Mapinduzi ya Kiislamu na matunda yake ya kiuchumi (2)
Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi na karibuni katika sehemu hii nyingine ya mfululizo wa makala zetu maalumu tulizokuandalieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 44 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran. Leo tutaendelea kuzungumzia matunda ya kiuchumi ya mapinduzi hayo matukufu tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hawi mwisho wa kipindi.
Wasikilizaji wapenzi, miongoni mwa shughuli na harakati za kiuchumi za Iran, na ambazo pia ni sehemu ya sera za kimkakati za Jamhuri ya Kiislamu, ni kuimarisha uchumi unaotegemea taasisi ambazo msingi wake ni elimu na maarifa. Kiongozi mpendwa, mwenye hikma na makini wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, mara kwa mara amekuwa akinukuu usemi wa Amirul Muumini, Imam Ali bin Abi Talib uliomo kwenye kitabu kitukufu cha Nahjul Balagha ambao unasema: "Elimu ni Sultani...” Naam, elimu ni nguvu. Moja ya nasaha za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na mawaidha yake ya mtawalia kwa wananchi na viongozi ni kuzingatia na kujifunza sayansi na kuwekeza ndani yake. Amesema: “Tunahitaji maendeleo ya kisayansi; Hili ndilo hitajio letu la uhakika. Ikiwa hatutaendelea kisayansi, tishio la maadui wa ustaarabu na maadui wetu wa kiutamaduni na kisiasa litakuwa la mara kwa mara. Tukiendelea kisayansi tishio litashimamishwa au hatari yake itapungua.
*******
Katika ulimwengu mpya, nguvu halisi itakuwa ya nchi ambazo zitafikia teknolojia mpya na uvumbuzi. Kwa hiyo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu anasisitiza uchumi unaotegemea sayansi kwa namna ya kuunda makampuni yenye ujuzi ili kuunda ubunifu na kuongeza tija na ufanisi wa kazi katika nyanja mbalimbali za uchumi. Licha ya kuwa na idadi kubwa ya vijana na wafanyakazi wenye elimu, Iran ina uwezo mkubwa pia wa kutumia sayansi na maarifa kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa uchumi humu nchini. Kwa hivyo, kuwekeza katika uchumi unaotegemea maarifa kunapaswa kuzingatiwa kuwa moja ya mafanikio muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu. Ubunifu, utafiti na maendeleo huunda misingi ya uchumi unaotegemea maarifa. Katika muda wa chini ya muongo mmoja, Iran iliweza kuboresha nafasi na hadhi yake katika masuala ya uvumbuzi miongoni mwa nchi zilizofanyiwa utafiti kiasi kwamba Iran imeweza kupanda kutoka kutoka nchi ya 120 hadi ya 60. Zaidi ya makusanyo 7,000 ya makampuni yanayotegemea maarifa na makampuni 1,600 ya ubunifu yamesajiliwa nchini Iran. Makampuni haya yanajihusisha na nyanja mbalimbali za kiteknolojia kama vile bioteknolojia, kilimo na viwanda vya chakula, teknolojia ya kemikali, mashine na vifaa vingine vya hali ya juu, vifaa vya tiba na umeme, mawasiliano ya simu, teknolojia ya habari na programu za kompyuta, na hutoa huduma zao kwa jamii na kwa matumizi ya viwandani.
*******
Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, Iran imepata maendeleo mazuri katika uga wa vifaa vya tiba na vifaa vinginevyo na kufikia kujitosheleza katika uzalishaji wa bidhaa nyingi. Zaidi ya kampuni 3,500 na mashirika 248 yanayotegemea elimu na maarifa na yanafanya kazi katika uwanja wa vifaa vya matibabu nchini Iran. Wataalamu wenye umahiri mkubwa wa Iran wameweza kuondoa ukiritimba wa baadhi ya nchi na makampuni makubwa ya kimataifa kwa kuzalisha baadhi ya vifaa vya matibabu vya hali ya juu.
Kwa mfano, tunaweza kutaja mafanikio ya kipekee ya tasnia ya vifaa vya matibabu wakati wa janga la corona. Sambamba na na kuanza janga la corona, nchi nyingi ulimwenguni zilikumbwa na uhaba mkubwa wa vifaa vya matibabu na bidhaa za watumiaji kiasi kwamba baadhi ya nchi hazikuruhusu kutuma hata barakoa moja kwa nchi nyingine bali hata zilifikia kupora bidhaa za nchi nyingine na kujikumbizia wao. Wakati huo na licha ya vikwazo vya kimataifa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, lakini wazalishaji wa Iran waliweza kukidhi mahitaji ya nchi na hata kuuza nje bidhaa zao katika kipindi kifupi tu cha tangu kuanza janga hilo. Leo hii, bidhaa na vifaa vya matibabu vya Iran vinasafirishwa kwa zaidi ya nchi 50 duniani. Kuwepo madaktari na wataalamu waliobobea, vituo vya matibabu vilivyo na vifaa vya hali ya juu na gharama nafuu kumesababisha mamia ya maelfu ya wagonjwa kutoka nchi jirani kuja kupata matibabu katika Iran ya Kiislamu kila mwaka.
