Dec 04, 2017 12:03 UTC
  • Kipindi maalumu cha Milaad an-Nabi SAW

Hizi ni siku za kusherehekea uzawa wa Bwana Mtume Muhammad al-Mustafa (saw). Huku tukikupeni mkono wa pongezi, fanaka na heri kwa mnasaba wa kuwadia siku hizi adhimu na za furaha kubwa, tunakuombeni mujiunge nasi ili tupate kusikiliza kwa pamoja kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba huu, karibuni.

Baada ya karne kadhaa za ulimwengu kusubiri, hatimaye subira hiyo ilifikia ukingoni kwa kuzaliwa kiongozi mkubwa wa jamii ya mwanadamu. Kiumbe bora zaidi wa Mwenyezi Mungu alidhihiri, mvua ya 'Rehema kwa Walimwengu" kunyesha, chemichemi ya huruma na wongofu kububujika na nuru ya Muhammad kuangaza ulimwengu na mbingu zote.

Wataalamu wa nujumu waliapa kwamba walikuwa wameshuhudia nyota inayong'ara ambayo mwanga wake mkubwa bila shaka ungeubadilisha ulimwengu. Katika kipindi hicho Muhammad alizaliwa hali ya kuwa amezungukwa na nuru. Kwa kuzaliwa kwake, jangwa la ujahili na taasubi lilibadilika na kuwa bustani la huruma na fikra na maisha yaliyovurugika ya mwanadamu kuimarika tena. Mbeba ujumbe huyo wa Mwenyezi Mungu alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal katika mji mtukufu wa Makka katika familia yenye imani na iliyokuwa inamwogopa Mwenyezi Mungu. Uzawa wake alisambaza harufu nzuri na ya kuvutia ya uturi miongoni mwa waumini na kububujisha chemichemi za maarifa kwenye nyoyo zao na kwa njia hiyo Mwenyezi Mungu akaweza kuwanuifaisha walimwengu kwa rehema zake zisizokuwa na mwisho. Tunakutakieni heri na fanaka wasikilizaji wetu wapenzi kwa mnasaba wa siku hii adhimu ya kuzaliwa Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw).

Bibi Amina ambaye ni mama yake mpendwa Mtume Mtukufu anasema: 'Usiku huo ni kana kwamba mwanga wa utukufu wa MwenyezI Mungu ulikuwa umeniteremkia. Nuru yenye mwanga ilitoka kichwani kwangu na kupaa mbinguni. Malaika waliteremka pembeni yangu nami kuhisi utulivu wa kuvutia ndani yangu. Chumba kilijaa nuru na hapo mwanangu Muhammad akazaliwa. Uso wake ulifanana na wa baba yake, Abdallah, lakini ulikuwa ni wa kupendeza na kuvutia zaidi. Kwenye paji lake la uso kulikuwa na nuru ya mbinguni iliyong'ara kwa mvuto maalumu. Alinyoosha mkono wake mmoja kuelekea ardhini na mwingine kuelekea mbinguni na kutoa shahada ya kuthibitisha upweke wa Mwenyezi Mungu kwa maneno ya kuvutia sana. Malaika walimbeba mikononi na kunipongeza huku wakininywesha sharubati tamu. Mmoja wao alipaza sauti na kusema: Ewe Amina! Muachie Mwenyezi Mungu Mmoja mwanao na useme: Ninamkinga na Mwenyezi Mungu Mmoja kutokana na shari ya kila mwenye chuki hasidi!'

Abdul Muttalib, baba yake Abdallah alifika mbele ya Amina. Alimbeba mtoto huyo mchanga na mwenye nuru na kumpeleka Masjidul Haram ili kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuikabidhi familia yake mtoto mtukufu kama huyo. Alipokuwa akiingia ndani ya Kaaba mdomo wa mtoto huyo mchanga ulifunguka na maneno ya Bismillahi ar-Rahmanir Raheem yakasikika kwa sauti kubwa. Katika hali hiyo maneno yafuatayo yalisikika: ''Tazameni, enyi walimwengu! Haki imekuja na batili kutokomezwa, na batili daima itaendelea kutokomezwa.'

