Siku ya Kimataifa ya Kulindwa Tabaka la Ozoni
https://parstoday.ir/sw/radio/world-i15307-siku_ya_kimataifa_ya_kulindwa_tabaka_la_ozoni
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika kipindi hiki cha kila wiki ambapo leo tumekuandalieni makala hii kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kulindwa Tabaka la Ozoni.
(last modified 2025-12-10T03:22:38+00:00 )
Sep 14, 2016 12:22 UTC
  • Siku ya Kimataifa ya Kulindwa Tabaka la Ozoni

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika kipindi hiki cha kila wiki ambapo leo tumekuandalieni makala hii kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kulindwa Tabaka la Ozoni.

Moja ya matatizo ya mazingira duniani leo ni kuzidi kuwa jembamba tabaka la Ozoni katika anga ya sayari ya ardhi, suala ambalo linapelekea kuongezeka miale ya jua inayopiga ardhini na kuleta athari mbaya kwa mazingira na usalama wa viumbe hai ardhini. Ni kwa sababu hiyo ndio maana mwaka 1994, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitangaza tarehe 16 Septemba kuwa Siku ya Kimataifa ya Kuhifadhi Tabaka la Ozoni ili katika siku hiyo, nchi mbalimbali duniani ziweze kuwa na ratiba maalumu za kuwaelimisha watu wao hatari zinazotokana na mgogoro huo wa mazingira. Ni matumaini yangu mtakuwa nami hadi mwisho wa makala hii.

                                           

Siku ya Kimataifa ya tabaka la Ozoni

 

Tabaka la Ozoni ni mada ya kemikali iliyoundwa na molekuli moja ya Oksijeni na atomu moja ya Oksijeni na ni tabaka tete sana linaloathirika kirahisi. Katika tabaka la Ozoni kuna mchanganyiko dhaifu sana wa Molekuli Oksijeni na Atomu Oksijeni, mchanganyiko ambao ukiguswa na kitu kidogo tu huparaganyika na ukipata nishati ndogo kabisa unaungana tena. Tabaka la Ozoni ambalo kimsingi ni kama gesi; kimaumbile linakuwa ndani ya matabaka ya juu ya anga ya ardhi ndani ya tabaka la Stratosfia. Ijapokuwa gesi ya Ozoni iko pia katika tabaka lililoko karibu na ardhi, lakini katika kila molekuli milioni moja za hewa, kuna molekuli moja tu ya Ozoni kwenye tabaka hilo lililo karibu na usawa wa ardhi, wakati ambapo katika umbali wa kilomita 15 hadi 25 kutoka usawa wa ardhi, upana wa Ozoni unaongezeka hadi molekuli 6 katika kila molekuli milioni moja za hewa. Unene wa tabaka hilo la gesi ambalo ni maarufu kwa jina la Ozoni unaongezeka na kuwa mpana zaidi nyakati za usiku ikilinganishwa na mchana kutokana na kutokuwepo nishati ya mionzi ya jua nyakati za usiku.

Kuna udharura wa kulindwa tabaka la ozoni

 

Gesi ya Ozoni iliyomo ndani ya tabaka la Angahewa (Atmosfia) inafanya kazi ya ulinzi na kuchuja mionzi hatari ya Kikiuka Urujuani (Ultraviolet) yaani UV isiifikie sayari ya ardhi. Mionzi ya Kikiuka Urujuani (Ultraviolet) ni kati ya mionzi ya jua yenye hatari na madhara kwa viumbe wa ardhini. Nuru ya jua huchukua dakika 27 na sekunde 8 kufika ardhini. Asilimia 70 kati ya asilimia mia moja ya mionzi ya jua inayoelekea ardhini hupitia kwenye matabaka ya gesi yanayofunika ardhi. Mionzi ya jua inaundwa na mabilioni ya rangi za kila aina na kila rangi moja ina mawimbi na nishati yake maalumu. Moja ya mionzi hiyo inajulikana kwa jina la mionzi ya Kikiuka Urujuani (Ultraviolet) yaani UV. Mionzi ya Kikiuka Urujuani ina mawimbi mafupi na nishati kubwa sana na ni hatari kwa viumbe vyote hai ardhini. Kwa bahati nzuri, Mwenyezi Mungu amejaalia ardhi kuwa na kinga ya kuzuia mionzi hiyo hatari, kinga hiyo inajulikana kwa jina la tabaka la Ozoni. Hapa linajitokeza swali kwamba, tabaka hilo linafanya kazi vipi ya kuilinda ardhi?

