UNESCO yapinga njama za kuiyahudisha Baitul Muqaddas
Eneo la Baitul Muqaddas (Jerusalem) na Haram tukufu ya Msikiti wa al Aqsa limekuwa likizusha hitilafu na migogoro kwa miaka mingi.
Umoja wa Mataifa unayatambua maeneo hayo kuwa yanakaliwa kwa mabavu na umeutaka utawala ghasibu wa Israel uondoke katika maeneo hayo na kurudi katika mipaka ya kabla ya vita vya siku sita kati ya Waarabu na Israel hapo mwaka 1967. Katika upande mwingine Israel inataka mji wa Baitul Muqaddas utambuliwa kuwa ni mji mkuu wa nchi ya Kiyahudi huku Wapalestina wakifanya harakati za kukomboa eneo la mashariki mwa mji huo na kutambuliwa kuwa ni mji mkuu wa nchi huru ya Palestina.
Siku chache zilizopita Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) lilipasisha azimio lililoashiria tu jina la Kiislamu la Haram Tukufu na kupuuza kabisa jina la "Temple Mount" linalotumiwa na Mayahudi kwa ajili ya Haram tukufu ya Baitum Muqaddas. Azimio hilo pia limelaani ukatili unaofanywa na Israel dhidi ya Waislamu katika eneo hilo tukufu na kusisitiza udharura wa kulindwa turathi za Wapalestina na sifa kuu za Baitul Muqaddas Mashariki.
Azimio hilo la UNESCO limeutaja utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni utawala ghasibu na vamizi na kukumbusha majukumu yake kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Vilevile limetumia majina ya Kiislamu kuashiria maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel na kusisitiza kuwa, maeneo hayo ukiwemo Ukuta wa Magharibi unaoitwa na Wayahudi kuwa ni "Western Wall" yanaheshimiwa na dini zote za mbinguni.
Azimio la UNESCO limeutaka utawala ghasibu wa Israel urejeshe udhibiti na masuala ya Msikiti wa al Aqsa katika hali ya kabla ya mwaka 2000 ambapo ulikuwa ukisimamiwa na Idara ya Waqfu ya Jordan. Sehemu moja ya kifungu nambari 8 cha azimio hilo inasema kuwa: UNESCO inalaani vikali uvamizi wa Israel na vizuizi visivyo vya kisheria vinavyowekwa na utawala huo dhidi ya wafanyakazi wa Idara ya Waqfu na kuwazuia Waislamu kuingia katika meneo yao matukufu na ya ibada kama Masikiti wa al Aqsa.
Kifungu nambari 9 cha azimio hilo kimesisitiza kuwa, Israel ndiyo inayopaswa kulaumiwa kutokana na mashambulizi yanayofanywa na Wayahudi wenye misimamo mikali dhidi ya Msikiti wa al Aqsa. Azimio hilo la UNESCO pia limelaani na kukemea vikali uvamizi unaofanywa mara kwa mara na Israel dhidi ya turathi na haki za Wapalestina, wanazuoni wa kidini na misikiti, kuwatia nguvuni na kuwajeruhi Waislamu wanaoshiriki katika ibada na shughuli za kidini.
Azimio hilo pia limelaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi unaofanywa na Israel katika ardhi ya Palestina, kutengwa njia makhsusi za Wayahudi na ujenzi wa ukuta unaotenganisha eneo la zamani la Al Khalil na kusisitiza udharura wa kusimamishwa ukatili unaofanyika kwa mpangilio maalumu dhidi ya raia wa Palestina na uchochezi wa walowezi na makundi yenye misimamo mikali ya Kiyahudi dhidi ya Wapalestina hususan watoto wadogo na wanafunzi.
UNESCO pia imeeleza masikitiko yake makubwa kutokana na hatua ya Israel ya kukataa kuyaondoa maeneo mawili ya kale katika orodha ya turathi za Kiyahudi na kuutaka utawala huo ghasibu utekeleze maazimio yaliyotolewa huko nyuma dhidi ya Israel.
Kwa kutilia maani hatua ya Israel ya kukataa kutekeleza maazimio ya hapo awali ya UNESCO, imeamuliwa kuwa, maudhui ya Palestina ijadiliwe tena katika kikao kijacho cha jumuiya hiyo ya Umoja wa Mataifa chini ya anwani ya Palestina Inayokaliwa kwa mabavu. Azimio la UNESCO limepasishwa kwa kura 24 za ndiyo na sita za kupinga. Wajumbe wengine 6 hawakupiga kura.
