Jun 14, 2021 13:06 UTC
  • Jihad Islami yaonya kuhusu hatua ya kichochezi ya Wazayuni ya 'Maandamano ya Bendera'

Harakati ya Jihad Islami ya kupigania ukombozi wa Palestina imesema mpango wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuandaa 'maandamano ya bendera' ni hatari na wa kichochezi.

Katika taarifa leo Jumatatu, Harakati ya Jihad Islami ya Palestina imetoa wito kwa Wapalestina wanaoishi katika ardhi zilizokaliwa kwa mabavu na Israel mwaka 1948 na wale walio katika Ukingo wa Magharibi na Quds Tukufu (Jerusalem) waelekee katika Msikiti wa Al Aqsa ili kuuhami Jumanne.

Jihad Islami imesisitiza kuwa, taifa la Palestina limeungana katika kuutetea na kuuhami Msikiti wa Al Aqsa mjini Quds na liko tayari kwa ajili ya mapambano na kuulinda msikiti huo unaokabiliwa na hujuma ya Wazayuni. Jihad Islami imetoa wito kwa Wapalestina kutoka miji na vijiji vyote na hata kambi za wakimbizi kuwa tayari kukabiliana na uvamizi wa aina yoyote kutoka kwa Wazayuni.

Mji wa Quds

Harakati ya Mapambani ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, nayo pia imetoa wito wa kuwepo Intifadha au mwamko wa Wapalestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel wakati wa kufanyika maandamano ya kichochezi ya 'bendera' ambayo yanapangwa na Wazayuni.

Siku ya Ijumaa , polisi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ilitangaza kuwa imeafiki mpango wa makundi ya walowezi wa Kizayuni wenye misimamo mikali ya kufurutu ada kufanya maandamano ya kichochezi yaliyopewa jina la 'maandamano ya bendera' katika mji wa Quds Jumanne.

Kwa mujibu wa taarifa, katika maandamano hayo Wazayuni watamiminiika katika mitaa ya Quds inayokaliwa kwa mabavu kwa lengo la kupeperusha bendera za utawala bandia wa Israel huku wakitoa nara za maangamizi ya kimbari dhidi ya Wapalestina.

 

Tags