Oct 20, 2019 07:33 UTC
  • Historia ya Matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein AS

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji wa Radio Tehran, Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote pale mlipo hususan huko nyumbani Afrika Mashariki.

 

Karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa masiku haya ya Matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein as. Makala yetu hii itazungumzia historia ya Matembezi ya Arubaini. Kuweni nami hadi mwisho.

Katika masiku haya kila mahala kunasikika harufu nzuri ya ziara na udongo wa Karbala, sauti ya Labayka ya Hussein imetawala kila mahala huku maashiki na vipenzi wa Imam Hussein wakiwa njiani wakikaza mwendo kuelekea katika ardhi ya Karbala ilipo Haram ya Bwana wa Mashahidi na kiongozi wa mabarobaro wa peponi Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib as. Hii leo maneno ya Bibi Zaynab al-Kubra binti Ali dada yake Imam Hussein as yanadhihirika na kuonekana uhakika wake zaidi kuliko kipindi na zama zozote zile. Maneno ambayo yaliyasema kwa ushujaa akiwa ndani ya mavazi ya mateka alipomwambia mtawala muovu na fasiki Yazid bin Muawiyah:

 یا یزید فَکِد کَیْدک وَاسْعَ سَعْیک و ناصِبْ جُهْدَک فوالله لا تمحُو ذکرنا و لا تُمیتُ وَحْیَنا

Ewe Yazid! Kwa hiyo panga  upangavyo (hila) kadiri uwezavyo na utekeleze njama zako na zidisha juhudi zako, lakini Wallahi, kamwe hutaweza kufuta utajo wetu na wala hutaweza kuua Wahyi (ulioteremshwa kwetu).

Kwa hakika siku ya Ashura mwaka 61 Hijria Mayazidi (Yazid na wafuasi wake) walikuwa wakitaka kuizika kabisa hamasa ya Imam Hussein na wafuasi wake palepale katika ardhi ya Karbala na hivyo isibakie athari yoyote kwa ajili ya vizazi vijavyo na hivyo kuufanya utajo na jina la familia ya Wahyi visahaulike kabisa. Hata hivyo walighafilika kwamba, jina la Imam Hussein pamoja na harakati yake iliyokabiliwa na umwagaji damu mkubwa itabakia kuwa hai milele na daima na kuwa kama Maktaba yenye kutoa ilhamu. Kwa hakika taa na nujru ing'arayo ya Allah katu si yenye kuzimika. Hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu aliyoitoa katika Aya ya 32 ya Surat al-Tawba aliposema:

یُریدُون أنْ یُطْفِؤُا نورَ اللهِ بِأفْواهِهِمْ وَ یَأْبیَ اللهُ إلاّ أنْ یُتِمَّ نورَهُ وَلَوْ کَرِهَ الکافِروُن

Wanataka kuizima Nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao, na Mwenyezi Mungu anakataa ila aitimize Nuru yake ijapo kuwa makafiri watachukia.

Matembezi ya mamilioni ya watu kwa ajili ya kwenda kulizuru kaburi tukufu la Imam Hussein as wakati huu wa kukaribia Arubaini, ni ishara ya wazi za kubakia hai utajo wa Imam Hussein as pamoja na risala na ujumbe wa Ashura. Matembezi hayo licha ya vita vyote, vitisho na vikwazo mbalimbali, lakini hii yamebadilika na kuwa matembezi makubwa zaidi ya kidini ulimwenguni. Matembezi katika siku ya Arubaini yalienea katika zama za Imam Ali bin Hussein al-Sajjad as. Jabir bin Abdillah al-Ansari sahaba mtukufu wa Mtume akiwa mfanyaziara wa kwanza mwaka 61 Hijria alianza kutembea kutoka Madina na kufanikiwa kufika Karbala asubuhi ya Arubaini ya kwanza tangu kuuawa Shahidi Imam Hussein as na wafuasi wake watiifu katika ardhi ya Karbala. Siku hiyo hiyo pia, Bibi Zaynab al-Kubra as na Imam Sajjad wakiwa pamoja na kafila na misafara mingine waliwasili Karbala ambapo baada ya kufanya mazungumzo na Jbir bin Abdillah al-Ansari, wakalizuru kaburi la Imam Hussein na hivi ndivyo ziara ya Arubaini ya Imam Hussein ilivyoanza.

Kwa hakika kufanyika ziara ya Arubaini kulikuwa kukikumbusha tukio la Karbala na kuwafedhehesha Bani Umayyah. Ni kutokana na ukweli huo ndio maana Makhalifa na watawala wa Bani Umayyah wakakata shauri la kuwazuia watu wasienda kufanya ziara Karbala na kuwawekea vizingiti mbalimbali. Wakiwa na nia ya kufikia lengo lao hilo na kukabiliana na mazuwwar (wafanyaziara) waliweka vituo vya usalama kando kando ya Karbala. Walinzi wa vituo hivyo walikuwa watu makatili na wenye roho mbaya ambapo walikuwa wakiamiliana vibaya mno na mazuwwar. Hali hiyo iliwafanya baadhi yao kuamua kuyachagua maeneo ya Ghadhiriyah na Nainawa kama ndio vituo vyao vya mwisho. Lakini baada ya kusimama kwa muda na unapowadia wakati wa usiku, huitumia fursa ya giza totoro kuelekea kwa siri upande wa kaburi la Imam Hussein. Wafanyaziara hao wakawa wakitembea wakati wa usiku kwa siri na kwa hofu kubwa mmoja mmoja na wakati mwingine katika vikundi vidogo vidogo kuelekea Karbala.

