Sep 11, 2018 07:42 UTC
  • Maswali Kuhusu Tukio la Ashura (1)

Katika kipindi hiki cha Maswali Kuhusu Tukio la Ashura, tunakusudia kujibu baadhi ya maswali ambayo huenda yakawa yanaulizwa na baadhi ya watu kuhusiana na tukio hili.

Moja ya maswali hayo ni kuwa, je, kwa mtazamo wa historia, tukio la Ashura lililotokea mwaka 61 Hijiria, lilijiri kama tunavyolielewa hivi sasa au la? Hili ndilo swali tutakalojaribu kulijibu katika kipindi hiki cha leo, karibuni.

*******

Tukio la Ashura ni tukio la kushangaza sana. Hili ni tukio ambalo ndani yake walijitokeza mashujaa wachache kupambana na makumi ya maelfu ya askari katili na wasio na huruma wa Yazid mwana wa Muawiyya, na wakaamua kusimama imara hadi kuuawa mtu wa mwisho kwa ajili ya kutetea imani yao sahihi ya  Mwenyezi Mungu na pia kutoishi maisha ya udhalili. Mapambano hayo ya kishujaa yaliyoonyeshwa na familia ya Mtume pamoja na wafuasi wao waaminifu na kwa madhumuni ya kufanya marekebisho katika umma wa Mtume Mtukufu (saw), yamewashangaza wengi duniani, tokea yalipotekelezwa hadi hadi.

Baada ya kumuua kinyama mjukuu wa Mtume, Imam Hussein (as) na wafuasi wake waaaminifu, Bani Ummaiyya walitangaza sherehe na idi kubwa ili kuondoa katika fikra za watu tukio hilo chungu la kumuua mjukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na kujaribu kufunika kashfa hiyo ya maadui wa Ahlul Beit, yaani familia au Watu wa Nyumba ya Mtume (saw), lakini hawakufanikiwa kufikia lengo hilo. Katika kipindi chote cha historia, tukio la Ashura limegeuka na kuwa njia ya maisha na utamaduni ambapo kupambana dhidi ya dhulma na ufisadi pamoja na kujitoa muhanga katika njia hiyo ni nguzo kuu mbili muhimu ya utamadunia huo. Utamaduni kama huo katika zama zote za historia umekuwa ukichukuliwa na madhalimu na mabeberu kuwa hatari kubwa ambapo wamekuwa wakifanya kila juhudi ili kuupinga na kujaribu kuutukomeza. Hii leo pia watu walio na fikra hiyo potovu kuhusiana na utamaduni wa Ashura, katika mrengo wa kifikra wa Yazid na Muawiyya wanatumia kila njia na mbinu ili kudhoofisha na kuondoa kabisa utamaduni huo muhimu wa kihistoria katika fikra za Waislamu. Kuzua shaka na wasiwasi miongoni mwa Waislamu kuhusiana na ukweli wa tukio hilo la kihistoria ni moja ya mbinu hizo ambazo hata hivyo hazikuanza kutekelezwa leo.

Kuhusiana na tukio hili la kihistoria, swali la kwanza linaloulizwa ni kuhusiana na ukweli wa kinyaraka na mapokezi kuhusiana na tukio zima la Ashura. Wanauliza kuwa, je, tukio la Karbala lilijiri kama tunavyojua leo au la? Wataalamu na wajuzi wa historia wanaamini kwamba hakuna tukio jingine katika historia ya Uislamu ambalo limeandikwa na kunukuliwa kwa usahihi kama lilivyo tukio la Karbala. Vitabu vya historia ya Kiislamu viwe ni vya Mashia au Masuni au hata vya wanahistoria wasiokuwa Waislamu, vimeelezea tukio la Ashura kwa umakini mkubwa wa kimapokezi kwa kadiri kwamba misingi muhimu ya kihistoria kuhusiana na tiukio hilo imelindwa, ila tu kwamba kuna tofauti ndogondogo ambazo zimeripotiwa, sawa kabisa na kama ilivyo hali kuhusiana na tukio jingine lolote la kihistoria. Kwa mujibu wa wanahistoria asilimia 90 ya mambo yaliyonukuliwa kuhusiana na tukio la Karbala ni sahihi.