Majibu ni kwamba, wakati mionzi ya UV inapogongana na molekuli za Ozoni, hupoteza sehemu kubwa ya nguvu zake na hubadilika kuwa miali isiyoonekana ya infrared, na katika upande wa pili, wakati mionzi ya UV inapogongana na tabaka la Ozoni, molekuli za Ozoni hutawanyika na kujigawa sehemu mbili, yaani Molekuli Oksijeni na Atomu Oksijeni na molekuli hizo zinapopigwa tena na jua hurudi katika hali ya gesi ya Ozoni. Hivyo ndivyo tabaka la Ozoni linavyowalinda viumbe hai ardhini wasiathiriwe na mionzi hatari ya Ultraviolet yaani UV.

Uharibifu wa tabaka la ozoni katika miongo kadhaa ya hivi karibuni

 

Hata hivyo tangu mwanzoni mwa muongo wa 1970, kwa mara ya kwanza, katika anga ya eneo la Antaktika (yaani Ncha ya Kusini mwa dunia), watafiti waligundua kuweko uharibifu katika tabaka la Ozoni. Awali ilidhaniwa kuwa, sababu za kutokea uharabifu huo ni gesi za Nitrogen Oxide zinazozalishwa na safari za ndege zinazokwenda mwendo wa kasi katika Angahewa (Atmosfia). Hata hivyo mwaka 1974 baadhi ya mada za kemikali zinazozalishwa na wanadamu zinazojulikana kwa jina la klorofluorokaboni (chlorofluorocarbon (CFC)) zilionekana katika tabaka la Ozoni. Gesi za CFC ni gesi zinazotengeneza ubaridi kwenye majokofu na viyoyozi na vilevile zinatumika katika utengenezaji wa mada za plastiki. Gesi hizo zina atomu zenye athari mbaya na wakati zinapopanda kwenda katika tabaka za juu ya ardhi, atomu za gesi hiyo hutawanyika baada ya kupigwa na mionzi ya jua na kuharibu haraka molekuli zinazounda gesi ya Ozoni. Gesi hizo za CFC ni mbaya kiasi kwamba, kila atomu yake inapotawanyika kwa kuguswa na mwanga wa jua hurudi ardhini na kabla ya kufika ardhini huwa imeshaharibu molekuli laki moja za gesi ya Ozoni. Baya zaidi ni kuwa, gesi za CFC hujitafutia makazi ya kudumu katika tabaka la Angahewa (Atmosfia) na kuendelea kufanya uharibifu katika tabaka la Ozoni kwa muda mrefu. Mwaka 1985 kundi moja la wataalamu liligundua kuweko uharibifu mkubwa katika eneo la Antaktika (Ncha ya Kusini mwa dunia), uharibifu ambao ulionekana waziwazi kwa jicho. Baada ya hapo, uharibifu mkubwa zaidi ulionekana mwaka 2006 kwenye eneo hilo. Hata hivyo janga kubwa zaidi ni kwamba, ripoti zote za Shirika la Taifa la Masuala ya Anga na Anga za Juu la Marekani zimeonesha kuwa, thuluthi mbili ya tabaka la Ozoni juu ya eneo la Ncha ya Kusini mwa dunia litakuwa limeharibiwa kikamilifu, na taathira zake kuenea dunia nzima. Wasiwasi uliopo hivi sasa ni kuwa, shimo hilo lilioko kwenye eneo la Antaktika litapelekea kuangamia maisha ya viumbe vyote hai katika sayari ya ardhi.