*******
Faida na kazi za makampuni yenye msingi wa elimu na maarifa zinaonekana pia katika maeneo mengine ya uchumi nchini Iran. Kwa mfano, katika sekta ya kilimo. Hapa kwenye sekta hii, tunaweza kuzungumza juu ya matumizi ya teknolojia ya kisasa ya kutumia droni na ndege zisizo na rubani kunyunyiza dawa na kufuatilia ukuaji wa mimea na kupambana na wadudu wanaoharibu mimea. Makampuni 298 yanayotegemea elimu, maarifa na ubunifu, yanafanya kazi katika sekta za kilimo, teknolojia ya kisasa ya jiolojia kwenye uwanja huo na sekta nzima ya chakula nchini Iran. Mafanikio hayo yameifanya Jamhuri ya Kiislamu kuwa msafirishaji mkubwa wa mazao kwa nchi nyingine mbali na kushibisha soko la humu ndani. Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni kabisa ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) mwaka 2020, Iran ilishika baina ya nafasi ya tatu hadi kumi na tisa katika uzalishaji wa bidhaa 20 muhimu za kilimo duniani.
*******
Katika sekta ya viwanda na madini pia, hadi kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, viwanda vya Iran vilitegemea zaidi vifaa vya nchi za kigeni katika masuala ya teknolojia, mitambo na baadhi ya malighafi. Hii ilikuwa mbaya kiasi kwamba, vifaa viliopochelewa kidogo tu kuingia humu nchini kutoka nje, uzalishaji wa bidhaa za viwandani uliporomoka. Hivi leo lakini, mashine na sehemu kubwa zinazohitajiwa na viwanda na migodi ya Iran zinazalishwa humu humu nchini na wataalamu vijana na wenye uwezo wa kutosha wa Iran. Hivyo, ustawi wa kiuchumi unaonekana katika sekta zote nchini Iran. Takwimu za sekta za madini zinathibitisha ukweli wa uhakika huo.
*******
Maeneo ya viwanda na maeneo maalumu ya kiuchumi yamenawiri na kupiga hatua kubwa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1979, maeneo ya viwanda yenye huduma zote muhimu za mji kama maji, umeme, gesi na huduma za simu yalikuwa mawili tu. Lakini leo, idadi ya maeneo hayo inafikia karibu 600. Katika uwanja wa uzalishaji chakula, vinywaji, n.k pia, idadi ya karakana kubwa za viwandani imeongezeka kutoka karakana 719 kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu yaani mwaka 1976 na kufikia hadi karakana zaidi ya 2,700 hivi sasa. Vile vile katika uwanja wa viwanda vya nguo, vitambaa, ngozi na ngozi mwigo, karakana za uzalishaji wa vituo hivyo zimeongezeka maradufu. Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu yaani mwaka 1976, kulikuwa na karakana 166 zilizokuwa zikifanya kazi ya kuzalisha na kutengeneza bidhaa za karatasi, usambazi vitabu na uchapishaji. Lakini leo, idadi ya makampuni yenye karakana za kufanya kazi hiyo yamefikia takriban 500. Hivi sasa, kuna karakana nyingi nchini Iran zinazofanya kazi ya uzalishaji wa bidhaa za viwandani, vifaa vya nyumbani, magari, n.k.