Baada ya Bani Umayyah, walipoingia madarakani pia Bani Abbas vikwazo hivyo vilikuweko. Baada ya Bani Abbas kuimarisha nguzo za utawala wao walibomoa kaburi la Imam Hussein na kuamiliana vibaya na wafanyaziara wa kaburi lake hilo. Katika kipindi hicho, hali ikawa ngumu mno na watu wakawa wakienda kufanya ziara Karbala kwa taabu na mashaka makubwa  mno wakihofia usalama wa roho zao au kukumbwa na mateso na adhabu kali pindi wanapokamatwa na makachero wa utawala wa Bani Abbas. Kwa maneno mengine ni kuwa, kwa mujibu wa watawala wa wakati huo, kwenda kuufanya ziara katika kaburi la Imam Hussein lilikuwa kosa na uhalifu mkubwa.

Katika zama za utawala wa Mutawakkil Abbas, kuamiliana vibaya na wafanyaziara, kubomoa na kulivunjia heshima kaburi la Imam Hussein as kulishika kasi na kufikia kileleni. Mtawala huyo alikuwa muovu na katili kiasi cha kufikia kutoa sharti la kukatwa mkono wa kulia kakma idhini ya kuzuru kaburi la Imam Hussein as. La kushangaza ni kwamba, hata kutolewa sharti hilo hakukupunguza hamu na shauku ya maashiki ya kwenda kuzuru kaburi tukufu la Imam Hussein as. Kwani watu wengi walikuwa wakijitokeza na kukubali kukatwa mikono yao ya kulia ili wapate idhini ya kwenda kuzuru kaburi la Imam Hussein as. Ibn Mas'ud mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu ameandika katika kitabu chake mashuhuri cha Muruj al-Dhahab kwamba:

Mwanamke mmoja alikwenda kujiandikisha kwa ajili ya kwenda kuzuru kaburi la Imam Hussein na kutoa mkono wake wa kushoto ili ukatwe. Hata hivyo maafisa wa Mutawakkil walimwambia mama huyo kwamba, anapaswa kutoa mkono wake wa kulia na sio wa kushoto ili ukatwe na hivyo apate idhini ya kwenda kuzuru kaburi la Hussein as. Mwanamke yule aliwaonyesha maaskari wale mkono wake wa kulia ambao ulikuwa umekatwa tayari na kusema: Mliukata mkono wangu huu wa kulia mwaka jana nilipotaka kwenda kulizuri kaburi la Imam Hussein.

Matembezi ya Arubaini yay Imam Hussein as mwaka 1916

 

Baada ya kupita karne kadhaa tangu kuanguka utawala wa Bani Abbas, yaani mwanzoni mwa karne ya 16, kundi potofu la Mawahabi liliuvamia na kuushambulia mji wa Karbala. Wakazi wa mji huo ambao walikuwa wameshtushwa waliwahi kufunga milango; lakini waovu hao walivunja mlango wa kuingia katika mji huo na kumiminika katika mji huo. Mawahabi hao wakaanza kuharibu na kubomoa haram mbili za Imam Hussein na Abul-Fadh al-Abbas na kuwaua karibu watu 50 jirani la dharih (kaburi) na watu wengine 500 wakauawa na Mawahabi hao ndani ya haram. Baadhi wanasema kuwa, idadi ya waliouawa katika tukio hilo la kinyama ilikaribia 1000. Baada ya hapo Iraq ikadhibiti na chama cha Baath.

Tangu awali chama hicho kilianza kutekeleza siasa za ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Kishia. Moja ya matukio ya umwagaji damu yaliyofanywa na Mabaath ni kutumia mabavu kuzuia shughuli za maombolezo. Katika miaka ya 1970, 1975, 1976 na 1977 Miladia, utawala wa Baath uliokuwa ukitawala wakati huo huko Iraq ulifanya mashambulio ya anga dhidi ya wafanyaziara waliokuwa njiani wakitokea Najaf kuelekea Karbala na kufanya umwagaji damu mkubwa na hivyo kuifanya Arubaini ya Damu.

Wakristo katikka matembezi ya Arubainii ya Imam Hussein as

Baada ya kusambaratika utawala wa Baath nchini Iraq, kulilipuka wimbi la watu kwenda kufanya ziara huko Karbala na kuyafanya matembezi ya Arubaini kuwa, mkusabnyiko mkubwa zaidi wa kimaanawi na wenye hamasa ya aina yake ulimwenguni.

Mwaka 2003 idadi ya watu walioshiriki katika matembezi makubwa ya Arubaini iliripotiwa kuwa milioni mbili hadi tatu. Idadi hiyo iliongezeka mno mwaka uliopita wa 2018 na kufikia milioni 20.

Kwa hakika katika matembezi ya Arubaini si Mashia au Waislamu tu wa madhehebu mengine wanaoshiriki katika mkusanyiko huo, bali kuna hata wafuasi wa dini nyingine wakiwemo Wakristo ambao nao hushiriki katika matembezi hayo na kuonyesha, heshima na mapeniz yao makubwa waliyonayo kwa Bwana wa Mashahidi Imam Hussein as.

Wapenzi wasikilizaji, tunakamilisha kipindi hiki maalumu cha Histroria ya Matembezi ya Imam Hussein as kwa kunukuu sehemu nyingine ya maneno ya Bibi Zaynab as kwa Yazid:

 Ewe Yazid! Tumia udanganyifu wako wote ulionao hadi moyo wako utosheke. Jaribu njia zote. Ongeza kasi ya juhudi zako na utimize matakwa yako. Hata hivyo, kumbuka kwamba, pamoja na yote haya, hutaweza kuharibu jina letu katika dunia hii au kuweza kupunguza heshima yetu au kusitisha kuenea kwa maoni yetu. Ni wewe ndiye utakayeangamizwa."

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabakaatuh

Tags