Utepe Mwekundu: Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ukimwi
Tarehe Mosi Disemba imepewa jina la Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ukimwi na kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku hii tumewaandalia kipindi hiki maalumu cha Utepe Mwekundu kwa mnasaba wa kuwadia tarehe Mosi Disemba ambayo kila mwaka huadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ukimwi.
Ukimwi au ugonjwa wa upungufu wa kinga mwilini husababishwa na virusi vya HIV. Virusi hivi hudhoofisha seli za kinga za mwili hadi kufikia hatua ambayo haziwezi tena kupambana na magonjwa madogo madogo. Virusi vya HIV yaani (Human Immunodeficiency Virus) au VVU, yaani virusi vinavyosababisha kinga ya mwili kupungua, huathiri seli nyeupe za damu za mwili hasa Lymphocytes ambazo zina kazi kubwa na muhimu ya kupambana na maambukizi mbalimbali ya magonjwa na kuukinga mwili dhidi ya vimelea vya maradhi. Virusi hivi ni wanachama wa kundi la virusi vya Retrovirus ambavyo huambukiza seli za binadamu na kuzaliana kupitia njia ya kutumia nishati na virutubisho vya seli hizo.
Ukimwi ni hatua ya mwisho na mbaya zaidi ya maambukizi ya VVU. Watu wenye ugonjwa huu wana idadi kubwa ya seli maalumu nyeupe za damu na mfumo wa kinga ulioharibiwa, ambayo mara nyingi huambatana na ugonjwa mwingine. Utafiti umeonyesha kuwa, kama virusi vya HIV havitapatiwa matibabu ya kuvifubaza (ARVs) vitasababisha Ukimwi baada ya karibu miaka 10. Lymphocyte au seli za CD4 ni aina maalumu ya seli za damu ambazo zina jukumu kubwa katika mapambano ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali ambapo virusi vya VVU huharibu seli hizo. Kadiri seli nyingi za CD4 zinavyotoweka, ndivyo mfumo wa kinga ya mwili unavyodhoofika, na yumkini mtu akawa na VVU kwa miaka mingi kabla ya kukua na kuwa Ukimwi.
Katika hatua hii, mtu aliyeambukizwa anaweza kuwa mbebaji au carrier wa ugonjwa huo, lakini mwili wake hauonyeshi dalili yoyote. Virusi vya Ukimwi vinaweza kuwepo mwilini bila mtu kudhihirisha dalili zozote. Hata hivyo, kwa watu wengine, dalili za Ukimwi zinaweza kuonekana baada ya mwaka mmoja. Kwa kawaida dalili za ugonjwa huu zinatofautiana kulingana na ukali wake.
Virusi vya Ukimwi vinapoingia mwilini husasababisha dalili kama za mafua makali ndani ya wiki 2 hadi 4. Dalili hizi ni pamoja na: Homa, vipele, kuhara, kuumwa kichwa, uchovu, kupungua uzito, matatizo ya ngozi, uvimbe wa tezi za limfu, maumivu ya misuli na viungo, kuwasha ngozi, na maambukizi ya fangasi mdomoni na katika meno (Oral thrush).
Kupungua uzito sana, uchovu mkali bila sababu, homa kali na ya mara kwa mara na kutokwa jasho nyakati za usiku, kuhara kwa muda mrefu (zaidi ya wiki), vidonda mdomoni, sehemu za siri na sehemu ya haja kubwa, vipele vya ngozi ndani ya mdomo, kwenye kope na pua, uvimbe wa nodi za limfu shingoni, makwapani na eneo la kinena, kuwa na hali ya mfadhaiko, matatizo ya neva na kupoteza kumbukumbu ni baadhi ya dalili za ugonjwa wa Ukimwi.
Mtu aliyeambukizwa virusi vya Ukimwi hubeba virusi hivyo katika vimiminika vya mwili kama vile damu, maziwa, nk. Uambukizaji wa virusi huwezekana tu ikiwa vitu hivyo vya majimaji vilivyoambukizwa virusi vya Ukimwi vitaingia kwenye damu ya mtu mwingine. Maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa kawaida hutokea kwa njia zifuatazo: Kujamiiana bila kinga na mtu aliyeambukizwa Ukimwi au kuchangia sindano na mtu aliyeambukizwa virusi vya HIV. Njia nyingine ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi ni kupitia mama mjamzito kwenda kwa kichanga kilichoko tumboni. Mwanamke yeyote ambaye ni mjamzito au ana mpango wa kuwa mjamzito, na kwa sababu yoyote anashuku kuwa kuna uwezekano wa kuambukizwa HIV, ni muhimu kwanza kupima afya yake na kupata ushauri kuhusu HIV kabla ya kubeba ujauzito. Iwapo majibu ya uchunguzi huo wa kimaabara utaonyesha kwamba mama mjamzito ni mwathirika, anapasa kupatiwa dawa husika ambazo zitamzuia kumwambukiza mtoto. Wakati huo huo mama wenye virusi vya HIV wanashauriwa kufuata masharti na ushauri wa daktari ili kuepuka kuwaambukiza watoto wao kupitia maziwa ya mama.
