ بَلْدَةً مَّيْتًا ۚ كَذَٰلِكَ الْخُرُوجُ

Ili iwe ni riziki kwa waja (wangu). Na tukaifufua kwa hiyo (mvua) nchi iliyokufa. Basi namna hivi ndivyo utakavyo kuwa ufufuaji.

Katika mwendelezo wa tuliyozungumzia katika darsa iliyopita, aya hizi zinajenga hoja na kubainisha uwezekano wa kusimama Kiyama kwa kuashiria kuchanua na kupata uhai tena miti na mimea wakati wa msimu wa machipuo. Katika msimu huo, mbegu mfu zisizo na uhai huhuika na kuchipuka ardhini baada ya ardhi hiyo iliyo mfu pia kunyeshewa na mvua. Na baada ya kugeuka kuwa mashuke marefu yaliyojaa mazao ya nafaka, wakulima huyavuna wakapata ndani yake riziki ya kujitengenezea anuai za mikate na vyakula vyao vingine. Wakati wa msimu wa baridi kali, miti nayo pia hufa, lakini unapowadia msimu wa machipuo na kunyesha mvua, matawi yaleyale ya miti hiyo yaliyokuwa yamekauka, huchanua juu yake majani mapya na hatimaye kuchipua na kumea aina mbalimbali za matunda ambayo ni ishara ya uhai wa mimea na miti. Kisha baada ya maelezo hayo, Qur'ani tukufu inaendelea kueleza kwamba, vivyo hivyo pia ndivyo kutakavyokuwa kufufuka na kutoka tena wanadamu ardhini Siku ya Kiyama. Kwa irada yake na atakapotaka Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu, chembe zote za miili ya wafu zilizokuwa zimetawanyika ndani ya tumbo la ardhi, kama zilivyokuwa mbegu za mimea, zitatoka tena ardhini na kuwa na uhai tena. Kufanyika hilo si muhali, wala si jambo lisilowezekana kwa uwezo mutlaki usio na mpaka wa Allah SWT. Baadhi ya tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, mvua, ni kitu chenye baraka nyingi sana na kipaji uhai; kwa sababu maisha ya viumbe wote wa ardhini ikiwemo mimea, wanyama na watu yanategemea mvua. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kati ya miti na matunda, mtende na matunda yake ya tende vina sifa na hali maalumu, na ndio maana Mwenyezi Mungu amevitaja peke yake. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, mimea na miti ni vitu vitoavyo mandhari nzuri na ya kuvutia ya kijani kibichi, ni wenzo wa kupatikana chakula na riziki ya viumbe na vilevile ni ishara na alama ya kuwepo tena maisha baada ya kufa. Hapana shaka watu wenye macho, uoni na akili za uzingatiaji wanayatazama mambo hayo kwa tafakuri kubwa.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 12 hadi 14 za sura yetu ya Qaaf ambazo zinasema:

كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ وَأَصْحَابُ الرَّسِّ وَثَمُودُ

Walikadhibisha kabla yao kaumu ya Nuhu na watu wa Rassi na Thamudi.

وَعَادٌ وَفِرْعَوْنُ وَإِخْوَانُ لُوطٍ

Na A'di na Firauni na ndugu wa Lut'i.

وَأَصْحَابُ الْأَيْكَةِ وَقَوْمُ تُبَّعٍ ۚ كُلٌّ كَذَّبَ الرُّسُلَ فَحَقَّ وَعِيدِ

Na watu wa Kichakani, na watu wa Tubbaa'. Wote hao waliwakadhibisha Mitume, kwa hivyo onyo langu likathibiti (juu yao).

