Oct 11, 2022 06:52 UTC
  • Uhusiano wa Umoja na ustaarabu wa kisasa wa Kiislamu (Wiki ya Umoja wa Kiislamu)

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema moja ya malengo ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni kuunda ustaarabu wa kisasa wa Kiislamu na kuwa lengo hilo haliwezi kufikiwa ila kwa kuwepo umoja wa Shia na Sunni.

Amesema: "Kiashiria kikuu cha kuwaunganisha Waislamu ni suala la Palestina, na kila mara juhudi zaidi zinapoofanyika kwa ajili ya kuhuisha haki za Wapalestina, ndivyo umoja wa Kiislamu unavyozidi kuimarika."

Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni wakati wa kuzaliwa Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw), ambaye ni kielelezo cha amani na upendo kwa wafuasi wa kweli wa Uislamu. Moja ya sifa mashuhuri zaidi za Mtukufu Mtume (saw) ilikuwa ni tabia yake njema, na katika historia nzima ya mwanadamu, hakuna mtu yeyote ambaye aliweza kukusanya pamoja makundi yenye mioyo migumu na ya jangwani ya wakati huo na kuunda umoja na maelewano kati yao, kama alivyofanikiwa kufanya Mtume Mtukufu (saw).

 

Kutokana na tabia yake njema na iliyowavutia wengi, Mtume (saw) aliweza kuwakusanya karibu naye washirikina wote na watu wa zama zake na kuarifisha dini tukufu ya Uislamu kwa ulimwengu mzima. Umoja baina ya Waislamu na baina ya madhehebu ya Kiislamu ni jambo la dharura na muhimu sana. Moja ya nukta muhimu alizozizingatia Mtukufu Mtume (saw) ni kanuni ya umoja, ambayo iliweza kuwaunganisha pamoja watu wa zama zake. Bila shaka, umoja na uelewa baina ya Waislamu, kuhuishwa utu wa mwanadamu na kupinga ukabila ni miongoni mwa baraka zilizoletwa na Mtume Mtukufu (saw).

Kubaathiwa Mtume (saw) ni tukio kubwa la kihistoria na mabadiliko makubwa katika historia ya mwanadamu, ambayo Mwenyezi Mungu anayachukulia kuwa ni baraka kubwa zaidi kwa wanadamu. Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu alimchagua mtu mmoja miongoni mwa wanadamu na kumtunuku daraja la ukamilifu ili awe kiungo muhimu cha kimaanawi kati ya ardhi na mbingu na kuwafundisha watu njia ya kufikia elimu na ukweli kuhusu uumbaji wa mbingu na ardhi. Ni wazi kuwa ustaarabu mpya wa Kiislamu, hauwezi kufikiwa bila kuwepo umoja wa Umma wa Kiislamu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ustaarabu wa Kiislamu unakusudiwa kuwanufaisha wanadamu wote ambao wanatakiwa kuishi chini ya kivuli chake cha kiroho na uadilifu kamili.

 

Mtume Muhammad (saw) alitumwa kwa ajili ya kuwatoa wanadamu kwenye giza na kuwaongoza kwenye njia ya ukamilifu. Kwa hakika, kazi ya kwanza ya Mtume (saw) ilikuwa ni kuwapa wanadamu elimu na ukweli kuhusu ulimwengu, tauhidi safi, kumjua Mwenyezi Mungu na mwanzo na mwisho wa maisha, ili waweze kufikia ukamilifu na saada chini ya maarifa hayo. Kubaathiwa  Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw) kulikuwa dhihirisho la nuru katika kilele cha giza na ujinga ambapo aliwaongoza wanadamu wote kutoka kwenye ukafiri na giza na kuwaelekeza kwenye nuru na ucha-Mungu.

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran anawahutubu vijana wa Kiislamu kwa kusema: “Vijana wa Kishia na Kisunni wanapasa kujua kwamba maelewano, kuishi pamoja kwa amani, kuelewana na kuhurumiana baina yao ni jambo kubwa na muhimu sana. Hiki ndicho chombo muhimu zaidi kinachopasa kutumika dhidi ya adui wa Iran, Uislamu na Qurani. Wanapasa kulijua hili vizuri na kulilinda. Hii leo harakati yoyote inayoongoza kwenye umoja wa Umma wa Kiislamu imebarikiwa na ni amali njema. Lengo la maadui wa Uislamu ni kuleta mgawanyiko. Nia yetu waumini wa Uislamu inapasa kuwa ni kuimarisha umoja katika ulimwengu wa Kiislamu na miongoni mwa Umma wa Kiislamu."

