Dec 01, 2016 05:17 UTC
  • Siku ya Kimataifa ya Ukimwi

Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni katika Makala ya Wiki ambayo juma hili inazungumzia Siku ya Kimataifa ya Ukimwi inayoadhimishwa kila mwaka tarehe Mosi Disemba.

Tarehe Mosi Disemba kila mwaka imeainishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Ukimwi. Hatua ya WHO ya kuainisha siku maalumu kuwa Siku ya Kimataifa ya Ukimwi ilichukuliwa kwa lengo la kuwazindua wanadamu, kutoa mafunzo na kupambana na ubaguzi na kuwanyanyapaa wagonjwa wa Ukimwi na vilevile kuzitanabahisha serikali na jamii katika nchi mbalimbali kuhusu hatari inayosababishwa na ugonjwa huo.  

Siku ya Kimataifa ya Ukimwi

Japokuwa inadaiwa kuwa ugonjwa wa Ukimwi ulianzia barani Afrika lakini inajulikana wazi kuwa, ugonjwa huo ulidhihiri kwa mara ya kwanza nchini Marekani hapo mwaka 1981 baina ya mabaradhuli na watu wanaoingiliana kinyume na maumbile. Ugonjwa huo ambao  hudhoofisha kinga ya mwili ya mtu anayepatwa na maradhi hayo ulienea kwa kasi katika maeneo mbalimbali ya dunia katika kipindi kifupi na kuwa changamoto kubwa kwa mwanadamu wa leo. Hii leo inakadiriwa kuwa watu wasiopungua milioni 40 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo hatari. Vilevile takwimu zinasema kuwa, watu zaidi ya milioni 36 wanaishi na ugonjwa huo kote duniani na mamilioni miongoni mwao hawajui kama wameambkizwa ugonjwa huo.

Sababu ya ugonjwa wa Ukimwi ni kirusi cha HIV. Wataalamu wa biolojia wanasema kuwa, virusi havina uwezo wa kuishi na kubakia hai kwa kujitegemea na wala haviwezi kuzaliana. Wanasisitiza kwamba iwapo havitapata seli za kiumbe kingine hai vitaangamia katika muda mfupi. Virusi hivyo hudumisha uhai wao kwa kuingia katika seli za kiumbe hai na kusababisha maradhi na taathira muhimu kwa viumbe hivyo. Virusi vya HIV kama vilivyo virusi vingine, vinaweza kudumisha uhai wao kwa kuingia katika seli hai. Virusi hivyo hupambana na seli nyeupe za mwili wa mwanadamu na kudhoofisha kinga ya mwili mbele ya maradhi na hatimaye kusababisha ugonjwa wa Ukimwi. Virusi hivyo vina uwezo mkubwa wa kubadili muundo wake na kwa sababu hiyo hadi sasa juhudi zilizofanywa na wataalamu kwa ajili ya kutengeneza dawa na kuua virusi hivyo bado hazijazaa matunda ya kuridhisha.

Jinsi ugonjwa wa Ukimwi unavyoambukizwa na kuenea

Ugonjwa wa Ukimwi unaosababishwa na virusi vya HIV, katika awamu ya kwanza ambayo hujulikana kama kipindi cha kujificha, hukuwa taratibu sana na bila ya kujulikana. Katika kipindi hicho mtu aliyepatwa na virusi hivyo huwa haoni dalili zake na yumkini  hata asijue kwamba ameambukizwa viusi vya HIV. Huchukua kipindi cha miaka 10 hadi 15 hadi ugonjwa wa Ukimwi kudhihiri na kuonekana wazi kwa mtu aliyeambukizwa virusi vya HIV. Kwa msingi huo inakadiriwa kuwa, asilimia 40 ya watu walioambukizwa virusi vya HIV hawajui kwamba wanaishi na virusi hivyo.

Wimbi la kuenea kwa kasi virusi vya Ukimwi ambalo lilitambuliwa kuwa janga la milenia ya tatu, lilianzia America ya Kaskazini na Ulaya Magharibi. Muda mfupi baadaye ugonjwa huo wa kuambukiza ulienea katika maeneo mengine ya dunia. Kasi ya kuenea ugonjwa wa Ukimwi barani Afrika ilikuwa kubwa na yenye maangamizi ya kutisha. Kasi ya kuenea ugonjwa huo duniani ilikuwa kubwa kwa kadiri kwamba, Julai mwaka 2000 Umoja wa Mataifa ulitangaza ugonjwa wa Ukimwi kuwa ni tishio kwa usalama na amani ya kimataifa na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za dharura za kuzuia na kukabiliana nao.

