Miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran
(last modified Tue, 12 Feb 2019 10:06:54 GMT )
Feb 12, 2019 10:06 UTC
  • Miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran

Assalam Alaykum warhmatullahi wabarakatuh hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nasi tena katika kipindi hiki maaluimu kinachokujieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 40 wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Endeleeni kuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Sherehe za kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka huu zinafanyika kwa shamrashamra kubwa zaidi kuliko miaka iliyopita na sasa wananchi Waislamu wa Iran wanasherehekea kutimia miaka 40 tangu mapinduzi hayo yalipopata ushindi mwaka 1979.

Sherehe za kutimia miaka 40 ya umri wa Mapindizi ya Kiislamu hapa nchini mwaka huu zina sifa makhsusi na muhimu. Miongoni mwa sifa hizo ni kwamba, sherehe hizo ni jibu mwakafa kwa njama zinazoendelea kufanywa na maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu wakiongozwa na Marekani na utawala bandia wa Israel. Hii ni kutokana na kwamba, baadhi ya maafisa mashuhuri na wa ngazi za juu wa serikali ya Marekani walikuwa wametangaza kuwa, katika mwaka wa 40 wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Jamhuri ya Kiislamu itakumbwa na changamoto kubwa na hata kuondolewa madarakani. Tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini Marekani daima imekuwa ikifanya njama za kutaka kuiangusha Jamhuri ya Kiislamu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, utawala wa kifalme wa Shah Muhammad Reza Pahlavi ulikuwa tegemezi sana kwa Marekani, na Iran ya wakati huo ilikuwa kituo kikuu cha kutekelezea manifesto na ilani serikali ya Washington katika eneo la Mashariki ya Kati. Rais wa zamani wa Marekani, Richard Nixon ambaye ndiye aliyebuni ilani hiyo aliitambua Iran kuwa ni wenzo na fimbo ya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati. Kwa mujibu wa stratijia ya Washington kuhusu eneo hilo, Marekani ilimpatia Shah Reza Pahlavi silaha na sana za kisasa kabisa. Zaidi ya washauri elfu 40 wa Marekani walikuwa nchini Iran na kivitendo ndio waliokuwa wakiendesha masuala ya nchi, na Shah Pahlavi alikuwa kibara na mwanaserere. Balozi wa Marekani nchini Iran ndiye mtu aliyekuwa karibu zaidi kwa mfalme wa Iran, Reza Pahlavi,  na Shah alishauriana naye kabla ya kuchua uamuzi wa jambo lolote muhimu.

Hivyo ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini ulikuwa pigo na dhoruba kubwa kwa siasa za kibeberu za Marekani. Kwa sababu hiyo tangu baada tu ya ushindi wa mapinduzi hayo, serikali ya Marekani ilifanya kila iwezalo kwa ajili ya kuuondoa madarakani utawala wa Kiislamu hapa nchini. Katika kipindi chote cha miaka 40 ya umri wa Mapinduzi ya Kiislamu Marekani imekuwa ikishirikiana na kuyapa himaya na misaada makundi yote yanayopiga vita Jamhuri ya Kiislamu au yaliyotaka kujitenga. Marekani ilifanya jitihada kubwa kuipindua Jamhuri ya Kiislamu kwa kutumia njia ya vikwazo vya kiuchumi, mauaji ya viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu, kuyafadhili makundi yaliyotaka kujitenga na kuwaunga mkono na kuwasaidia wapinzani waliotimuliwa na wananchi na hatimaye kuusaidia utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein kuanzisha vita dhidi ya Jamhuri changa ya Kiislamu na kuvamia ardhi ya Iran.

Uhasama ya uadui huo wa Marekani na waitifaki wake vilipelekea kuimarika zaidi misingi na nguzo za Jamhuri ya Kiislamu na kuungwa mkono zaidi viongozi wake ndani ya nje ya nchi. Kwa mfano utaona kuwa wakati mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini alipofariki dunia jeneza lake lilisindikizwa na karibu watu milioni 10. Idadi hiyo ya watu ilikuwa mara mbili zaidi ya ile ya watu waliokwenda kumlaki Imam Khomeini wakati aliporejea nchini baada ya kulazimishwa kuishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15 mwezi Februari mwaka 1979. Vivyo hivyo kiongozi wa sasa wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ambaye anahesabiwa kuwa mtu anayependwa zaidi baina ya wananchi wa Iran. 

Imam Ruhullah Khomeini

Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita ya uhai wa Jamhuri ya Kiislamu kumefanyika chaguzi 36 zilizoshirikisha idadi kubwa ya wananchi na kila uchaguzi ulikuwa na vuguvugu kubwa kuliko wa kabla yake.

