Oct 10, 2022 07:44 UTC
  • Wiki ya Umoja na Maulidi ya Mtume (saw)

Siku hizi za mwezi wa Mfunguo Sita Rabiu Awwal ni fursa adhimu kwa Waislamu kote duniani kupitia tena Aya zinazohusiana na umoja na mshikamano wa Waislamu katika Qur'ani Tukufu na Hadithi za Mtume wetu Muhammad (saw) ambaye kwa mujibu wa riwaya na mapokezi mawili tofauti ya wanazuoni na wanahistoria, alizaliwa ama tarehe 12 au 17 ya mwezi huu.

Kipindi hiki cha baina ya tarehe 12 na 17 Mfunguo Sita kimetangazwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni Wiki ya Umoja na Mshikamano baina ya Waislamu wote duniani, lengo likiwa ni kuwakusanya pamoja Waislamu wote wa madhehebu na mitazamo tofauti katika Tauhidi na umoja wa Kiislamu. 

Mtume wetu mtukufu, Muhammad (saw) na muujiza wake mkubwa, Qur'ani tukufu, ndio kiungo kikubwa cha mawasiliano kati ya Waislamu na chimbuko la umoja wao katika nyakati na vipindi tofauti vya historia; na kwa vile imani ya Waislamu kwa mtukufu huyo inaandamana na mapenzi na hisia makhsusi, Mtume Muhammad (saw) ndiye kitovu cha hisia na imani zao zote. Hivyo tunaweza kusema kuwa, mhimili huo ni mojawapo ya sababu za ukaribu wa nyoyo za Waislamu na kituo cha kukurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu.

Alipozaliwa alipewa jina la Muhammad, lenye maana ya msifiwa na mstahiki. Hadi wakati huo hakuna mwanaadamu aliyekuwa amepewa jina la Muhammad. Ni jina lililoteuliwa na Mwenyezi Mungu, kama alivyokuwa yeye mwenyewe, na limetajwa na kubashiriwa katika vitabu vitakatifu vya kabla yake. Hata hivyo hii leo hakuna mwanaadamu asiyejua jina la Muhammad ambalo kwa uchache linatukuzwa na kutajwa kila siku na zaidi ya Waislamu bilioni moja ya nusu kote duniani.

Wale waliodurusu na kufanya uchunguzi kuhusu dini ya Uislamu wanajua vyema kwamba, mafanikio na maendeleo ya haraka ya Uislamu mwanzoni mwa kudhihiri kwake yalitegemea umoja na mshikamano wa Waislamu, na uwepo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (SAW). Suala hili lilikuwa mashuhuri sana mwanzoni mwa Uislamu kiasi kwamba, watafiti wamelitaja kuwa ni mojawapo ya sababu za ushawishi na kupanuka haraka dini ya Uislamu. Mtume Muhammad (saw) aliwatambua wanadamu kuwa wote ni sawa kama meno ya kitana, na alifanya jitihada kubwa za kueneza upendo na huruma baina yao. Makabila na kaumu mbalimbali zilizochagua na kukubali dini ya Uislamu zilikusanyika kwenye mhimili wa imani na kufuata mafunzo ya mtukufu huyo. Mwanafikra Mwingereza, John Davenport ameandika katika kitabu chake, An Apology for Mohammed and the Koran kwamba: "Muhammad alikuwa kwa namna ambayo kila mtu alivutiwa na sura yake yenye haiba na kuathiriwa na macho yake. Tabia na mwenendo wake wa kijamii ulikuwa sawa kwa matajiri na maskini. John Davenport anaendelea kusema kuwa: Muhammad aliyabadilisha makabila yaliyotawanyika na madogo ya ardhi yake kuwa jamii iliyoungana na ya watu wenye tabia na maadili mapya. Badala ya vita na mizozo ya mara kwa mara, dini ya Muhammad ilipandikiza ukarimu na hisani katika nafsi, na kwa sababu hii, imekuwa na athari kubwa kwa ustaarabu wa dunia", mwisho wa kunukuu.

Tunaweza kusema kwamba, takwa muhimu zaidi la Mtume Muhammad (saw) kwa Waislamu lilikuwa umoja na mshikamano, kwa sababu matokeo ya mgawanyiko yana madhara makubwa sana ambayo baadhi yake tumeyaona mara nyingi; na kutokana na hitilafu zilizojitokeza baina ya Umma wa Kiislamu na kuchochewa zaidi hitilafu hizo na maadui wa Uislamu, kulidhihiri udhaifu katika Ulimwengu wa Kiislamu, na maadui wa Waislamu wakaweza kushika hatamu za udhibiti wa masuala ya kisiasa na hata ya kijeshi ya nchi nyingi za Kiislamu na kupora rasilimali za Waislamu. Hii ni licha ya kwamba Uislamu una mambo mengi ya kuwaunganisha pamoja wafuasi wake; mojawapo na muhimu zaidi akiwa ni Mtume Muhammad mwenyewe (saw). Waislamu wote wanamtambua Muhammad Mwaminifu kama mjumbe wa mwisho wa Mwenyezi Mungu na kielelezo kamili cha uokovu na ustawi. Kwa hivyo imesisitizwa kuwa Waislamu hususan madola ya Kiislamu yanapaswa kumtambua kuwa ni mhimili wa umoja na mshikamano wa Ulimwengu wa Kiislamu hususan katika zama hizi zenye misukosuko mingi. Aya ya 46 ya Suratul Anfal inasema:

وَأَطِیعُوا۟ ٱللَّهَ وَرَسُولَهُۥ وَلَا تَنَـٰزَعُوا۟ فَتَفْشَلُوا۟ وَتَذْهَبَ رِیحُکُمْ ۖ وَٱصْبِرُوٓا۟ ۚ إِنَّ ٱللَّهَ مَعَ ٱلصَّـٰبِرِینَ

Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, wala msizozane mkavunjika moyo, na zikapotea nguvu zenu, na subirini, (simameni imara) hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri."

