Algeria: Hatutaanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa kikoloni wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i101148-algeria_hatutaanzisha_uhusiano_wa_kawaida_na_utawala_wa_kikoloni_wa_israel
Naibu Spika wa Bunge la Algeria amesisitiza kuwa, taifa hilo la kaskazini mwa Afrika halitafuata mkumbo wa nchi nyingine za Kiarabu wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel, akisisitiza kuwa Waalgeria wanautazama utawala huo kuwa wa kikoloni.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 17, 2023 03:14 UTC
  • Algeria: Hatutaanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa kikoloni wa Israel

Naibu Spika wa Bunge la Algeria amesisitiza kuwa, taifa hilo la kaskazini mwa Afrika halitafuata mkumbo wa nchi nyingine za Kiarabu wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel, akisisitiza kuwa Waalgeria wanautazama utawala huo kuwa wa kikoloni.

Katika mahojiano na shirika la habari la Sputnik kitengo cha lugha ya Kiarabu, Moussa Kharfi, Naibu Spika wa Bunge la Algeria amesema taifa hilo la Kiarabu litaendelea kusimama kidete na kamwe halitaanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni.

Kharfi amesema, "Tunaiangalia Israel kuwa moja ya tawala za kikoloni, na katu haiwezi kuwa sehemu ya ulimwengu wa Kiarabu hata siku moja."

Ameeleza bayana kuwa, Algeria kwa miongo mingi imekuwa muhanga wa jinai za tawala za kikoloni, na inafahamu vyema dhulma za tawala za aina hiyo.

Naibu Spika wa Bunge la Algeria amebainisha kuwa, nchi hiyo ya Kiarabu haitubali kuburuzwa kuanzisha uhusiano wa aina yoyote na utawala haramu wa Israel.

Waalgeria wakiwatetea Wapalestina kwenye maandamano

Mwezi uliopita, Algeria ilikosoa vikali uamuzi wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wa kutambua mamlaka ya Morocco katika eneo linalozozaniwa la Sahara Magharibi.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria, hatua hiyo ya Israel ya kutambua mamlaka ya Morocco kwa eneo linalozozaniwa la Sahara Magharibi inakanyaga wazi sheria za kimataifa.