Maswali Kuhusu Tukio la Ashura (11)
Imam Hussein bin Ali (as) na wafuasi wake 72 waliuawa shahidi katika tukio la Ashuraa mwaka 61 Hijria na watu wa familia ya Mtume wakachukuliwa mateka na jeshi katili la Yazid bin Muawiya alasiri ya siku hiyo.
Yumkini hapa kukajitokeza swali kwamba, inawezekana vipi kustahamili mashaka na masaibu hayo yote na hatimaye kuuliwa shahidi kwa njia ya kutisha kukatambuliwa kuwa ni ushindi?
Mshindi katika medani ya vita, kama ilivyo katika medani nyingine za maisha ya mwanadamu, huwa yule aliyefanikiwa kufikia malengo yake na kwa msingi huo kushindwa huwa na maana ya kutofikia malengo. Sasa inatupasa tutazame, pande hizi mbili za vita hivyo vya kihistoria zilikuwa na malengo gani? Na ni upande upi uliofanikiwa kufikia malengo yake? Je, lengo la Imam Hussein (as) na watu wa familia ya Mtume Muhammad (saw) lilikuwa kuokoa maisha yao na kuepuka kifo, na kwa msingi huo kuuawa kwao shahidi kutambuliwe kuwa ni kushindwa katika vita?
Kama bado mnakumbuka tulisema katika mfululizo wa makala hizi kwamba, Bwana wa Vijana wa Peponi, Imam Hussein (as) alikuwa akiwajua vyema maadui wake na kwamba alikuwa na habari kuhusu jinsi atakavyouliwa shahidi katika ardhi ya Karbala kama alivyoambiwa na baba na babu yake. Vilevile alijua kwamba, ahli yake na familia hiyo ya Mtume (saw) itachukuliwa mateka. Pamoja na hayo alisimama na kufanya mapambano kwa ajili ya kutekeleza wajibu wake wa kukabiliana na upotovu uliokuwa umefanywa katika dini ya babu yake. Lengo la Imam lilikuwa kuurejesha Umma katika njia yake ya asili na sahihi na kupaza sauti ya kudhulumiwa Uislamu katika zama na vipindi vyote.
Muawiya bin Abi Sufiyan alitawala dola la Kiislamu kwa kipindi cha miaka 20 kwa kukanyaga sheria za dini ya Mwenyezi Mungu lakini kwa ujanja na ulaghai, akafanya dhulma kubwa kwa Uislamu kwa kutumia vifuniko na visingizio vya aina mbalimbali. Mafundisho asili ya Uislamu yaligeuzwa na kupotoshwa na hakikubakia chochote katika Uislamu isipokuwa jina lake tu. Alieneza uzushi na bidaa katika dini badala ya Suna za Mtume (saw) na mafundisho yake. Hali ya Umma wa Kiislamu ilikuwa mbaya kwa kadiri kwamba, baada ya mtawala huyo dhalimu na muovu kuaga dunia, mwanaye Yazid mnywa pombe na mlevi alishika madaraka ya kuongoza Umma na akawataka Waislamu wamtambue kama Khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Yazid huyu aliyeshika usukani wa kuongoza Waislamu alimkana Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiyama waziwazi na kadamnasi. Alikuwa akikanyaga sheria za Uislamu mchana kweupe. Hali hii ilienea katika safu za maafisa wa utawala wake ambao walifanya jinai, dhulma na uovu mkubwa na kukengeuka mafundisho ya Uislamu. Wakati huo Umma wa Kiislamu ulikuwa katika usingizi na mghafala mkubwa. Uislamu ulikaribia kuangamia na kutoweka kutokana na jinsi mafundisho yake yalivyobadilishwa. Usingizi na mghafala huo ulienea hata baina ya watu mashuhuri, na wale waliokuwa macho na wenye mwamko hawakuwa na ujasiri wa kusimama kidete na kupaza zauti zao dhidi ya dhulma na uovu wa utawala wa Yazid bin Muawiya. Naam, dini ya Uislamu katika mazingira haya ilikuwa katika ncha ya kuangamia na kutoweka kutokana na jinsi ilivyokuwa imepotoshwa.
Hapa ndipo Imam Hussein (as) aliposimama na kupaza sauti. Alikuwa Imam na mshika bendera ya babu yake, Mtume Muhammad (saw) na kwa msingi huo aliwajibika kubainisha haki na kuwafichua wanafiki na madhalimu sambamba na kuwazindua Waislamu. Kwa sababu hiyo alisema katika barua yake aliyowatumia vinara wa mji wa Kufa nchini Iraq kwamba: “Ninawalingania Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Suna za Mtume (saw), kwani Suna za Mtume zimetoweka na bidaa na uzushi vimehuishwa. Kama mtanisikiliza na kufuata amri yangu nitakuongozeni katika njia sahihi.”
