Udiplomasia wa Kihollywood au Hujuma ya Kisiasa?
Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nasi tena katika kipindi chetu cha Makala ya Wiki. Ni matumaini yangu kuwa utaendelea kuwa nami hadi mwisho wa makala ya leo itakayozungumzia nafasi ya Hollywood katika siasa za nje za Marekani.
Hii leo imethibitika kuwa sekta ya filamu ya Marekani, Hollywood inatumikia na kupeleka mbele zaidi malengo na siasa za kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine za serikali ya Washington kuliko hata Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Ulinzi na hata shirika la ujasusi la Marekani CIA. Hollywood imekuwa ikitumia umashuhuri wa waandishi, waongozaji na waigizaji na kuwatumia katika maeneo mbalimbali ya dunia kama mabalozi wa kupeleka mbele sera za kikoloni za Marekani.
Taasisi zinazoshughulikia sera na siasa za nje za Marekani zimekuwa zikitumia maelfu ya watu wenye taaluma za masuala mbalimbali kama wataalamu wa masuala ya kiutamaduni na kijamii, mamia ya taasisi za kisiasa na vituo vya uchunguzi na utafiti kwa ajili ya kufikia malengo yao ya kimataifa. Hata hivyo inaonekana kuwa waandishi, watengenezaji, waongozaji na waigizaji wa filamu ndio wanaotumiwa zaidi kutokana na umashuhuri wao mkubwa.
Mwezi Machi mwaka 2012 habari ya kukamatwa mwigizaji na mtengeneza filamu mashuhuri George Clooney iliwaacha bumbuazi Wamarekani wengi wa kawaida. Mtengeneza filamu huyo mashuhuri wa Hollywood alitiwa nguvuni pamoja na baba yake wakiwa kwenye maandamano ya kupinga ukiukaji wa haki za binadamu nchini Sudan mbele ya ubalozi wa nchi hiyo mjini Washington. Hapa linakuja swali kwamba, kuna uhusiano gani baina ya George Clooney na nchi kama Sudan?
Sudan ni nchi ya tatu kwa ukubwa barani Afrika na ina idadi kubwa zaidi ya Waislamu. Nchi hiyo ina umuhimu mkubwa wa kistratijia kutokana na kuwa jirani na Bahari Nyekundu. Waislamu ambao ndiyo jamii kubwa zaidi ya Sudan wanaishi maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo na Wakristo wachache wanaishi maeneo ya kusini na jamii nyingine ndogondogo za kidini. Kutokana na hali hiyo na vilevile hitilafu za kikabila zilizopandikizwa au zinazochochewa na wakoloni, Sudan daima imekuwa uwanja wa tamaa za madola ya kibeberu.
Vita vya ndani nchini Sudan kati ya makabila ya kusini mwa nchi hiyo na serikali kuu ya Khartoum vilianza miaka 50 iliyopita sambamba na uhuru wa nchi hiyo. Katika kipindi cha vita vya ndani Sudan iliendelea kubakia nyuma kwa miaka mingi kutokana na njama za aina mbalimbali za madola ya kibeberu licha ya kuwa na utajiri wa gesi na mafuta. Wamagharibi waliyapa makabila ya kusini aina mbalimbali za silaha na kuchochea vita vya ndani vilivyoendelea kwa miongo kadhaa. Katika vita hivyo baadhi ya makabila yalidhibiti maeneo ya kusini na kuyaruhusu makampuni ya mataifa kadhaa kufaidika na utajiri wa maliasili ya Sudan kwa miaka mingi.
Hatua iliyofuata ilikuwa ya kutekeleza mpango wa kikoloni wa kuigawa Sudan, njama ambayo ilikwenda sambamba na kusalimu amri baadhi ya makundi ya waasi na kuzidishwa mashinikizo ya kisiasa ya Wamagharibi. Njama hiyo ilifikia malengo yake na serikali ya Sudan ikachukua uamuzi wa kuitisha kura ya maoni juu ya suala la kujitenga neo la Kusini mwa nchi hiyo. Baada tu ya kutangazwa habari hiyo Marekani ilianzisha operesheni kubwa nchini Sudan na majeshi ya Hollywood yalipewa nafasi kubwa zaidi katika operesheni hiyo.