Umoja na mshikamano ni jambo muhimu na la dharura baina ya Waislamu. Kwa sababu hiyo, katika Aya yake iliyo wazi kabisa kuhusu umoja, Qur'ani tukufu imewataka waumini wote kushika kamba ya Mwenyezi Mungu kwa pamoja na kuepuka mifarakano. Aya ya 103 ya Suratu Aal Imran inasema:

وَٱعْتَصِمُوا۟ بِحَبْلِ ٱللَّهِ جَمِیعًۭا وَلَا تَفَرَّقُوا۟ ۚ وَٱذْکُرُوا۟ نِعْمَتَ ٱللَّهِ عَلَیْکُمْ إِذْ کُنتُمْ أَعْدَآءًۭ فَأَلَّفَ بَیْنَ قُلُوبِکُمْ فَأَصْبَحْتُم بِنِعْمَتِهِۦٓ إِخْوَٰنًۭا وَکُنتُمْ

Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu; mlipokuwa maadui Naye akaziunganisha nyoyo zenu; hivyo kwa neema Yake mkawa ndugu..." Baadhi ya wafasiri wa Qur'ani tukufu wanasema, mfano bora na wa wazi zaidi wa Kamba ya Mwenyezi Mungu ni Qur'ani yenyewe. Mtume (saw) pia ameielezea Qur'ani kuwa ni kamba ya Mwenyezi Mungu SW iliyotandazwa baina ya mbingu na ardhi. Qur'ani pia imewataka waumini kurejea kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wakati wa migogoro na hitilafu zao. Qur'ani Tukufu inaitaja migawanyiko kuwa ni matokeo ya roho ya ubinafsi, vinyongo na chuki baina ya wanaadamu na kukumbusha kwamba, watu wa zama zilizopita pia walishindwa kukwea ngazi za ukamilifu na maendeleo na kufikia malengo yao aali kutokana na kuwa na mioyo ya aina hiyo. Kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu kinataja umoja wa nyoyo kati ya wanaadamu kuwa mojawapo ya baraka za Mola Muumba SW ambazo huwafikisha wanaadamu kwenye maisha yenye furaha na saada. 

Tunapotazama hehistoria na pandashuka za kipindi cha awali cha kudhihiri Uislamu, tunafikia hitimisho kwamba, utukufu na maendeleo ya Ulimwengu wa Kiislamu vilipatikana katika kivuli cha kujiepusha na migogoro na hitilafu, na chini ya umoja na mshikamano wa Waislamu. Ni kutokana na mshikamano na umoja huo ndipo Waislamu wakaweza kuzishinda tawala zilizokuwa na nguvu wakati huo za Roma na Iran na kuanzisha utamaduni na ustaarabu mkubwa ulioenea dunia nzima; kiasi kwamba baadhi ya wanafikra wa Kimagharibi wanakiri kwamba, mageuzi makubwa ya kipindi cha mwamko wa Ulaya, Renaissance, yalitegemea maendeleo makubwa ya kielimu na ustaarabu wa Kiislamu. Kwa mfano tu, katika ulimwengu wa tiba, Ibn Sina (Avicenna) alijulikana kama mkuu na kinara wa taaluma hiyo duniani na amekuwa na nafasi muhimu katika vyuo vikuu mashuhuri kwa kipindi cha miaka 700 kutokana na kitabu chake maarufu cha elimu ya tiba cha The Canon of Medicine chenye juzuu 14. Zakariya Razi, baba wa sayansi ya tiba, Abu Rayhan Biruni, Omar Khayyam, Khwaja Nasiruddin Tusi, Ibn Haitham na wanasayansi wengine wengi wa Ulimwengu wa Kiislamu walikuwa na nafasi muhimu katika kuasisi sayansi na msingi wa mfumo wa elimu duniani na katika ustaarabu wa Kiislamu. Vilevile Algebra ni matunda ya juhudi za Khwarazmi na Algorithm imepewa jina la mwanasayansi huyu.

Uwezo wa ustaarabu wa Kiislamu yalikuwa matunda ya kazi kubwa ya Mtume Muhammad (saw) ambaye mafanikio yake muhimu ni kuunda Umma wa Kiislamu. Hata hivyo hapana shaka yoyote kwamba, masuala mengi ya kihistoria yamekuwa pia na taaathira katika msafara wa Umma wa Kiislamu.

Kila mwaka, inapofika Wiki ya Umoja na maadhimisho ya Maulidi na kuzaliwa Mtume Muhammad (saw), matumaini ya kufufuka ustaarabu wa Kiislamu na kurejea tena nguvu yao hupata nguvu zaidi na zaidi. Hasa ikizingatiwa kwamba, mlango wa mazungumzo na kukurubiana zaidi madhehebu mbalimbali uko wazi, na wanafikra na wanazuoni wa kidini wanaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha kwamba kaulimbiu ya kushikamana barabara na Kamba ya Mwenyezi Mungu inatekelezwa kivitendo siku baada ya siku. 

Tags