Aya hizi zinamliwaza na kumfariji Bwana Mtume SAW na waumini kwa kuwaambia: msidhani ni washirikina wa Makka peke yao ndio wanaokadhibisha na hawaukubali ujumbe wa Nabii Muhammad SAW, kwani tangu zama za Mtume mteule wa Mwenyezi Mungu Nuh AS hadi sasa, Mitume wote waliokuja wamepingwa na kukadhibishwa. Kwa kutumia visingizio tofauti, makundi na kaumu mbalimbali za watu ziliukataa katakata wito wa haki na hazikuwa tayari kuwaamini Mitume wa Mwenyezi Mungu. Na kwa kuwa ukanushaji na ukadhibishaji huo wa haki ulitokana na inadi, taasubi na ukaidi, haukuachwa upite vivi hivi, bali watu wa kaumu hizo walifikwa na adhabu na ikabu ya Mola kwa sura tofauti. Wako miongoni mwao waliokumbwa na mafuriko na vimbunga, wako walioangamizwa kwa radi iliyowashukia kutoka mbinguni na wako waliohilikishwa kwa zilzala na tetemeko la ardhini. Miongoni mwa mambo tunayojifunza katika aya hizi ni kwamba, Mungu huyohuyo aliyeuleta ulimwengu huu wenye adhama na akamuumba na mwanadamu, amemletea pia kiumbe huyo mwongozo na uongofu kupitia Mitume wake ili aweze kufuata njia ya uongofu itakayomfikisha kwenye ukamilifu wa kiutu. Lakini pamoja na hayo, haki hailazimishwi kufuatwa; na katika jambo hili wanadamu wana hiari na uhuru wa kuchagua, ama kuamini na kuifuata haki au kuikufuru na kuipa mgongo. Halikadhalika aya hizi inatufunza kuwa, kaumu zilizopita ambazo ziliwaona Mitume kwa macho yao na ukawabainikia waziwazi ukweli wa ujumbe waliokuja nao, zilifikwa na adhabu ya Allah kwa sababu ya kukadhibisha wito huo wa haki ulioletwa na Mitume hao. Hili ni somo la ibra na mazingatio kwa waliokuja baada yao.

Aya ya 15 ya sura yetu ya Qaaf ndiyo inayotuhitimishia darsa yetu ya leo. Aya hiyo inasema:

أَفَعَيِينَا بِالْخَلْقِ الْأَوَّلِ ۚ بَلْ هُمْ فِي لَبْسٍ مِّنْ خَلْقٍ جَدِيدٍ

Kwani tulichoka kwa kuumba kwa mara ya kwanza! (hapana!) Bali wao wamo katika shaka tu juu ya uumbaji mpya.

Washirikina na makafiri wengi wanakubali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa ulimwengu na wanadamu na wala hawakanushi kuwepo kwake. Ni kwa msingi huo ndipo aya hii ikahoji: Kwani sisi tulichoka na kuemewa katika kukuumbeni nyinyi mara ya kwanza, hata tushindwe na tusiwe na uwezo wa kukuumbeni tena mara ya pili? Baadhi ya mafunzo tunayopata katika aya hii ni kwamba, shaka juu ya uwezo wa Allah SWT wa kuwaumba watu tena Siku ya Kiyama haina mashiko wala hoja yoyote ya msingi. Na sababu ni kuwa, kiumbe alichoweza kukiumba mara ya kwanza, anao uwezo wa kukirejesha kwa kukiumba tena mara ya pili. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, katika mazungumzo na majadiliano na wakanushaji itumike mbinu ya uulizaji masuali ili kuwafanya wao wenyewe wawaze na kutafakri, asaa wataweza kuibaini haki. Wa aidha aya hii inatuelimisha kwamba, wakadhibishaji na wakanushaji wa Ma’adi, yaani kufufuliwa kwa viumbe hawana hoja ya mantiki ya kutetea ukanushaji wao, bali wanaitumia na kuitaja shaka waliyonayo, kuwa ndiyo hoja na sababu ya kukanusha kwao. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 949 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaze nyoyo zetu imani ya yakini juu ya kufufuliwa kwetu, itakayotutia raghaba ya kufanya mema na kujiepusha na mabaya, ili kuifanya ya kheri na ya saada hatima yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/