Moja kati ya operesheni za waziwazi za Marekani katika uwanja huu ni kuanzisha satalaiti ya ujasusi ambayo gharama zake zilitolewa na George Clooney. Mtengenezaji huyo mashuhuri wa filamu wa Marekani alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na taathira kubwa katika kupanga stratijia za Marekani kabla ya kura ya maoni ya Sudan.
Clooney ambaye kwa miaka mingi amekuwa katika medani ya siasa, alitumia umashuhuri wake kimataifa kuwaelekeza walimwengu kwenye stratijia za serikali ya Washington kuhusu masuala ya Sudan. Hapa inatupasa kukiri kwamba, kuwaelekeza walimwengu kwenye masuala ya ndani ya Sudan si jambo baya hasa kwa kutilia maanani matatizo yanayoshuhudia nchini humo kama ukatili dhidi ya wanawake na watoto na ukiukaji wa haki za binadamu. Hata hivyo tatizo lililopo hapa ni kwamba, kazi hiyo haikufanyika kwa sababu ya kuwaonea huruma Wasudan, bali suala hilo lilitumiwa kama ngazi na mawimbi yaliyodandiwa na Marekani kwa ajili ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi huru na kutimiza malengo yake ya kisiasa.
George Clooney alifanya jitihada kubwa na kuweza kuhalalisha vikwazo vya Marekani dhidi ya Sudan. Hata hivyo ni wazi kuwa, vikwazo hivyo havikuwa na madhara isipokuwa kwa raia wa kawaida wa nchi hiyo. Hii ni pamoja na kuwa msanii huyo angetumia umashuhuri wake kuishawishi serikali ya Marekani na jumuiya za kimataifa kwa ushirikiano wa Umoja wa Afrika kufanya jitihada za kutatua mgogoro wa Sudan.
Si hayo pekee yaliyofanywa na George Clooney kuhusiana na Sudan. Mwaka 2010 msanii huyo alitengeneza filamu aliyoipa jina la "Mwisho wa Mchezo nchini Sudan". Vilevile alikutana na Rais Barack Obama wa Marekani na kumuomba asitishe ukiukaji wa haki za binadamu nchini Sudan. Mbali na hayo alianzisha kampeni kubwa ya kihollywoodi na kutayarisha mazingira kutumwa majeshi ya Marekani huko Sudan. Katika kampeni hiyo George Clooney aliwashirikisha Emmanuel Jal ambaye ni muimbaji wa Kisudan anayeishi Canada, Alicia Keys na Peter Gabriel ambao wote ni wasanii mashuhuri katika nchi za Magharibi. Wasanii hao watatu waliungana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan na rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter na kusambaza video ya muziki iliyopewa jina la Tunataka Amani" (‘We Want Peace’). Video hiyo ilitoa ujumbe kwa watu wa Sudan kwamba wana haki ya kuitisha kura ya yaini ya kujenga eneo la kusini.
Januari mwaka 2011 kulifanyika kura ya maoni na takwimu zinasema asilimia 98 ya watu wa Sudan Kusini walipigia kura kujitenga na kujitawala eneo hilo. Kwa utaratibu huo Sudan Kusini ilitambuliwa kuwa nchi ya 55 ya Afrika na mwanachama rasmi wa 196 wa Umoja wa Mataifa.
