AU yataka kusuluhishwa mzozo wa Burundi haraka
Umoja wa Afrika umetoa wito wa kufanyika haraka mazungumzo ya kina yatakayojumuisha pande zote husika kwa ajili ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa nchini Burundi.
Hayo yamesemwa na ujumbe wa maafisa 15 wa Baraza la Usalama na Amani la umoja huo, baada ya kufanya ziara ya siku nne nchini Burundi. Lazare Makayat Safouesse, kiongozi wa ujumbe huo wa ngazi za juu wa Umoja wa Afrika jana Jumatatu aliwaambia waandishi wa habari mjini Bujumbura kuwa, katika kipindi cha siku nne zilizopita, maafisa hao wa AU wamekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa kisiasa wa nchi hiyo akiwemo Rais Pierre Nkurunziza, viongozi wa kidini, wanaharakati wa asasi za kiraia, wanadiplomasia na maafisa wa mashirika tofauti ya Umoja wa Mataifa nchini humo. Amesema Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika limeafiki kwamba kuna udharura wa kufanyika mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo, ambao hadi sasa umesababisha vifo vya watu 450 na wengine zaidi ya laki mbili na elfu 70 wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi. Amesema mazungumzo hayo yanafaa kufanyika katika ngazi tofauti na kwa kuwaleta pamoja wadau wote wa mgogoro wa Burundi. Burundi ilitumbikia katika mgogoro mkubwa wa ndani Aprili mwaka jana na mauaji ya hapa na pale yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara nchini humo hususan baada ya Rais Pierre Nkurunziza kugombea tena kiti hicho licha ya upinzani mkubwa wa vyama vya siasa.