Jun 13, 2021 07:03 UTC
  • Kifungo cha miaka 10 jela kinamsubiri Benjamin Netanyahu

Wakili wa Katiba ya utawala wa Kizayuni kutoka kituo cha uchunguzi wa demokrasia cha utawala huo amesema kuwa, waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netnyahu lazima atapandishwa kizimbani baada ya kung'olewa madarakani na kwa uchache basi hawezi kukwepa kifungo cha miaka 10 jela kwa makosa yake ya ufisadi.

Amir Fuchs pia amesema, tangu mwezi Mei 2020 Netanyahu anapambana na kesi kadhaa za ufisadi, utapeli, kufilisi mali n.k, na iwapo atatimuliwa madarakani, hatokuwa na kinga yoyote ya kutoshitakiwa.

Wakili huyo vile vile amesema kuwa, kwa muda wa miaka miwili sasa kumekuwa na mjadala unaohoji itakuwaje iwapo Benjamin Netanyahu atabadilisha vipengee vya katiba ya utawala wa Kizayuni ili ajiwekee kinga ya kutoshitakiwa. Hivi sasa lakini atakuwa hana uwezo tena wa kufanya jambo hilo iwapo atatimuliwa madarakani na kwa uchache hatoweza kukwepa kifungo cha miaka 10 jela.

 

Mwendesha mashtaka mkuu wa utawala wa Kizayuni amefungua mashtaka matatu dhidi ya Benjamin Netanyahu. Kesi hizo ni maarufu kwa majina ya 1000, 2000, na 4000. Miaka yote hii Netanyahu amekuwa akifanya jinai za kinyama na za kila namna dhidi ya Wapalestina ili kujiwekea kinga ya kubakia madarakani na kukwepa kushitakiwa.

Ikumbukwe kuwa, katika vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na serikali ya Benjamin Netanyahu dhidi ya Wapalestina wa Ghaza, utawala wa Kizayuni ulipata pigo kutoka kwa wanamapambano wa Palestina.

Lakini pia wanajeshi wa Israel walifanya jinai kubwa dhidi ya watoto wadogo, wanawake na vizee wa Palestina. Wapalestina 253 waliuawa shahidi katika vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ukanda wa Ghaza mwezi Mei mwaka huu. 

Tags