   

Udharura wa kukomeshwa ugonjwa wa Ukimwi

Sisitizo hilo la jamii ya kimataifa juu ya udharura wa kupambana na Ukimwi ni kutokana na janga hilo kuharibu rasilimaliwatu ya nchi mbalimbali, suala ambalo linaweza kuwa na madhara yasiyoweza kufidika katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Kwa mfano tu ripoti ya utafiti uliofanywa na Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) inasema kuwa, kufikia mwaka 2020 wafanyakazi milioni 90 watajitenga na kazi za uzalishaji kutokana na kuathiriwa na ugonjwa wa Ukimwi. Watu walioambukizwa ugonjwa wa Ukimwi si tu kwamba hawawezi kufanya kazi, bali pia wanahitajia uangalizi makhsusi wa kitiba, kiafya, lishe maalumu na dawa zinazofaa.

Katika suala la athari mbaya za kijamii za Ukimwi katika jamii mbalimbali, tunaweza kuashiria wanawake na watoto wadogo walioathiriwa na virusi vya HIV. Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinasema kuwa, watoto karibu milioni mbili wanaishi na virusi vya Ukimwi kote duniani na nusu yao tu ndio wanaoweza kupata dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo. 

نقشه پراکنش ایدز در کشورهای مختلف جهان در سال 2011

Katika jamii nyingi za dunia ya leo ugonjwa wa Ukimwi na virusi vya HIV vinatambuliwa kuwa ni aibu kubwa kwa mtu aliyeambukizwa. Katika jamii kama hizo watu walioambukizwa ugonjwa huo hutengwa na kukataliwa katika jamii. Wakati mwingine wagonjwa wa Ukimwi hunyimwa hata haki zao za kijamii na kukabiliwa na ukatili na mienendo isiyo ya kibinadamu. Kutokana na tabia hii ya kuwanyanyapa wagonjwa wa Ukimwi, watu hawa hukumbana na mashaka na matatizo makubwa katika kutafuta kazi na ajira, nyumba, matibabu na kubaguliwa. Mienendo hii huwafanya watu walioambukizwa virusi vya HIV na ugonjwa wa Ukimwi kuishi maisha ya kutengwa na kukosa fursa ya kupata elimu, huduma na haki nyingine muhimu. Woga wa mauti na kifo, wasiwasi wa kufukuzwa katika familia na jamii, woga wa kuishi pekee, kufukuzwa kazi na kunyanyapaliwa na ndugu na marafiki huwa sababu ya watu wenye Ukimwi na virusi vya HIV kuficha hali zao za kiafya.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa, katika mwaka uliopita wa 2015 watu zaidi ya milioni mbili waliambukizwa virusi vya HIV kote duniani. Hata hiyo jambo la kutia matumaini kidogo ni kwamba, idadi ya vifo vya watu vilivyosababishwa na Ukimwi imepungua mwaka jana ikinganishwa na mwaka 2005 na inasemekana kuwa suala hilo kwa kiasi fulani linafungamana na kuongezeka taathira za dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi.

Japokuwa hadi sasa wataalamu hawajafanikiwa kugundua dawa ya kutibu Ukimwi lakini dawa za kufubaza na kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa huo zimeweza kupunguza kasi yake na hivyo kuboresha kiasi na kurefusha umri wa mtu aliyeambukizwa. Katika uwanja huu nchi zilizoendelea zimekuwa na takwimu nzuri zaidi katika kudhibiti ugonjwa wa Ukimwi na taathira zake. Utambuzi wa watu kuhusu sababu na njia za maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi katika nchi za Ulaya na Marekani umepunguza sana kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo. Wakati huo huo inasikitisha kwamba, ugonjwa huo bado unachukua wahanga wengi katika nchi zinazoendelea. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 90 ya wagonjwa wapya wa Ukimwi wapo katika nchi zinazostawi. Ughali wa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi na gharama za afya na lishe ya watu walioambukizwa ugonjwa huo ni miongoni mwa matatizo yaliyopo katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo katika nchi zinazostawi. Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa, kutopatikana dawa hizo kwa kiwango sawa kwa waathirika wa Ukimwi ni kikwazo katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo katika nchi zenye pato la chini.

Umoja wa Mataifa unatarajia kuwa, utafanikiwa kudhibiti ugonjwa wa Ukimwi kufikia mwaka 2030. Hata hivyo kunahitajika juhudi na ushirikiano wa jamii yote ya kimataifa ili kuweza kufikia lengo hilo. Kutoa mafunzo ya jinsi ya kuchunga vigezo vya fya na jinsi ya kuamiliana na waathirka wa Ukimwi kama vile sheria za kusafisha vifaa na zana zinazotumika katika tiba ya masuala mbalimbali kama meno, kutoa matibabu na huduma za afya kwa walioathiriwa na kuwapa ushauri nasaha na misaada ya kisheria vinaweza kusaidia jitihada za kupunguza na kuzuia maambukizi zaidi ya ugonjwa huo na kuboresha maisha ya walioambukizwa. 

Siku ya Kimataifa ya Ukimi

 

     

        

Tags