Muhammad (saw) alikuwa na umri wa miaka 12 aliposafiri na ami yake Abu Talib katika safari ya kibiashara huko Sham. Njiani, msafara huo ulifika katika kituo kimoja cha utawa na kuamua kupumzika hapo. Katika kituo hicho kulikuwa na mtawa mmoja mwenye imani kwa jina la Buhaira ambaye alikuwa akipokea na kuwahudumia wasafiri. Wakati wasafiri walipoingia humo, mtawa huyo aliuliza: 'Je, hakuna mtu mwingine aliyebaki nyuma?' Abu Talib akamjibu kwa kusema: 'Ni kijana mmoja tu aliyebaki nje.' Buhaira alitaka kijana huyo pia aletwe ndani. Wakati Muhammad (saw) alipoingia nyumbani, Buhaira alisema kwa mshangao: 'Nina swali; ninaapa kwa masanamu makubwa ya Lata na Uzza uniambie ukweli! Muhammad akajibu: 'Vitu ninavyovichukia zaidi ni masanamu mawili haya.' Kisha Buhaira akasema: 'Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu aliye Mkuu, uniamnie ukweli!' Muhammad (saw) akasema: 'Mimi daima husema ukweli." Buhaira akauliza: 'Ni kitu gani unachokipenda zaidi?' Muhammad akajibu: 'Kuwa peke yangu.' Buhaira akauliza: 'Ni mandhari gani unayoipenda zaidi?' Muhammad akajibu: 'mbingu na nyota.' Baada ya kumuuliza maswali mengine kadhaa Buhaira alitaka kuona mabega ya Muhammad ili alinganishe alama ambayo angeiona hapo na alama ile iliyozungumziwa na Nabii Isah Masih (as) kuhusiana na Mtume amabaye angekuja baada yake ambaye jina lake ni Ahmad. Baada ya kuona alama hiyo, alimuuliza Abu Talib kwa msisimko: 'Huyo ni mtoto wa nani?' Abu Talib akajibu: 'Ni mtoto wangu.' Buhaira akasema: 'Hapana!' Baba wa kijana huyu hapasi kuwa hai.' Abu Talib aliuliza kwa mshangao: 'Unayajuaje haya?' Buhaira aliyekuwa ameshakwishashangazwa na ukweli na huruma ya Muhammad alisema kwa utulivu: 'Mustakbali wa kijana huyu ni muhimu sana. Ikiwa watu wengine wataona na kuyajua niliyoyaona kwenye kijana huyu bila shaka watamuua. Mchunge sana kwa sababu yeye ni Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu.'


Muhammad daima alikuwa akitatizwa na mazingira mabaya ya jamii yake. Kila mara upeo wa fikra zake ulipokuwa ukiongezeka ndivyo pengo la kifikra baina yake na jamii yake lilivyozidi kuogezeka. jambo hilo lilimfanya atumie wakati wake mwingi kwenda mlimani kwa ajili ya kutafakari zaidi juu ya hali na uumbaji wa ulimwengu na wakati huohuo kufanya ibada na kuomba dua. Alipohitimu umri wa miaka 40 na akiwa katika pango la Hira, Mtume Mtukufu (saw) aliteremshiwa Wahyi wa kwanza ambapo Aya za: Bismillahir Rahmanir Raheem. Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba. Amemuumba binaadamu kwa tone la damu..... ziliteremshwa

Mtume alikuwa akiamini kwamba matatizo ya kijamii, baada ya kuzingatiwa maadili yanaweza kutatuliwa kwa kuzingatiwa umoja na mshikamo kwenye jamii. Kwa msingi huo aliyaunganisha makabila tofauti hasimu na kuyafanya yahurumiane na kuwa na upendo badala ya kuchukiana na kupigana vita. Kwa kueneza mafundisho aali ya Uislamu Mtume (saw) alifanikiwa pakubwa kueneza katika jamii yake umoja, udugu na ushirikiano bila ya kujali misingi ya ukabila. Katika miaka yake ya kwanza ya kuingia katika mji mtakatifu wa Madina, Mtume (saw) alifanya ubunifu muhimu wa kuunga udugu baina ya Waislamu wote wanaume kwa wanawake. Uunganishaji huo uliopinga mienendo ya kikabila ulisimama na kuzingatia tu misingi ya haki na ushirikiano wa kijamii. Kwa msingi huo Mtume Mtukufu (saw) aliwaunganisha Muhajirina na Maansar wa Madina hadi mwishowe aliposalia Imam Ali (as) ambapo aliungana naye na kumfanya kuwa ndugu yake wa dunia na Akhera.

