Jun 04, 2023 01:27 UTC
  • Jumapili, tarehe 4 Juni, 2023

Leo ni Jumapili tarehe 15 Dhulqaada 1444 Hijria sawa na Juni 4 mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, sawa na tarehe 14 Khordad mwaka 1368 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia sawa na mwezi Juni 1989, Imam Ruhullah Musawi Khomeini (M.A) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 87. Ulimwengu wa Kiislamu uligubikwa na majonzi na huzuni kubwa kuutokana na kutangazwa kifo cha Imam.

Imam Khomeini (M.A) alizaliwa tarehe Mosi mwezi wa Mehr mwaka 1281 Hijiria Shamsia sawa na tarehe 24 Septemba 1902 katika mji wa Khomein ulioko katikati mwa Iran. Alianza kujishughulisha na siasa sambamba na masuala ya kielimu na kiutamaduni. Mapambano ya Imam dhidi ya utawala wa Shah na uingiliaji wa Marekani nchini Iran yalishtadi mwaka 1963 Milaadia sawa na 1342 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, na kupelekea Imam kubaidishwa kwa miaka 13 nchini Iraq, Uturuki na Ufaransa. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi mwaka 1357 Hijiria Shamsia sawa na tarehe 1979 kwa uongozi shupavu wa Imam Khomeini (M.A).

Imam alibobea katika taaluma mbalimbali, na mbali na kuwasomesha wanafunzi wengi na kutoa hotuba nyingi za kihistoria, alikuwa pia mwandishi hodari wa vitabu. Miongoni mwa vitabu vyake ni Tahrirul Wasilah, Kashful Asrar, Misbahul Hidayah, na Utawala wa Kiislamu na Uongozi wa Faqih.

Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran inatoa salamu za rambirambi kwa mnasaba huu wa kukumbuka siku ya kuaga dunia hayati Imam Khomeini.

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita inayosadifiana na tarehe 4 Khordad mwaka 1368 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu lilimchagua Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kuwa Kiongozi Muadhamu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Uchaguzi huo ulifanyika masaa machache tu baada ya kufariki dunia Imam Khomeini (M.A) ambapo wasia wa Imam ulisomwa mbele ya hadhirina.

Hadi sasa Ayatullah Khamenei anaendeleza njia ya Imam Khomeini MA kwa msingi wa mafundisho ya Kiislamu na ameyaongoza Mapinduzi ya Kiislamu kwa hekima, tadbiri, uono wa mbali na ustahiki.

Sayyid Ali Khamenei

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, sawa na tarehe 4 Juni mwaka 1989, wanafunzi kadhaa wa vyuo vikuu vya China waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa na polisi katika mji mkuu wa nchi hiyo Beijing.

Siku hiyo maelefu ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya China walikuwa wamekusanyika katika Medani ya Tiananmen mjini Beijing, wenye maana ya 'Amani ya Mbinguni' wakitaka kuwepo mazingira ya wazi ya kisiasa nchini humo, kupunguzwa uwezo wa chama cha kisoshalisti, kuongezwa uwezo wa Bunge na kuchaguliwa wawakilishi wake.

Ingawa serikali ya China ilipiga marufuku maandamano hayo lakini wanafunzi waliendelea kukusanyika na mwishowe askari polisi na vikosi vya jeshi vikatumia silaha kuwakandamiza wanafunzi hao.

Tukio la mauaji ya Tiananmen

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Watoto Wasio na Hatia Waathirika wa Unyanyasaji (International Day of Innocent Children Victims of Aggression).

Siku hiyo ilitangazwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1982 kwa ajili ya kushughulikia mashaka ya watoto wanaosumbuliwa na unyanyasaji wa kimwili, kiakili na kiroho kufuatia hali mbaya ya watoto wa Palestina na Lebanon wanaosumbuliwa na ukatili wa utawala haramu wa Israel.

Ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto una sura na aina mbalimbali na unasababishwa na uzembe wa wazazi, viongozi wa kitaifa na kimataifa na makatili wasio na chembe ya huruma na wasiojali isipokuwa maslahi yao ya kimaada.

 

Tags