Mapambano ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yanaweza kufanikiwa kwa kipindi kifupi kama wajawazito watahudhuria kiliniki kwa mara ya kwanza chini ya wiki ya 12; ili kuanza utekelezaji wa hatua za kuwakinga watoto iwapo atagundulika kuwa na virusi hivyo. Wakati huo huo mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unasisitiza umuhimu wa kufika kiliniki kwa mara ya kwanza kabla ya wiki ya 14 ya ujauzito. Hii kwa hesabu ya miezi, ni sawa na miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito.

VVU haviambukizwi kwa njia ya hewa au chakula (kwa mfano, kwa kupiga chafya au kukohoa). Ukimwi pia hauambukizwi kwa kukumbatiana na kubusiana. Huwezi kuambukizwa virusi vya HIV kupitia kuvuta hewa, kusaliminiana, kutumia pamoja vyombo vya chakula, kutumia maji pamoja, kutumia vifaa vya mazoezi, kugusa kiti cha msalani, komeo la mlango na kadhalika. Wakati huo huo nzi, mbu na wadudu wengine pia hawaenezi VVU.
Wapendwa wasikilizaji utafiti wa baadhi ya wataalamu unaonyesha kuwa virusi vya VVU vilihamishwa kutoka kwa sokwe hadi kwa wanadamu kwa mara ya kwanza barani Afrika mwanzoni mwa karne ya 20. Mnamo 1998, sampuli ya plasma ya mwaka 1959 ilichambuliwa na matokeo yake yaliyonyesha kuwa VVU-1 iliingia kwenye mwili wa binadamu karibu mwaka 1940 au mwanzoni mwa mwaka 1950. Wanasayansi wengine wanaamini virusi vya VVU viliingia katika mwili wa binadamu miaka mingi huko nyuma. Wataalamu wengi wanaamini kwamba kwa kuwa VVU vilitokana na aina ya SIV miongoni mwa jamii ya sokwe huko magharibi mwa Afrika, hivyo kesi ya kwanza HIV kwa binadamu ilianzia Afrika Magharibi, na kisha maambukizi yakaenea duniani kote.
Ingawa yumkini kwamba sokwe hakuwa chanzo cha asili cha kuenea VVU, na huenda maambukizi ya virusi hivyo yalitokea baina ya wanadamu katika zaidi ya eneo moja, kuna uwezekano mkubwa kwamba virusi hivyo viliibuka huko Amerika ya Kusini na Afrika kwa wakati mmoja. Huwenda ikawa vigumu kutaja mahali hasa ambapo kwa mara ya kwanza virusi vya HIV viligunuduliwa lakini ni wazi kuwa katikati ya karne ya 20 maambukizi ya HIV yalienea pakubwa duniani.
Kuhusu takwimu za ugonjwa wa Ukimwi duniani; ripoti iliyotangazwa katika tovuti ya Umoja wa Mataifa kama takwimu za kimataifa kuhusu Ukimwi inaonyesha kuwa: "Mwaka 2021 watu milioni 38 na laki 4 walikuwa wakiishi na VVU duniani. Aidha watu milioni moja na laki tano waliambukizwa virusi vya Ukimwi na 650,000 waliaga dunia kwa ugonjwa huo ambapo watoto na mabarobaro walikuwa 110,000.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, watu milioni 84 na laki mbili waliambukizwa Ukimwi na milioni 40 na laki moja wamepoteza maisha tangu kuibuka maambukizi ya ugonjwa huo.
Kulingana na taarifa zilizopo, maambukizi mpya ya HIV duniani kote yamepungua kwa kiasi kikubwa katika muongo uliopita. Hata hivyo huko Magharibi mwa Asia na Kaskazini mwa Afrika hali ni tofauti. Dunia imepitisha kipindi kirefu tangu kupamba moto maambukizi ya Ukimwi mwaka 1996; ammbapo katika kipindi cha baina ya miaka ya 2010 hadi 2021 idadi ya maambukizi mapya ya virus ivya HIV duniani yalipungua kwa asilimia 32 lakini idadi ya maambukizi mapya huko Asia Magharibi na Kaskazini mwa Afrika yaliongezeka kwa asilimia 33 katika kipindi hicho.
Siku ya Kimataifa ya Ukimwi ilianishwa mwaka 1988 kwa ajili ya kuongeza uelewa, kuelimisha na kupiga vita unyanyapaa. Umuhimu wa maadhimisho ya siku hiyo ni kuwakumbusha walimwengu kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika mapambano na maradhi haya yasiyo na tiba. Utepe Mwekundu ni moja ya nembo zilizotambulikwa kwa ajili ya ugonjwa huu ukiwa na maana ya kuwa na ufahamu na kuwasaidia watu walioathirika na VVU.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Ukimwi Duniani mwaka huu wa 2023 ni "Remember and Commit. Asanteni wapendwa wasikilizaji kwa kuwua nasi katika kipindi hiki.Tunawatakia afya njema, na Mungu awabariki.