Licha ya kushindwa njama zote za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu lakini Washington na waitifaki wake wangali wanafanya kila wawezalo kutoa dhoruba na pigo kwa Mapinduzi ya Kiislamu hasa kupitia njia ya kueneza propaganda chafu na kuchafua sura ya Iran ya baada ya Mapinduzi. Misukosuko na changamoto zote hizo zimeikomaza Iran na kuifanya kuwa miongoni mwa nchi zenye taathira kubwa zaidi katika usalama wa Mashariki ya Kati ya siasa za dunia.

Katika kipindi cha miaka 8 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa miongoni mwa nchi zilizokuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugaidi na makundi ya kigaidi hususan Daesh linalofadhiliwa na kusaidiwa na Marekani, Saudi Arabia na washirika wao. Serikali ya Washington inadhani kuwa, inaweza kuuondoa madarakani utawala wa Kiislamu hapa nchini kupitia njia ya kuwachochea wananchi na kutumia makundi ya kigaidi. Hata hivyo mahudhurio ya wananchi wa Iran katika medani mbalimbali na kuwa macho kwao vimekuwa vikizima njama hizo na hapana shaka kuwa, mahudhurio makubwa ya Wairani katika maandamano ya mwaka huu ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yatatoa pigo jingine kwa maadui hao. 

Donalr Trump

Baada ya kushika hatamu za uongozi wa Marekani, serikali ya Donald Trump ilizidisha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuzitisha nchi na mashirika yaliyokuwa yakifanya biashara na Iran kwamba, yataadhibiwa na kuwekewa vikwazo iwapo yataendeleza ushirikiano huo. Hata hivyo hatua hizo za Trump zimekabiliwa na upinzani wa nchi za Ulaya wanachama katika kundi la 5+1 zilizotia saini makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na Iran. Trump na serikali yake imeendeleza mashinikizo ya aina mbalimbali dhidi ya Iran kiasi kwamba Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, John Bolton mwaka jana alithubutu kusema kwamba, matokeo ya siasa kali za serikali ya Washington dhidi ya Iran ni kwamba Jamhuri ya Kiislamu haitauona mwaka wa 40 wa kuzaliwa kwake! Wamarekani wanadhani kuwa, vikwazo vya kiuchumi, vita vya kinafsi na mashinikizo ya kisiasa yanaweza kuwafanya wananchi wa Iran wasimame kukabiliana na serikali ya nchi yao kutokana na matatizo ya kiuchumi. Mradi huo wa kuwachochea Wairani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu waliupachika jina la "Msimu wa Joto Kali wa Iran".

Kuhusu njama hiyo khabithi ya Marekani, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei anasema: "Lengo la Marekani na maadui wengine wa Iran lilikuwa kuzusha mgawanyiko, hitilafu na vita baina ya makundi mbalimbali hapa nchini kupitia njia ya vikwazo na hujuma dhidi ya usalama wa taifa na kwa njia hiyo wawachochee wananchi kumiminika mitaani dhidi ya serikali. Mpango huo waliupa jina la "Msimu wa Joto Kali wa Iran", lakini njama hiyo ya maadui imefeli na msimu wa joto hapa nchini mwaka jana ulikuwa miongoni mwa misimu bora zaidi ya majira ya joto."

Vilevile Rais Hassan Rouhani wa Iran alijibu njama hiyo ya Marekani na hatua ya Trump ya kuiondoa nchi yake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuwaambia viongozi wa serikali ya Washington kwamba jibu la harakati zao za kishetani litaonekana katika sherehe kubwa za maadhimisho ya mwaka wa 40 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mitaa ya miji mbalimbali hapa nchini hapo tarehe 12 Februari.

Naam, Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran hii leo yanatimiza miaka 40 na yanaendelea kusonga mbele katika njia ya kukamilisha malengo yake kutokana na kusimama kidete kwa wananchi na mapambano yao dhidi ya mabeberu na wakoloni mamboleo na yataendelea kupiga hatua za maendeleo na kuwa tochi na kigezo bora cha wapenda haki na uadilifu kote duniani licha ya vinyongo na uadui wa makafiri. Tunakamilisha kipindi hiki kwa aya ya 32 ya Suratu Tauba inayosema:

یُرِیدُونَ أَن یُطْفِئُوا نُورَ اللَّهِ بِأَفْوَاهِهِمْ وَیَأْبَى اللَّهُ إِلَّا أَن یُتِمَّ نُورَهُ وَلَوْ کَرِهَ الْکَافِرُونَ

Wanataka kuizima Nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao, na Mwenyezi Mungu anakataa ila aitimize Nuru yake, ijapo kuwa makafiri watachukia.