Kuna udharara wa kupambana vilivyo na uharibifu wa tabaka la ozoni

 

Kuharibiwa na kutoboka tabaka la Ozoni kumepelekea kuongezeka joto ardhini na kuyeyuka barafu katika ncha za dunia, suala ambalo pia limekuwa sababu ya kuongezeka maji baharini na hatimaye kuzama majini kilomita nyingi za fukwe za ardhi. Madhara mengine ya kuharibiwa tabaka la Ozoni ni kuangamia bakteria wanaotia nguvu nitrojeni inayojenga muundo wa kijenetiki wa viumbe hai katika mashamba ya mpunga, na matokeo yake ni kupungua uzalishaji katika mashamba hayo. Ni wazi kuwa, uzalishaji unapopungua, chakula nacho hupungua, na matokeo yake ni kuenea njaa duniani. Tukio hilo pia hupelekea mionzi ya Kikiuka Urujuani (Ultraviolet) aina ya A kuvutwa na tabaka la Ozoni na kupenya vibaya sana ndani ya ngozi za wanadamu na hatimaye kusababisha uzee wa kabla ya wakati wake au ugonjwa wa saratani ya ngozi. Mionzi ya Kikiuka Urujuani (Ultraviolet) aina ya B nayo ni mionzi hatari zaidi kati ya mionzi hiyo ya urujuani, kwani inapenya kwenye vina virefu vya maji na kuangamiza viumbe vya majini ambavyo vinaunda sehemu kubwa ya mzunguko wa maisha ya viumbe hai majini, hususan katika eneo la Ncha ya Kusini mwa ardhi. Utafiti uliofanywa unaonesha kuwa, asilimia 25 ya uharibifu katika tabaka la Ozoni unaweza kupelekea kuangamia asilimia 10 ya viumbe hai waishio katika tabaka la juu la bahari na asilimia 25 ya viumbe vinavyoishi katika tabaka la chini la bahari.

Ni kutokana na kulitambua vyema jambo hilo, ndiyo maana mwaka 1993 Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuja na mpango wa kuanzishwa ofisi maalumu ya kulinda tabaka la Ozoni chini ya Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na taasisi ya kulinda mazingira ya Iran. Ofisi hiyo ilianza kufanya kazi rasmi mwaka 1994 na hadi sasa kumeshachukuliwa hatua mbalimbali za kakabiliana na makundi yote ya mada zinazoharibu tabaka la Ozoni. Hatua hiyo imeifanya Iran kuwa nchi ya kwanza ya Asia na Pasifiki kuangamiza sehemu kubwa ya mada zinazoharibu tabaka la Ozoni katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Juhudi za kimataifa za kulinda tabaka la ozoni

 

Jambo la kusikitisha ni kuona kuwa Marekani, ambayo ndiye mzalishaji mkuu wa mada zinazoharibu tabaka la Ozoni duniani, inaendelea kukaidi kilio cha walimwengu cha kutekeleza mkataba kama wa Kyoto wa kukabiliana na janga hilo na kulinda mazingira. Takwimu zinaonesha kuwa Marekani inaunda asilimia kama 4 tu ya jamii ya watu wote duniani lakini nchi hiyo pekee inatumia asilimia 20 ya nishati ya fosili ya dunia na kuzalisha asilimia 25 ya "Gesi za Nyumba ya Kijani" (Green House Gas) ambazo ndizo zinazochangia sana ongezeko la joto duniani. Pamoja na hayo Washington inakataa kutekeleza majukumu yake ya kimataifa katika kulinda mazingira. Mkataba huo ulipasishwa mwezi Disemba 1997 katika mji wa Kyoto nchini Japan kwa shabaha ya kupunguza uzalishaji wa gesi hizo hatari. Baya zaidi ni kuwa tangu mwaka 2005 Marekani imekuwa msambazaji mkubwa zaidi wa gesi ya Carbon dioxide ambayo ni hatari mno kwa tabaka la Ozoni.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kukuleteeni makala hii umeisha kwa leo. Hadi wakati mwengine nakuombeeni kila la kheri maishani.