Oct 06, 2025 02:20 UTC
  • Jumatatu, Oktoba 6, 2025

Leo ni Jumatatu tarehe 14 Mehr, 1404 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 13 Rabiuthani, 1447 Hijria Qamaria, na inayosadifiana na Oktoba 6, 2025 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1228 iliyopita yaani tarehe 13 Rabiuthani mwaka 219 Hijria aliaga dunia Ibn Hisham msomi na mwanazuoni mkubwa wa Kiarabu. Ibn Hisham alizaliwa Basra nchini Iraq na alibobea katika elimu ya fasihi na utungaji mashairi. Alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufanya uchunguzi kuhusu maisha ya Nabii Muhammad (saw). Umashuhuri mkubwa wa Ibn Hisham unatokana na kitabu chake cha al Sira al Nabawiyya ambacho ni miongoni mwa marejeo muhimu kuhusu maisha ya Mtume Muhammad (saw).

***************

Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani Oktoba 6, mwaka 1981 maafisa kadhaa wa kundi la Kiislamu la "Al-Jihad" walishambulia na kumuua rais wa wakati huo wa Misri, Muhammad Anwar Sadat. Rais huyo aliuawa kwa sababu ya kutia saini makubaliano ya udhalilishaji ya Camp David mnamo mwaka 1978 na utawala ghasibu wa Israel sambamba na kuutambua rasmi utawala huo haramu. Kufuatia hatua hiyo rais huyo alihesabiwa kuwa msaliti wa malengo matukufu ya Waislamu na Waarabu. Kwa upande mwingine hatua hiyo ilipelekea kutengwa Misri baina ya nchi za Kiislamu. Ni kwa sababu hiyo ndipo makundi ya Kiislamu na wanamapambano wa Misri wakaamua kumuua Sadat, ambaye alionekana kuwa msaliti mkubwa kwa kuutambua rasmi utawala huo ghasibu unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu. Aliyetekeleza mauaji hayo alikuwa Khalid Islambuli, mmoja wa maafisa wa jeshi la Misri wakati huo. 

***************

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita sawa na tarehe 6 Oktoba mwaka 1973, vilianza vita vya nne kati ya Waarabu na utawala ghasibu wa Israel. Katika siku hiyo jeshi la Misri lilivishambulia vikosi vya utawala huo haramu katika oparesheni ya kushtukiza katika upande wa pili wa Mfereji wa Suez. Baada ya kuvunja mstari imara wa ulinzi wa Barlow, vikosi hivyo vikafanikiwa kuingia katika jangwa la Sinai. Katika vita hivyo vikosi vya majeshi ya Misri na Syria viliyatia hasara kubwa majeshi ya utawala wa Israel na idadi kadhaa ya ndege za kivita za Wazayuni zikasambaratishwa. Hata hivyo kutokana na hatua ya Marekani ya kuupatia silaha za kisasa utawala huo wa Kizayuni, Waarabu walipoteza baadhi ya ushindi waliokuwa wameupata katika vita hivyo.

***************

Na leo tarehe 6 Oktoba ni siku ya taifa ya Misri. Misri ambayo ni moja kati ya tamaduni za kale zaidi duniani ilianzisha serikali ya jamhuri yenye bunge baada ya kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Jamhuri ya Kiarabu ya Misri ina siku mbili za taifa ambazo ni tarehe 23 Julai na 6 Oktoba. Tarehe 23 Julai ni siku ya mapinduzi dhidi ya utawala wa kifalme wa Mfalme Faruq hapo mwaka 1952 mapinduzi ambayo yaliandaa uwanja wa kutangazwa jamhuri ya nchi hiyo.