*******
Katika upande wa migodi na sekta ya madini pia, kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, Iran ilikuwa na migodi isiyofika 200 lakini hivi sasa migodi hiyo imefikia 10,000. Asilimia 60 ya utajiri wa madini wa Iran hivi sasa unazalishwa kwa ajili na kutumika kwenye vifaa vya ujenzi. Madini mengine yanayozalishwa na wataalamu wa ndani ya Iran kwa kuktumia vifaa vilivyotengenezwa na vijana wenyewe wa Iran ni feleji na n.k. Hapa tutataja madini ya aina mbili ambayo ni muhimu mno katika ustawi na maendeleo duniani yaani, chuma na saruji. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2022, Iran ilizalisha tani milioni 6.9 za chuma na kuwa miongoni mwa nchi 10 zinazozalisha kwa wingi bidhaa hiyo ya kimkakati duniani. Leo, kuna takriban viwanda 100 vya chuma vinavyofanya kazi ya uzalishaji nchini Iran. Bidhaa nyingine muhimu ya kiistratijia ambayo uzalishaji wake mkubwa ni ishara ya ustawi na maendeleo, ni saruji. Iran hivi sasa ina uwezo wa kuzalisha aina 27 za saruji ya kijivujivu, chokaa na rangi. Mwaka 2021, Iran ilikuwa kati ya wazalishaji wanane wakubwa wa saruji ulimwenguni. Kuna takriban viwanda 80 nchini Iran vinavyofanya kazi katika uzalishaji wa madini hayo, ambayo mbali na kukidhi mahitaji ya ndani, viwanda hivyo vinasafirisha kwa wingi bidhaa zake katika nchi jirani kama vile Iraq, Afghanistan, Syria, Kuwait, Oman, Pakistan, Qatar, Turkmenistan na Kazakhstan na nje ya bara la Asia.
*******
Mizani ya kibiashara ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaonesha kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, mauzo ya Iran ya bidhaa zisizo za mafuta katika nchi jirani na ukanda huu wa Asia Magharibi, yameongezeka kwa kiasi kikubwa. Kwa mujibu wa Waziri wa hivi sasa wa Viwanda na Madini wa Iran, Bw. Fatemi Amin, mauzo ya Iran nje ya nchi ya bidhaa zisizo za mafuta na gesi, yanaongezeka kwa kasi na inatarajiwa kwamba mafuta yataondolewa kwenye mizani ya bidhaa za biashara mwaka ujao. Amesema, lengo letu hivi sasa ni kuuza nje bidhaa zetu hizo si tu kwa shabaha ya kupata fedha za kigeni, lakini pia kuthibitisha nguvu zetu za kiuchumi duniani. Hivyo, tunapaswa kuachana na uzalishaji na usafirishaji nje malighafi kama mafuta, na badala yake tutegemee bidhaa nyingine kama vile dawa na vifaa ambavyo ni nchi chache zinaweza kuzizalisha. Hadhi ya Iran mwaka 2021 ilikuwa ni nambari 65 katika orodha ya nchi zinazotegemea elimu na maarifa katika uzalishaji na kusafirisha nje bidhaa. Juhudi zinazofanyika hivi sasa ni kuhakikisha nafasi ya Iran inakuwa chini ya 40 katika faharasa na orodha hiyo katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Hilo likifanyika, Iran itatambuliwa kuwa nchi yenye uchumi unaotegemea kikamilifu elimu na maarifa duniani.
*******
Ustawi wa vifaa vya mawasiliano ni moja ya mambo yanayoifanya nchi kuwa karibu na ufanikishaji wa jambo hilo. Satelaiti zina nafasi muhimu sana katika ustawi na maendeleo. Huko nyuma, kazi kubwa za satelaiti zilikuwa zinahusiana na masuala ya usalama au ushindani, lakini leo masuala ya kiuchumi na matumizi ya maendeleo ya teknolojia hiyo yamekuwa muhimu sana. Picha na data zinazotumwa na satelaiti zina matumizi makubwa na muhimu, kuanzia kwenye mawasiliano hadi kwenye kutabiri majanga ya kimaumbile na kudhibiti athari zake ili kupunguza uharibifu na pia kwenye uvumbuzi wa madini, ufuatiliaji wa mabadiliko ya hali ya hewa, ufuatiliaji wa misitu, malisho na viumbe wa baharini. Hivi sasa, mashirika na makampuni ya Iran yanayotegemea elimu na maarifa yanafanya kazi ya kubuni na kutengeneza satelaiti, vituo vya kurushia satelaiti hizo anga za mbali, vituo vya kupokea picha na data kutoka kwenye satelaiti hizo n.k. Moja ya mafanikio ya karibuni kabisa ya Iran katika uwanja huo ni hatua yake ya kurusha anga za mbali, kombora la kubeba satelaiti liitwalo Qaim-100, ambalo lilirushwa tarehe 4 Novemba 2022, kutokana na juhudi za wataalamu wa Kikosi cha Wanaanga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH. Moja ya mipango ya kombora hilo ni ni kuipeleka satelaiti ya Nahid 1 kwenye kizingo cha dunia. Satelaiti ya Nahid ni ya mawasiliano ya simu iliyotengenezwa na Taasisi ya Utafiti wa Anga ya Iran. Kurushwa kwa mafanikio kombora hilo katika anga za mbali kunaonyesha dhamira ya Iran ya kusonga mbele kuelekea kwenye mipaka ya elimu, sayansi na teknolojia za kisasa.