Bwana wa Vijana wa Peponi na taa ya uongofu ya Umma wa Muhammad, Hussein bin Ali (as) aliuawa kikatili sana katika siku ya Ashuraa. Hata hivyo sherehe ya ushindi wa kidhahiri wa Yazid bin Muawiya iliishia katika fedheha na kashfa kubwa. Kwani hotuba zilizotolewa na Bibi Zainab bin Ali na Imam Sajjad (as) siku chache tu baada ya msafara wa mateka wa Karbala kuwasili Sham kwa mtawala wa Banii Umayyah, zilimfedhehesha mtawala huyo na kutikisa nguzo za utawala wake. Hotuba hizo zilimfanya Yazid atambue kuwa, ameshindwa katika njama zake za kutaka kuzima nuru ya Uislamu na kumlazimisha aseme walau kidhahiri na kimaonyesho tu kwamba: Mwenyezi Mungu amlaani Ibn Ziyad aliyefanya ukatili huo mkubwa! Hotuba za mateka wa Karbala ziliwaamsha watu wa Sham waliokuwa katika usingizi mkubwa na kumtia woga na hofu Yazid na wasaidizi wake.
Miongoni mwa uzushi na upotovu uliokuwa umeenezwa wakati wa utawala wa Muawiya na mwanaye, Yazid ni itikadi potofu na iliyokuwa dhidi ya dini inayosema kwamba, amri ya Khalifa na mtawala ni muhimu na iko juu hata ya amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Wakati utawala wa Banii Umayyah uliposhambulia mji mtakatifu wa Makka na kuchoma moto Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba, watawala walijibu lawama za wapinzani wao wakisema: Kumtii Khalifa kumekabiliana na utukufu wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu lakini kumtii Khalifa kumeshinda utukufu wa Nyumba na Allah na kunatangulizwa mbele.” Kwa mtazamo wa watawala hao hakuna kitu kilichokuwa na utukufu sawa na ule wa Khalifa na mtawala, na kwamba hukumu na maamuzi ya Khalifa ndiyo Uislamu na dini yote, ndiyo maamuzi ya Mwenyezi Mungu na ndiyo radhi zake; hivyo inapaswa kutangulizwa mbele ya kila kitu. Walisema: "Hukumu ya Khalifa inafuta na kusamehe madhambi yote na kumpa mwanadamu hatima nzuri."
Kwa msingi wa itikadi kama hizi, kumuua mjukuu wa Mtume (saw), kuchoma moto al Kaaba na kubaka na kunajisi wanawake wa mji mtukufu wa Madina wakiwemo wake na mabinti wa masahaba wa Mtume (saw) ni njia inayomwelekeza na kumfikisha mtu peponi. Hata hivyo mapambano ya Imam Hussein (as) na masahaba zake yalibatilisha fikra hizo potofu na kung’oa mizizi yake.
Imam Hussein (as) alifanikisha malengo yake ya muda mfupi yaani kung’oa utawala wa Yazid, na yale ya muda mrefu na ya kihistoria. Lengo la kizazi cha Abu Sufiyan lilikuwa kuangamiza Uislamu na kufuta jina la Mtume Muhammad (saw) na mafundisho ya Qur’ani. Lakini kuuliwa shahidi Imam Hussein lilikuwa tukio kubwa na la aina yake katika historia ya Uislamu. Kwa sababu utawala wa kizazi cha Abu Sufiyan ambao Muawiya alitumia miaka ishini ya utawala wake kuimarisha nguzo na misingi yake, uliporomoka na kung’olewa madarakani katika kipindi cha chini ya miaka minne baada ya mapambano ya siku ya Ashuraa. Yazid kamwe hakufaidi ushindi wa kidhahiri wa kuwaua kinyama watu wa familia ya Mtume (saw) huko Karbala na wala hakuweza kuzima nuru ya Mwenyezi Mungu iliyomulika ulimwenguni kutoka katika nyumba hiyo tukufu. Badala yake, hii leo na baada ya kupita karne nyingi tangu baada ya mauaji ya siku ya Ashuraa yaani tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria, bendera ya Uislamu inapepea juu zaidi, na jina na Hussein, njia yake, malengo yake na ujumbe wake vinawavutia wafuasi wengi siku baada ya siku.
Mapambano ya Imam Hussein (as) ni somo na darsa kubwa kwa wapigania uhuru na haki kote duniani. Hussein ametufundisha kusimama kidete na kupambana na adui wa haki na kweli hata kama atakuwa amejizatiti kwa silaha za kisasa na kwamba, kusalimu amri na kurudi nyuma mbele ya adui kama huyo ni mwanzo wa mashaka, fedheha na mwisho mbaya hapa duniani na huko Akhera. Ashuraa imetufundisha kwamba, hatimaye haki itashinda batili na kwamba hakuna linaloweza kuzima nuru ya Allah kama inavyosisitiza aya ya 8 ya Suratu Saff inayosema: Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao, na Mwenyezi Mungu atakamilisha nuru yake ijapokuwa makafiri watachukia.