Imam Hussein, Nguzo ya Umoja na Mshikamano wa Kiislamu
(last modified Tue, 31 Oct 2017 10:40:22 GMT )
Oct 31, 2017 10:40 UTC
  • Imam Hussein, Nguzo ya Umoja na Mshikamano wa Kiislamu

Zimebakia siku chache tu hadi siku ya Arubaini ya Imam Hussein (as) na barabara zote za kuelekea katika mji wa Karbala nchini Iraq zimefurika watu kama mto wa maji unaoelekea katika mji mtakatifu wa Karbala.

Waislamu hao wako mbioni kuhakikisha kwamba, wanakuwa ndani ya mji wa Karbala hadi kufikia tarehe 20 Safar, siku ya arubaini tangu baada ya mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) tarehe 10 Muharram. Siku hiyo inajulikana kwa jina la Arubaini ya Imam Hussein (as). Yumkini idadi kubwa ya Waislamu wanaokadiriwa kufikia milioni ishirini isiruhusu waumini wote kufika kwenye ziara na Haram ya mtukufu huyo kwa ajili ya kuonesha mapenzi na uaminifu wao kwa Mtume na kizazi chake, lakini waumini hao wanatosheka kwa kutoa salamu kwa mbali kidogo na kusoma ziara makhsusi katika siku hiyo. 

Matembezi ya Arubaini

Katika kipindi chote cha safari ya mamilioni ya Waislamu ya kutembea kwa miguu kutoka mji mtakatifu wa Najaf kuelekea Karbala kunashuhudiwa na kusikika nara na kaulimbiu fupi lakini yenye maana kubwa inayosema "حُبُ الحسینِ یَجمَعُنا" kwa maana kwamba, penzi la Hussein linatukutanisha pamoja sote. Huu ni ukweli unaoonekana katika shughuli yote ya siku ya Arubaini ya kukumbuka mauaji ya mjukuu huyo wa Mtume (saw). Kwani mtukufu huyo ni kituo kikuu cha umoja na mshikamano wa Waislamu wa madhehebu na makundi yote waliotoka katika nchi mbalimbali za dunia kwa ajili ya kuzuru kaburi na Haram ya mjukuu wa Mtume wao, Muhammad bin Abdillah (saw). Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayati Imam Khomeini (MA) anasema: Uislamu umehimiza sana suala la umoja na mshikamano baina ya wa wafuasi wake na kufanyia kazi suala hilo. Kwa maana kwamba, dini hiyo ina baadhi ya siku ambazo matukio yake yanaimarisha umoja na mshikamano wa Kiislamu kama siku za Ashura na Arubaini ya Imam Hussein. Vilevile Qur'ani tukufu inasisitiza sana suala la kujiepusha na mifarakano baina ya Waislamu na kuwataka wawe na umoja na kushikamana katika kamba ya Mwenyezi Mungu", mwisho wa kunukuu. Kwa msingi huo siku ya Arubaini ni miongoni mwa siku za Mwenyezi Mungu ambazo Allah SW amewataka Waislamu wazitukuze na kuziadhimisha. Siku hizo ni siku zenye umuhimu mkubwa katika maisha ya mwanadamu na zinakumbusha adhama na utukufu wa Allah SW. Aya ya 5 ya Suratu Ibrahim inasema: Na tulimtuma Musa pamoja na miujiza yetu, tukamwambia: Watoe watu wako kwenye giza uwapeleke kwenye mwangaza. Na uwakumbushe siku za Mwenyezi Mungu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru

Hapa wapenzi wasikilizaji hapa linajitokeza swali kwamba, ni kwa nini mamilioni ya Waislamu wanaoshiriki katika matembezi ya siku ya Arubaini na mamilioni ya wengine waliobakia katika nchi zao wakampenda na kumuashiki kiasi hiki Abu Abdillah Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as)?

Hapana shaka kuwa mtukufu huyo hakuwa shakhsia wa kawaida, bali ni mjukuu wa Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) na mwana wa wasii wake Ali bin Abi Twalib na binti yake kipenzi Bibi Fatimatu Zahraa (as). Alikuwa mchamungu zaidi, mjuzi zaidi na shakhsia kubwa zaidi ya zama zake. Mtume (saw) alikuwa akiwasifia na kuwamtukuza Maimam Hassan na Hussein na amenukuliwa akisema kuhusu mjukuu wake huyo kwamba: "Hussein ni taa ya uongofu na safina na wokovu". Ni kwa sababu hiyo na kutokana na mauaji ya kutisha ya mjukuu huyo wa Mtume na watu wa familia yake ndiyo maana Waislamu hususan wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume, wanahuzunishwa na kusikitishwa mno na tukio la kuuliwa shahidi Imam Hussein na wakawa wanafanya shughuli maalumu za maombolezo na kumkumbuka mtukufu huyo licha ya kupita miaka na karne nyingi tangu auawe kidhulma.      

Ahlusunna katika matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein

Kumuenzi na kumkumbuka Imam Hussein si jambo linalowahusu Waislamu wa madhehebu ya Shia pekee bali Waislamu wa madhehebu za Ahlusunna pia wanampenda na kumuenzi mjukuu huyo wa Mtume wetu Muhammad (saw) na baadhi yao hushiriki katika matembezi ya siku ya Arubaini tarehe 20 Safar. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Waislamu hao wanajua vyema kwamba, mtukufu huyo hakusimama kupambana na utawala dhalimu wa Bani Umayyah kwa ajili ya maslahi yake binafsi bali kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu ya kubakisha hai dini ya Uislamu na mafundisho yake. Katika wasia wake, Imam Hussein amesema: "Sikusimama kupambana kwa ajili ya kufanya uharibifu na dhulma, bali kwa ajili ya kufanya marekebisho katika Umma wa babu yangu. Nataka kuamrisha mema na kukataza maovu na kutekeleza sira na mwenendo wa babu na baba yangu Ali bin Abi Twalib".

