Aug 13, 2023 02:40 UTC
  • Wafanyakazi Waturuki wanaojenga reli ya SGR Tanzania wagoma baada ya mishahara kucheleweshwa

Mamia ya wafanyakazi Waturuki walioajiriwa na kampuni ya ujenzi ya Uturuki ya Yapı Merkezi katika mradi wa reli ya Tanzania ya Standard Gauge (SGR) wamegoma tangu Agosti 5, wakitaka kulipwa mishahara yao ambayo hawajalipwa kwa muda wa miezi saba iliyopita.

Siku ya Ijumaa, wakati mgomo ulipoingia siku ya saba, wafanyikazi wa Yapı Merkezi walisema, "Tutaendelea na mgomo wetu hadi sauti zetu zisikike na hadi tupate mishahara yetu. Hatutoi sadaka, tunataka tunachostahiki.”

Ömer Tanrıverdi, mmoja wa wafanyakazi wa Yapı Merkezi waliogoma, ameliambia Shirika la Habari la Bianet la Uturuki lenye makao yake Beyoğlu, Istanbul, kwamba amekuwa akifanya kazi katika mradi huo kwa miezi 10 na hajapokea mshahara wake tangu mwezi Februari.

Tanrıverdi amesema kuwa Yapı Merkezi imekuwa ikikabiliwa na matatizo ya kiuchumi kwa miaka mitatu iliyopita, na kusababisha malipo kuchelewa.

Shirika la Yapi Merkezi limeviambia vyombo vya habari vya Uturuki kuwa halina habari yoyote kuhusu mgomo huo wa wafanyakazi wake, na hivyo maafisa wa shirika hilo wamekataa kujibu maswali mengine yanayohusiana nayo.

Mnamo Januari mwaka huu, kampuni ya ujenzi ya Türkiye, Yapı Merkezi, ilizindua ujenzi wa awamu ya 4 ya mradi wa SGR, sehemu ya Tabora-Isaka, ambao ujenzi wake unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 42 kuanzia Januari 2023.

Awamu ya 4 kutoka Tabora hadi Isaka inakuja baada ya awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu ya reli ya Dar Salaam-Mwanza nchini Tanzania. Yapı Merkezi ilianza kujenga vipande vyote vya ujenzi wa vituo vitatu kati ya miji ya Tabora na Isaka.

Kulingana na mapatano yaliyopo, kampuni hii pia ina jukumu la kujenga karakana ya matengenezo, eneo la bohari, jengo la ofisi za wasimamizi, Taasisi ya Utafiti wa Reli, na reli ya njia moja yenye urefu wa kilomita 165 na njia za kando, suhula za mawasiliano na uwekaji umeme katika reli hiyo.

Baada ya kukamilika, SGR ya Tanzania itakuwa reli ndefu zaidi kujengwa na mkandarasi wa Kituruki na ya kasi  zaidi katika Afrika Mashariki.

Dev Yapı-İş, chama chenye uhusiano na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi vya Maendeleo ya Uturuki, kina wanachama miongoni mwa wafanyakazi wa Uturuki wanaogoma nchini Tanzania, huku Rais wake Mkuu Özgür Karabulut akiliambia shirika la habari la Bianet kwamba chama hicho kinawaunga mkono wafanyakazi waliogoma.

Karabulut alibainisha kuwa pia kumekuwa na ucheleweshaji wa malipo kwa wafanyakazi wa Kitanzania kwenye mradi huo.

Kwa ujumla mradi huo wa SGR ya Tanzania unagharimu dola za Kimarekani Bilioni 10.

Tags