Kwa sasa na baada ya kupita miaka kadhaa habari za msanii huyo kuhusiana na Sudan Kusini zimeteka tena kurasa za magazeti na vyombo vya habari. Hivi karibuni George Clooney na mwigizaji, mtengenezaji na mwongozaji wa filamu wa Marekani, Don Cheadle walichapisha ripoti rasmi kuhusu vita vya Sudan Kusini katika gazeti la Washington Post. Inasemekana kuwa, ripoti hiyo ni matokeo ya uchunguzi wa kipindi cha miaka miwili huko Sudan Kusini. Ripoti hiyo imefichua mengi kuhusu uhusiano baina ya Rais wa Sudan Kusini na makamu wake, na harakati na kazi za mabenki ya kimataifa, makampuni ya mataifa kadhaa ya mafuta, makampuni ya madini na makampuni ya biashara ya silaha nchini Sudan Kusini. Ripoti hiyo imeonesha jinsi miamala ya makampuni hayo ilivyosaidia kudumisha vita na mapigano ya umwagaji damu mkubwa zaidi katika historia ya sasa ya dunia.
Ripoti hiyo inasema: Katika nchi changa zaidi duniani ya Sudan Kusini maelfu ya watu wamepoteza maisha katika vita vya kutisha vya ndani na wengi wao wamelazimika kukimbia ardhi na makazi yao. Idadi kubwa ya watu wamebakwa na kunajisiwa, watoto wanatumiwa kama wapiganaji vitani na watu milioni tano wanasumbuliwa na njaa na wanahitaji misaada ya dharura ya chakula na dawa.
Sehemu muhimu zaidi ya ripoti hiyo inahusu habari za ndani juu ya jinsi wababe wa vita wanavyotumia fursa hiyo kwa ajili ya kununua milki nje ya nchi, magari ya kifahari, vilevile kununua hisa katika masoko ya kimataifa, makampuni ya mafuta na mashirika ya madini ya mataifa kadhaa na katika mabenki mbalimbali. Maeneo mengine yanayotumiwa na wababe wa vita wa Sudan kusini kwa ajili ya kuwekeza ni majumba ya kasino na mashirika ya ndege.
Jambo la kutiliwa maanani ni kuwa, George Clooney ambaye hadi miaka ya hivi karibuni hakuacha kufanya kila liwezekanalo kwa ajili ya kujitenga Sudan Kusini akisisitiza kuwa ndiyo njia pekee ya kuwaokoa watu wa eneo hilo, sasa ametoa wito wa kubuniwa statijia mpya ya kukabiliana na wababe wa vita na kurejeshwa amani katika nchi hiyo.
Yote tuliyoyasema kuhusu masuala ya Sudan na matukio ya miaka kadhaa ya nchi hiyo yanathibitisha kwamba, masuala kama utamaduni na vita laini vimepata uhimu mkubwa zaidi katika dunia ya sasa kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Utamaduni umekuwa wenzo wenye nguvu na taathira kubwa katika maisha ya watu wa zama hizi na inasikitisha kuona kwamba, watu wengu duniani wanahadaiwa na kuvutwa na utamaduni na vyombo vya habari vya Kimarekani.
Miongoni mwa mbinu zinazotumiwa katika siasa za nje za Marekani ni kueneza utamaduni na mwenendo wa kimaisha wa nchi hiyo katika mataifa mengine duniani. Siasa huzo zinatekelezwa sana kupitia watu mashuhuri, sanaa na utamaduni. Hollywood ambayo ni silaha laini ya Marekani ina nafasi muhimu na kubwa sana katika uwanja huo na filamu na waigizaji mashuhuri wa Hollywood ni mithili ya risasi ya kwanza kabisa inayofyatuliwa na Marekani lakini mara hii si katika miili ya taifa linalohujumiwa na kushambuliwa, bali katika fikra, akili na nafsi zao.
Kwa utaratibu huo tunaona kuwa Holywood daima huenda sambamba kuhudumia siasa za nje za Marekani na kufanya kazi ambazo awali na katika miaka ya nyuma zilikuwa zikifanywa kupitia mashambulizi na hujuma za kijeshi.