Sehemu kubwa ya habari na maelezo yaliyotufikia kuhusiana na tukio la Karbala yanatoka kwa Ahlul Beit wa Mtume (saw) na Maimamu Maasumu (as). Si wote waliokuwa pamoja na Imam Hussein (as) Karbala mwezi wa Muharram 61 Hijiria waliuawa shahidi bali kuna wale waliobaki hai kutokana na sababu moja au nyingine miongoni mwao wakiwemo Imam Sajjad (as) ambaye katika kipindi hicho alikuwa mgonjwa sana, Bibi Zeinab (as) Binti ya Imam Ali (as), Imam Muhammad Baqir (as) ambaye katika kipindi hicho alikuwa mdogo sana kiumri na watu kadhaa katika familia ya Imam Hussein (as) ambapo wote walikuwa mashuhuda wa tulio hilo chungu la Karbalaa. Mashuhuda hao walikuwa wakinakili na kuwahadithia watu mara kwa mara machungu ya siku hiyo kwa miaka mingi iliyofuata. Vilevile kuna hadithi nyingi  mno ambazo zimenukuliwa kutoka kwa Maimamu Ja'ffar as-Swadiq na Ali bin Musa ar-Ridha (as) kuhusiana na jinsi tukio hilo la kuhuzunisha lilivyojiri. Kwa kutilia maanani kwamba kwa mujibu wa imani ya Mashia, Maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtume (saw) ni maasumu, yaani waliokingwa kufanya dhambi, hivyo mapokezi yao ni uthibitisho na hoja tosha kwetu.  Baadhi ya wafuasi wa Imam Hussein (as) kama vile mtumishi wa Hadhrat Rubaab (as) ambao walijeruhiwa kwenye vita, walibaki hai na kusimulia mambo yaliyojiri kwenye vita hivyo.

Sehemu nyingine ya habari za kihistoria kuhusiana na tukio la Karbala ilisimuliwa na maadui wa Imam Hussein (as). Katika zama hizo kulikuwepo na watu maalumu ambao walikalifishwa kuandika kuhusu matukio yaliyojiri wakati wa vita na kwa hakika wao ndio waliokuwa waandishi rasmi wa matukio ya vita. Humaid bin Muslim alikuwa mmoja wa waandishi hao ambaye alikalifishwa na jeshi la Omar Sa'd kuandika matukio hayo, ambapo aliandika mambo mengi kuhusiana na vita hivyo. Mbali na hayo kulikuwa na watu wengine ambao walikuwa wakimsimuliaYazid bin Muawiya yale yote yaliyojiri katika medani ya vita Karbala ili kujipendekeza na kumfurahisha mtawala huyo dhalimu, ambapo visa vyao vyote vimenukuliwa na kurekodiwa katika vitabu vya historia. Licha ya kuwa matukio ya Ashura yanapatikana katika vyanzo vingine ambavyo viliandikwa na watu ambao baadhi yao walikuwa na itikadi inayogongana lakini bado vina mambo mengi ya pamoja na yanayofanana kuhusu matukio hayo.

 

Kwa mtazamo wa wanahistoria, nyaraka za kihistoria za tukio hilo ni za kuaminika kiasi kwamba hakuna mwanahistoria yeyote awe ni Mwislamu au asiyekuwa Mwislamu ambaye ametilia shaka misigi na nguzo muhimu za tukio hilo. Hata watu wanaodai kwamba Imam Hussein (as) hakuwa upande wa haki, wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo chungu na la kuhuzunisha ambapo hata baadhi yao wamelaani wale wote waliohusika na mauaji hayo ya kinyama dhidi ya mjukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Kuhusiana na suala hilo Shahab ad-Deen Mahmoud bin Abdallah al-Aalusi, mwmanahistoria na msomi mashuhuri wa Ahlu Sunna ambaye aliaga dunia mwaka 1270 Hijiria na ambaye hakuwa na mtazamo mzuri kuhusu Mashia, naye pia baada ya kunukuu mambo fulani kuhusiana na tukio la Ashura anasema: ''Ni wazi kwamba Yazid hakutubu nao Ibn Ziad na Ibn Sa'd wanafungamana naye, na madamu kuna jicho ambalo linaendelea kumlilia Imam Hussein, Mwenyezi Mungu ataendelea kumlaani Yazidi na wafuasi wake.''

Kwa hakika ukubwa wa tukio hilo na athari zake katika historia ya Uislamu, Ushia na hata historia nzima ya nzima ya mwanadamu kwa ujumla, ni kubwa kwa kadiri kwamba wanahistoria kutoka madhehebu yote na bila kujali mielekeo yao, wamenukuu na kulichambua kwa kina tukio hilo ambapo hata wapinzani wameshindwa kuficha ukubwa na taathira zake.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tumefikia mwisho wa sehemu hii ya kwanza ya makala hii. Ishini salama.

Tags