Mitume wote wa mwenyezi Mungu wana mvuto maalumu kutokana na ukweli na uaminifu wanaoueneza. Wao ni watawala wa nyoyo wasiokuwa na wapinzani na imani yao huvutia wimbi na umati mkubwa wa wanadamu kuwaelekea. Kuhusiana na hilo, Muhammad (saw) ambaye ni Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu anasema: 'Mimi niliteuliwa kwa ajili ya kuja kukamilisha maadili mema.' Na kuhusu suala hilohilo Qur'ani Tukufu yenyewe inasifu maadili na akhlaki nzuri ya Mtume huyo wa Rehema na kukumbusha kwamba lau angelikuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka watu wangelimkimbia. Huruma na upole wake uliwashangaza wengi. Katika njia aliyokuwa akipitia Mtume (saw), Yahudi mmoja alikuwa akimuudhi kila siku kwa kumwagia jivu kichwani kutoka kwenye paa la nyumba yake. Licha ya maudhi hayo yote lakini Mtume alikuwa mtulivu na mwenye subira kubwa na aliendelea na safari yake bila kumchukulia hatua yoyote Yahudi huyo. Siku moja alipita mahala hapo na kutomwagiwa jivu wala kumwona Yahudi yule aliyekuwa akimumwagia jivu kila mara alipokuwa akipita mahala hapo. Baada ya kuona hivyo aliuliza kwa upendo: 'Je, mbona rafiki yetu hakuja leo?' Aliambiwa kuwa alikuwa ni mgonjwa. Baada ya kusika hayo alienda kumtembelea kwake nyumbani. Aliketi pembeni alikokuwa amelazwa Yahudi yule ni kana kwamba hakuwa amemfanyia udhia wowote na Yahudi huyo. Yahudi huyo alishangazwa sana na tabia hiyo nzuri na ya kuvutia ya Mtume Mtukufu (saw).

Katika kipindi cha kukombolewa Makka ambapo Mtume na jeshi lake walikuwa katika kilele cha nguvu na uwezo mkuwa wa kijeshi, mmoja wa wabeba bendera wake alisikika akisoma shairi ambalo lilisema: 'Leo ni siku ya vita! Leo roho na mali zenu zitachukuliwa kuwa halali, leo ni siku ya kudhalilishwa Quraish.' Baada ya kusikia maneno hayo, Mtume (saw) alikasirishwa sana na ili kutoruhusu watu wa Makka wakate tamaa na ahadi zake za msamaha kwa wote kutotumiwa vibaya kumaanisha njama na hila, alijibu matamshi hayo mara moja kwa kusema: 'Leo ni siku ya rehema, leo ni siku ya utukufu kwa Qureish, leo ni siku ambayo Mwenyezi Mungu ameitukuza Kaaba.'

Tunaweza kusema kuwa maelekezo na mipango ya Mtume Muhammad (saw) ndiyo inayohitajika sana na mwanadamu wa elo kwa ajili ya kujikwamua kutoka kwenye mtego wa fitina, machafuko na ufisadi anaokabiliwa nao kwa sasa. Kwa kutilia maanani hilo, tunaweza kusema bila kusita kwamba mwanadamu wa leo ambaye ana matumaini makubwa ya kufikia amani na kuishi kwenye mazingira ya utulivu anaweza tu kifikia lengo hilo na mustakabali unaong'ara kwa kutekeleza na kufuata kikamilifu mafundisho halisi ya mjumbe huyo wa Mwenyezi Mungu.

Tukiwa tanakaribia mwisho wa kipindi hiki wasikilizaji wapenzi, tunakupongezeni tena kwa mnasaba huu adhimu wa kukumbuka kuzaliwa Mtume wetu Mpendwa, Muhammad al-Mustafa (saw). Hadi tutakapokutana tena wakati mwingine panapo majaaliwa, tunakuageni nyote wapendwa wasikilizaji kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags