Kuuawa shahidi Imam Hassan Askari (as)
Imam Hassan Askari (as) aliuawa shahidi mwaka 260 Hijiria sawa na mwaka 873 Miladia kutokana na njama iliyofanywa katika siku kama hizi na mmoja wa watawala dhalimu wa Bani Abbas.
Mwaka 260 Hijiria sawa na mwaka 873 Miladia moja ya maua ya bustani ya Ahlul Bait wa Mtume Mtukufu (saw) lilinyauka na jua la umri wake wenye saada na faida kubwa kwa wanadamu kutua. Imam Hassan Askari (as) aliuawa shahidi katika siku kama hizi kufuatia njama iliyofanywa na mmoja wa watawala dhalimu wa Bani Abbas. Kwa mnasaba huu mchungu wa kukumbuka kifo cha Imam Hassan Askari (as), tunakupeni mkono wa pole, wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na tunakukaribisheni kusikiliza machache tuliyokuandalieni katika kipindi hiki maalaumu, karibuni.
Katika kipindi cha utawala wao, makahalifa na watawala wa Bani Ummaiyya na Bani Abbas walifanya juhudi kubwa kuwazuia watu wasipate kunufaika na mafundisho ya kimaanawi na fikra za Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw). Hii ni kwa sababu kuwepo kwa watukufu hao wa Nyumba ya Mtume (saw) au kwa ibara nyingine Ahlul Bait (as), kulikuwa kikwazo kikubwa katika njia ya watawala hao kuweza kueneza siasa zao za kidhalimu na za hadaa katika jamii. Hivyo, watawala hao walifanya kila waliloweza ili kuwaweka Ahlul Bait (as) katika mbinyo na mazingira magumu kabisa ya kimaisha. Kuhusiana na Imam Hadi na Imam Hassan Askari (as) Bani Abbas walizidisha mbinyo na mashinikizo hayo na kuyafikisha katika kilele kwa kadiri kwamba Maimamu hao hawakuweza kutembea wala kuendesha shughuli zao kirahisi kati ya watu na wafuasi wao. Watawala hao walimlazimisha Imam Hassan Askari akiwa na baba yake kuhamia katika mji wa Samarra, makao makuu ya utawala wao, ili wapate kufuatilia mienendo yao na kuwadhibiti zaidi.
Kati ya watawala wa Bani Abbas, Mu'tamid ndiye aliyewaudhi zaidi Imam Hassan Askari (as) na wafuasi wake, na kumfunga jela kwa muda fulani. Alikuwa mpenda madaraka na akitambua vyema kwamba kama hangemdhibiti Imam Askari (as) kwa wakati na kumuachilia aeneze mafundisho yake kwa uhuru miongoni mwa watu, basi muda si mrefu wangeweza kumuondoa madarakani kutokana na dhulma kubwa aliyokuwa akiwafanyia. Katika upande wa pili, Mu'tamid na watawala wengine dhalimu wa Bani Abbas walikuwa wamesikia Hadithi sahihi kutoka kwa Mtume (saw) kwamba Imam Askari (as) angezaa mtoto ambaye baadaye angeujaza ulimwengu kwa uadilifu na usawa na kuondoa kabisa utawala wa kidhalimu na uonevu. Kwa kuzingatia hilo, watawala hao walibana na kumdhibiti Imam Askari (as) kwa kila njia waliyoweza. Kuhusiana na suala hilo, Imam (as) anasema: " Bani Ummaiyya na Bani Abbas walitulenga kwa mapanga yao kwa dalili mbili. Ya kwanza ni kuwa walitambua vyema kwamba ukhalifa na uongozi wa Uislamu haikuwa haki yao na wala hawakuwa na hadhi yoyote kwenye haki hiyo. Walikumbwa na wasiwasi na hofu kubwa kuwa tusije tukaanzisha mapambano ya kusimamisha utawala adilifu na wa haki. Dalili ya pili ni kwamba walikuwa wamesikia Hadithi za wazi na sahihi kwamba utawala wa madhalimu na waonevu ungeangushwa na Qaim wetu, na wao wakitambua vyema kwamba walikuwa ni watawala dhalimu na waonevu. Hivyo waliazimia kukata na kuuawa kizazi cha Mtume ili kutoruhusu kuzaliwa kwa Qaim wa Aali za Mtume (saw). Lakini Mwenyezi Mungu hakuruhusu wajue alikokuwa Qaim (af) ili apate kudhihiri na kusimamisha utawala wake wa uadilifu hata kama makafiri watachukizwa na jambo hilo."
Licha ya uadui na njama zote hizo zilizofanywa na watawala wa Bani Abbas dhidi ya Ahlul Bait wa Mtume Mtukufu (saw), lakini njama na uadui huo haukumfanya Imam Hassan Askari (as) aache kuwatakia mema na kuwasaidia watawala hao katika utatuzi wa matatizo mengi yaliyoikumba serikali ya Kiislamu katika kipindi cha uhai wake. Imam (as) alikuwa kiongozi wa wanazuoni na wanamapambano wa kisiasa na kiitikadi katika zama zake. Katika zama hizo, wafuasi wa Imam Hassan Askari (as) walijishughulisha na uanezaji wa Hadithi na mafundisho ya Ahlul Bait wa Mtume (saw) pamoja na sheria za Kiislamu.
Licha ya kukabiliwa na hali ngumu ya kisiasa katika zama zake, Lakini Imam Hassan Askari (as) alitumia uwezo wake wote kutetea sheria za Kiislamu na kupambana na bida' na uzushi katika Uislamu. Juhudi kubwa za kielimu, kubainisha mitazamo na fikra safi na sahihi za Uislamu, kuanizsha mawasiliano na Mashia walioishi katika sehemu za mbali zaidi duniani na kuwatayarisha kwa ajili ya kipindi cha ghaiba (kutokuwepo machoni) ya Imam wa kumi na mbili, ni miongoni mwa majukumu muhimu aliyokuwa nayo Imam Hassan Askari (as).
Imam Hassan Askari (as) alikuwa mja bora na wa kupigiwa mfano kuhusiana na suala la ibada na ucha-Mungu. Abu Hisham Ja'ffari mmoja wa wafuasi wa Imam Hassan Askari (as) anasema: 'Wakati wa swala ulipofika, aliacha shughuli aliyokuwa akiifanya na hakutanguliza kazi yoyote mbele ya swala. Uwepo mtukufu wa Imam (as) lilikuwa dhihirisho la kuvutia la ibada na kunyenyekea mbele ya Mwenyezi Mungu.'
Historia inatwambia kuwa maafisa kadhaa wa utawala wa Bani Abbas na hasa walinzi wa jela, walishuhudia na kuvutiwa sana na unyenyekevu mkubwa alioudhihirisha Imam Hassan Askari (as) alipokuwa kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu. Alidhihirisha ikhlasi kubwa mbele ya Muumba wake na hivyo kuwavutia pakubwa maafisa hao wa utawala wa Bani Abbas kiasi cha kuwafanya wabadilishe mkondo na kufuata njia sahihi na ya saada ya Imam (as).
Imam Hassan (askari (as) alikuwa mwenye huruma kubwa zaidi miongoni mwa watu na aliteua mawakili katika maeneo mengi ya Kiislamu ili wapate kutatua matatizo yaliyokuwa yakiwakabili wakazi wa maeneo hayo na kuwatengea watu masikini na wasiojiweza kiwango maalumu cha msaada wa fedha. Aliwataka mawakili hao kutumia fedha hizo katika kutatua matatizo ya watu, masuala ya heri, kuondoa hitilafu miongoni mwa Waislamu na mambo mengine yenye manufaa kwa umma wa Kiislamu. Mbali na hayo, katika nasaha zake, Imam (as) aliwaomba watu wawe na subira na kulinda heshima zao katika kukabiliana na matatizo na changamoto tofauti za maisha. Anasema katika moja ya nasaha zake hizo za busara kwa mmoja wa wafuasi wake: "Kadiri unavyoweza kujizuia, isimuombe mtu. Hii ni kwa sababu kila siku ina riziki yake mpya, na fahamu kwamba kuombaomba humuondolea mtu heshima na thamani yake. Hivyo kuwa na subira hadi Mwenyezi Mungu atakapokufungulia mlango. Fursa na neema kila moja ina wakati wake, hivyo usilifanyie pupa tunda ambalo halijaiva bado, bali muda wake ukifika utanufaika nalo."
Katika nasaha zake zote, Imam Hassan Askari (as) anawataka wafuasi wake wawe ni wenye kutafakari na kuwa na fikra sahihi. Anasema: "Kuweni ni wenye kutafakari! Hakika, kutafakari huhuisha nyoyo na kuzifanya kuwa makini na ni funguo za milango ya hekima. Watu wasiotumia akili zao kutafakari wala macho ya nyoyo zao kuona hakika, watafufuliwa Siku ya Kiama wakiwa vipofu." Imam (as) alibainisha wazi hakika hiyo katika barua aliyomuandikia Is'haq bin Ismail Nishaburi akimwambia kwamba atambue kuwa kila anayetoka humu duniani akiwa kipofu basi Siku ya Mwisho pia atakuwa kipofu na aliyepotea njia.
Ni wazi kuwa imani inayotokana na fikra sahihi, hufuatilia matendo mema, ibada na kumkumbuka Mwenyezi Mungu na hili ndilo jambo lenye thamani. Ni kutokana na ukweli huo ndipo Imam (as) akawa anawakumbusha wafuasi wake umuhimu wa kumkumbuka Mwenyezi Mungu na mauti, kusoma Qur'ani daima na kumswali Mtume (saw) na Aali zake (as). Anasema: "Watu wenye busara na werevu zaidi ni wale wanaokumbuka kipindi cha baada ya mauti na kuhesabu matendo ya nafsi zao wenyewe."
Ni wazi kuwa Mu'tamid hengeweza kuvumilia kuwepo mtu na shakhsia wa aina hiyo pembeni yake, hivyo aliamua kumtumia mmoja wa watu wa karibu yake kumpa Imam sumu, ambapo alilazimika kuvumilia kwa siku kadhaa akiwa kitandani, maumivu makali yaliyosababishwa na sumu hiyo. Katika kipindi hiki chote Mu'tamid alikuwa akiwatuma madaktari wake kwa Imam (as) ili kuwahadaa watu na kuwafanya wadhani kwamba alikuwa anaugua maradhi ya kawaida. Baada ya kuvumilia maumivu hayo makali, Imam hatimaye aliaga dunia shahidi siku ya Ijumaa tarehe 8 mwezi wa Rabiul Awwal mwaka 260 Hijiria wakati wa swala ya alfajiri, na kuzikwa pembeni ya kaburi takatifu la baba yake mjini Samarra katika Iraq ya leo.
Ja'ffar bin Ali mashuhuri kwa jina la Ja'ffar Kaddhab, ndugu yake Imam Hassan Askari ambaye alitaka kujipa uimamu kwa njia isiyo sahihi, alimwandikia khalifa barua akimtaka amfanye yeye kuwa imamu wa Waislamu baada ya kuaga dunia ndugu yake Imam Hassan Askari (as). Lakini khalifa Mu'tamid licha ya kuwa alikuwa na chuki kubwa dhidi ya Imam lakini alimjibu Ja'ffar Kaddhab kwa kumwambia: "Sio sisi tuliompa ndugu yako Hassan Askari cheo hicho bali ni Mwenyezi Mungu. Sisi daima tulifanya juhudi za kupunguza athari ya cheo hicho lakini kinyume chake, ilikuwa ikiongezeka na hii ni kutokana na usafi wa uzawa, tabia njema, elimu na ibada yake. Ikiwa wewe una thamani kama hiyo mbele ya wafuasi wa ndugu yako, bila shaka hauhitajii idhini yetu, na kama si hivyo sisi hatuna uwezo wa kufanya lolote."
Maneno hayo ya khalifa Mu'tamid yanabainisha wazi kwamba taa iliyowashwa na Mtume wa Uislamu (saw) pamoja na Ahlul Bait wake (as), kamwe haiwezi kuzimwa na itaendelea kuwa mwokozi wa wanadamu. Ni kama anavyosema Mtume mwenyewe wa Mwenyezi Mungu: "Ahlu Bait wangu ni kama safina ya Nuh. Kila anayeipanda ataoongoka na anayeachwa nyuma ataghariki."