Umoja na mshikamano wa Umma wa Kiislamu utaupa nguvu na kuwafanya maadui wa kigeni wasithubutu kuingilia masuala ya ndani ya nchi za Kiislamu. Katika miongo ya karibuni tumeshuhudia nchi za kibeberu zikishambulia na kuvamia nchi za Kiislamu kwa visingizio bandia eti vya kuzidhaminia usalama na uhuru ambapo si tu kwamba hilo halikuthibiti bali ziliharibu zaidi usalama wa nchi hizo na kukanyaga ustaarabu na utamaduni wao. Kwa mfano katika nchi kama vile Iraq ambayo ina ustaarabu unaorudi nyuma maelfu ya miaka, askari wa Marekani waliivamia nchi hiyo na kuharibu na kupora ustaarabu huo bila kujali lolote. Si hayo tu bali walipora hata utajiri wake wa mafuta, kuharibu turathi zake na kuua kinyama zaidi ya watu nusu milioni wa nchi hiyo wakiwemo wanawake na watoto wachanga.


Akizungumza mbele ya washiriki na wageni wa mkutano wa Umoja wa Kiislamu mwaka jana, Ayatullah Khamenei alisema kuwa jukumu la Umma wa Kiislamu ni kubainisha na kueneza mafundisho ya Uislamu katika pembe zote za maisha ya mwanadamu na kuongeza kuwa mihimili ya kisiasa na kimaada daima hufanya juhudi za kubana na kuutenga Uislamu katika eneo moja tu la maisha na kutaka kuufanya kuwa usiohusiana na pande zote za maisha ya mwanadamu. Alisisitiza kuwa Uislamu sio dini inayohusiana tu na maisha ya mtu binafsi na ya kiroho ya mwanadamu bali inahusiana na jamii nzima ikijumuisha masuala yake ya kiutamaduni, kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Mwenyezi Mungu Katika Qur'ani Tukufu anawabashiria ushindi Waislamu lakini anasisitiza kwamba hilo litawezekana tu iwapo watajitenga na ugomvi, mapigano na migawanyiko na kuzingatia mambo yanayowakutanisha na kuwaunganisha pamoja kama Umma wa Kiislamu. Anasema katika Aya ya 46 ya Surat Anfaal: Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri.

Maadui na tawala za kibeberu daima hupanga na kutekeleza njama za uhasama na chuki dhidi ya dini tukufu ya Uislamu na ili kufikia lengo hilo hueneza uongo na uzushi dhidi ya Uislamu na kizazi cha Mtume Mtukufu (saw) ili kwa njia hiyo zipate kuwatenganisha Waislamu na kwa bahati mbaya zimefanikiwa kufikia baadhi ya malengo yao hayo maovu dhidi ya Umma wa Kiislamu.


Suala la kutisha na kuenezwa chuki dhidi ya Uislamu ni jambo ambalo limefanya kuwepo udharura wa kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Umma wa Kiislamu. Serikali za Kiislamu zinapaswa kuchukua tahadhari kubwa na kutoruhusu maadui wa Uislamu kuingilia masuala ya ndani ya Umma wa Kiislamu kwa madhumuni ya kuibua fitina za kuwatenganisha. Waislamu wanapasa kutambua kwamba kunaweza kuwepo tofauti za kifikra na kimtazamo kuhusiana na masuala tofauti ya kifikhi, kiitikadi na kihistoria lakini hilo halipasi kuwa chanzo cha kuwatenganisha bali wanawajibika kuzingatia masuala yanayowakutanisha na kuwaweka pamoja kama Umma wa Kiislamu. Madhehebu yote ya Kiislamu licha ya kuwa na tofauti za kifikhi na kiitikadi lakini yote kwa pamoja yanapasa kutilia maanani misingi ya kiitikadi inayoyakutanisha kama Umma mmoja wa Kiislamu, kama vile Tauhidi, Qur'ani, Mtume na Kibla kimoja na kujiepusha na mambo yanayowatenganisha ambayo ndiyo yanayofuatiliwa na maadui wa Uislamu ili kufikia malengo yao maovu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Tags