Serikali na wapinzani wakabana koo Madagascar
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10084-serikali_na_wapinzani_wakabana_koo_madagascar
Serikali ya Madagascar na wapinzani wake wanatuhumiana kuhusika na mlipuko uliotokea katika mji mkuu wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 27, 2016 16:03 UTC
  • Serikali na wapinzani wakabana koo Madagascar

Serikali ya Madagascar na wapinzani wake wanatuhumiana kuhusika na mlipuko uliotokea katika mji mkuu wa nchi hiyo.

Mlipuko huo uliotokea jana mjini Antananarivo umezidisha mgogoro wa kisiasa unaoisumbua nchi ya Madagascar.

Kiongozi mwandamizi katika kambi ya upinzani nchini Madagascar, Guy Rivo Randrianarisoa, amesema kuwa ni upuuzi kwa serikali kuituhumu kambi ya upinzani kuwa ndiyo iliyohusika na mlipuko huo. Vilevile waziri mkuu wa zamani wa Madagascar, Omer Beriziky ambaye kwa sasa ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Antananarivo amesema hitilafu za kimitazamo si suala linaloweza kuchochea upande wa upinzani kutekeleza kitedo cha kinyama kama hicho.

Ripoti zinasema kuwa mlipuko huo uliotokea jana kwenye sherehe za kitaifa zilizofanyika katika uwanja wa michezo wa Mahamasina umesababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi wengine 80. Hali ya baadhi ya majeruhi imeripotiwa kuwa ni mbaya.

Katika miezi ya hivi karibuni Madagascar imetumbukia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa uliowafanya wapinzani wa serikali watoe wito wa kufanyika uchaguzi mkuu wa mapema.