Lengo hilo tukufu la Imam Hussein la kutaka kuhuisha tena Uislamu uliokuwa ukiangamizwa na mtawala dhalimu wa kizazi cha Bani Umayyah, Yazid bin Muawiya linatosha kabisa kuwafanya Waislamu wote kutukuza harakati yake katika medani ya Karbala. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, katika harakati hiyo Imam Hussein (as) alisabilia kila kitu alichokuwa nacho kuanzia watoto wake, ndugu zake, masahaba zake na hatimaye nafsi yake mwenyewe kwa ajili ya kubakisha hai mafundisho sahihi ya dini ya Uislamu. Hakukubali kumtii mtawala dhalimu na fasiki kama Yazid na kwa njia hiyo akatufundisha jinsi ya kusimama imara kutetea haki na dini hata kama italazimu kusabilia nafsi na kila lililo ghali katika njia hiyo.

Mahudhurio ya Waislamu wa madhehebu za Ahlusunna katika matembelezi na shughuli ya siku ya Arubaini ya Imam Hussein (as) yanaimarisha umoja na mshikamano baina ya Waislamu wa Shia na Suni na kuwakutanisha pamoja katika harakati ya kupinga dhulma ya uonevu ya mtukufu huyo. 

Katika harakati yake ya Karbala, Imam aliwafundisha wanadamu wote somo la kuwa huru, kujitoa mhanga kwa ajili ya malengo aali na makuu, kupambana na madikteta na watawala waovu, udharura wa kuamrisha mema na kukata maovu na kadhalika. Thamani hizi haziwahusu Waislamu pekee bali wanadamu wote bila ya kujali dini, kabila na maeneo yao. Ni kwa sababu hiyo pia ndiyo maana tunawaona hata wafuasi wa dini nyingine kama Wakristo, Wahindu na Wazartoshi bali hata watu wasioamini kabisa dini wakimuenzi na kumuadhimisha Imam Hussein bin Ali ambaye alisimama mbele ya maadui siku ya Ashura katika mapambano ya Karbala na kuwaambia kwamba: "Kama hamna dini basi kuweni watu huru katika dunia yenu".

Kasisi maarufu wa Iraq, Joseph Ilyas ambaye amekuwa akishiriki katika matembezi na shughuli ya siku ya Arubaini ya Imam Hussein anasema: Makundi ya Wakristo yanashiriki katika matembezi ya Arubaini pamoja na Waislamu ili kutangaza mshikamano wao na Ahlubaiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Kasisi huyo anasisitiza kuwa Hussein bin Ali anashabiana sana katika harakati na maisha yake na Nabii Isa Masiih (as).

Dakta Saad Petros ambaye ni Mkristo wa Iraq pia anasema: Hatujafanya sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa Isa Masih (as) kwa kipindi cha miaka mitatu kutokana na kipindi cha sherehe hizo kusadifiana na mwezi wa maombolezo wa Muharram", mwisho wa kunukuu. 

Si hayo tu bali wanadamu hao wasio Waislamu wamekuwa wakiandaa misafara na makundi yanayoshiriki na kutoa huduma kwa Waislamu wanaofanya ziara na kushiriki katika matembelezi ya Arubaini huko Karbala. Katika uwanja huo tunaweza kuashiria kundi la "Isa Mwana wa Maryam" linaloshiriki kutoa huduma kwa Waislamu wanaoshiriki katika shughuli za Arubaini huko Iraq.

Miongoni mwa mambo ya kuvutia ni kujiandikisha kwa mamia ya watu wa Ulaya na Marekani kwa ajili ya kushiriki katika matembezi ya mwaka huu ya Arubaini ya Imam Hussein (as). Kwa mfano tu taasisi ya Msafara wa Arubaini wa Ulaya imetangaza kuwa, itapeleka watu 1200 huko Iraq kushiriki katika matembezi ya Arubaini. Idadi hiyo ni tofauti kabisa na ile ya watu binafsi au kupitia makundi mengine kutoka Ulaya na Marekani wanaokwenda huko Karbala.

Waumini wakitayarisha chakula kwa ajili ya watu wanaozuru Haram ya mjukuu wa Mtume (saw)

Hamu hii kubwa ya kutaka kushiriki katika shughuli ya Arubaini ya Imam Hussein inatokana na mvuto makhsusi aliopewa mtukufu huyo kutoka kwa Mwenyezi Mungu Karimu. Mamilioni hayo ya maashiki wanavutiwa na harakati ya mtukufu huyo ambaye mwaka 61 Hijria aliuawa kidhalimu katika medani ya Karbala lakini thamani na matukufu ya kibinadamu aliyopigana kwa ajili yake yanawavuta zaidi ya watu milioni 20 kandokando ya ziara na Haram yake. Mvuto na mapenzi haya ya wanadamu kwa Imam Hussein (as) yanatukumbusha sehemu ya aya ya 40 ya Suratul Hajj inayosema: Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humnusuru yule anaye mnusuru Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu. Na vilevile aya ya 69 ya Suratul Ankabut inayosema: Na wanaofanya jihadi kwa ajili yetu Sisi tutawaongoa kwenye njia zetu, na hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na watu wema.