Aug 04, 2023 12:09 UTC
  • Amnesty International: Uhalifu wa kutisha wa kivita unafanyika nchini Sudan

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema katika ripoti yake mpya kwamba uhalifu mkubwa wa kivita unafanywa nchini Sudan, na kwamba raia kote nchini humo wanaishi katika hufo na woga "usiofikirika".

Ripoti ya Amnesty International inasema, watu wanauawa wakiwa majumbani mwao au wakati wa kutafuta chakula, maji na dawa, na wananaswa katika mapigano wakikimbia vita na kupigwa risasi kwa makusudi katika mashambulizi ya kupanga.

Ripoti ya Amnesty International iliyopewa anwani ya "Kifo Kimekuja Nyumbani Kwetu: Uhalifu wa Kivita na Mateso ya Raia nchini Sudan," inaorodhesha vifo vya raia wengi katika mashambulizi ya makusudi na ya kiholela ya pande mbili zinazopigana, yaani vikosi vya jeshi la Sudan na vile vya Msaada wa Haraka (RSF) kwa kifupi.

Ripoti hiyo pia inaelezea unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana, mashambulizi yanayolenga taasisi za kiraia - kama hospitali na maeneo ya ibada - na uporaji mkubwa.

Makumi ya wanawake na wasichana - wengine wakiwa na umri wa miaka 12 - wamefanyiwa ukatili wa kingono, ikiwa ni pamoja na kubakwa na wanajeshi wa pande mbili zinazozozana, na wengine wameshikiliwa kwa siku kadhaa katika hali ya utumwa wa ngono.

Sudan

Amnesty International imesema, baadhi ya ukiukaji wa kupangwa - kama mashambulizi yanayolenga raia, mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kibinadamu, ubakaji na aina nyingine za unyanyasaji wa kingono, na uporaji - ni sawa na uhalifu wa kivita, na kwamba ripoti hiyo imejikita zaidi katika maeneo ya Khartoum na Darfur Magharibi.

Katibu Mkuu wa Amnesty International, Agnès Callamard amesema: "Raia kote nchini Sudan wanaishi katika hofu isiofikirika kila siku, wakati RSF na vikosi vya jeshi la Sudan vikishindana kudhibiti maeneo zaidi."

Amnesty International imetoa wito kwa vikosi vya Msaada wa Haraka na jeshi la Sudan kukomesha mashambulizi yanayowalenga raia na kuhakikisha njia salama kwa wale wanaotafuta amani. Vilevile imesisitiza ulazima wa kuchukuliwa hatua za haraka za kuwadhaminia uadilifu na fidia waathiriwa na manusura wa uhalifu huo.

Tags