Aug 20, 2023 02:28 UTC
  • Taharuki yatanda nchini Niger baada ya ECOWAS kuamua tarehe ya kuishambulia nchi hiyo

Mji mkuu wa Niger, Niamey, unashuhudia vuguvugu na taharuki kubwa ya jeshi na wananchi wanaowaunga mkono viongozi wa mapinduzi wakipinga uwezekano wa uingiliaji kijeshi wa nchi wanachama wa Jumuiya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) nchini humo.

Taharuki hiyo imeanza kushuhudiwa siku moja baada ya wakuu wa majeshi ya kundi hilo kuamua tarehe ya kuingilia kijeshi huko Niger ili eti kurejesha uawala wa kikatiba.

Ripoti zinasema, wakuu wa majeshi ya Niger, Mali na Burkina Faso wamefanya mkutano mjini Niamey kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na hujuma yoyote ya kijeshi ya vikosi vya ECOWAS.

Wakuu wa majeshi ya Mali, Burkina Faso na Niger walikutana kujadili mkakati wa pamoja wa ulinzi, kujibu tamko la ECOWAS la kuwa tayari kuingilia kijeshi nchini Niger.

Katika muktadha huo, Waziri wa Ulinzi wa Burkina Faso, Kassoum Coulibaly, ametangaza utayarifu wa nchi yake kukabiliana na hujuma ya kijeshi ya kundi la ECOWAS nchini Niger.

Coulibaly ameeleza upinzani wa nchi yake kwa "hujuma" yoyote dhidi ya Niger, akitangaza kwamba Ouagadougou iko tayari kujiondoa katika kundi la ECOWAS, ambalo amesema halina mantiki katika sera yake kuhusiana na Niger.

Waziri wa Ulinzi wa Burkin Faso amesema inasikitisha kuona baadhi ya nchi za kanda ya Magharibi mwa Afrika zikiunga mkono chaguo la vita kwa kisingizio cha demokrasia.  

Tags