Utawala haramu wa Israel umeamua kusimamisha ushirikiano wake na UNESCO kama alama ya kulalamikia azimo hilo. Waziri wa Elimu wa Israel amemwandikia barua Katibu Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova akilituhumu shirika hilo kuwa eti limepuuza uhusiano wa maelfu ya miaka wa Wayahudi na Baitul Muqaddas na kwamba, limetetea alichokiita "ugaidi wa Kiislamu". Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema, UNESCO imeendeleza mchezo wake wa kuigiza na wenye maafa. Mfasiri wa redio ya utawala haramu wa Israel, Mushe Emir amesema taasisi za Umoja wa Mataifa hazina haya na kwamba viongozi wa taasisi hizo wanapaswa kujiepusha na siasa na kukaa kando. Nukta ya kutiliwa maanani zaidi ni kwamba Mushe Emir amesema azimio la UNESCO limekariri maneno yanayosemwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran!
Uhusiano wa Israel na UNESCO umekuwa na mivutano tangu mwaka 2011 wakati shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilipotambua rasmi uanachama wa Palestina.
Baada ya kupasishwa azimio hilo Katibu Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova alitoa taarifa akisisitiza umuhimu wa kulindwa turathi za kiutamaduni, kidini na kihistoria za mji wa Baitul Muqaddas. Irina Bokova amesema kuwa, Kama ilivyosisitizwa katika vikao viliyopita vya UNESCO, Jerusalem ( Baitul Muqaddas) ni mji mtakatifu kwa dini zote zinazompwekesha Mwenyezi Mungu za Uyahudi, Ukristo na Uislamu na kwamba, mji huo umewekwa kwenye orodha ya turathi za dunia kwa ajili ya kuenzi na kutukuza muungano huo wa kiutamaduni na kidini.
Ameongeza kuwa, turathi za Baitul Muqaddas haziwezi kugawanyika na kwamba, kila jamii zilizopo katika mji huo zina haki kutambua rasmi historia na mfungamano wake na mji huo. Vilevile amepinga hatua yoyote ya kukana na kufuta ada na turathi zinazohusiana na Uislamu, Ukristo na Uyahudi za mji huo.
Irina Bokova amesema kuwa, wajibu wa jumuiya hiyo ni kueneza moyo wa kustahamiliana na kuheshimu historia na kwamba, yeye kama Katibu Mkuu wa UNESCO na nchi zote wanachama zinafungamana na suala hilo.
Jambo la kuzingatia zaidi katika azimio la sasa la UNESCO kama yalivyokuwa maazimio mengine yanayohusiana na ukatili wa Israel, ni idadi kubwa ya wawakilishi waliokataa kupiga kura au ambao hawakuhudhuria kikao cha kupiga kura zikiwemo nchi kama Uhispania, Ufaransa, Italia, Argentina, Uganda, Kenya, Korea Kusini na Sri Lanka. Nchi nyingi kati ya hizo zinautambua utalii kuwa ni sekta inayoingiza pato kubwa zaidi la kigeni na kiuchumi lakini sasa zimekhitari kunyamaza kimya mbele ya uvamizi wa Israel dhidi ya Msikiti wa al Aqsa ikiwemo Uhispania ambayo huingiza mamilioni ya dola za Marekani kila mwaka kutokana na pato la watalii wanaotembelea misikiti mikubwa ya nchi hiyo.
Miezi sita iliyopita UNESCO ilipasisha azimio kama hilo mbalo liliungwa mkono na nchi kadhaa za Ulaya zikiongozwa na Ufaransa. Hata hivyo mara hii kama lilivyoripoti gazeti la Guardian la Uingereza, lobi na makundi ya mashinikizo ya Kizayuni yameweza kuzishawishi nchi za Ulaya zisipigie kura azimio la UNESCO.
Katika upande mwingine msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria azimio hilo la UNESCO dhidi ya Israel na kulipongeza shirika hilo la kimataifa kwa kuthibitisha haki za kidini za Waislamu kuhusu Msikiti wa al Aqsa na kutetea haki za wananchi wa Palestina. Bahram Qasemi amesema kuwa, hasira za utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya hatua hiyo ya UNESCO zimedhihirisha njama za utawala huo za kutaka kuzifadaa fikra za walimwengu na kutowajibika kuhusu maazimio na sheria za kimataifa.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa kabla ya hapo Shirika la UNESCO liliutangaza mji wote wa Quds kuwa ni mji mkuu wa utawala ghasibu wa Israel, uamuzi ambao ulilaaniwa vikali na nchi na jumuiya mbalimbali za kimataifa. Wakati huo makundi ya kupigania uhuru ya Palestina na nchi za mbalimbali duniani ziliitaja hatua hiyo kuwa inakiuka sheria za kimataifa na kuunga mkono utawala vamizi. Jumuiya hizo zilisema, uamuzi huo unakiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanayolitambua eneo la Quds Mashariki kuwa linakaliwa kwa mabavu na Israel.
Alaa kulli hal, kupasishwa kwa azimio la sasa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa kunaweza kufidia makosa yaliyofanywa huko nyuma na jumuiya hiyo na kudhihirisha sehemu ndogo ya sura halisi na ya kikatili ya utawala ghasibu na vamizi wa Israel.