Walibya: Serikali ya Dbeibah itimuliwe kwa kuvuka mistari myekundu
Viongozi na wanasiasa mashuhuri wa Libya wametoa mwito wa kuondolewa mamlakani serikali nzima ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Abdul Hamid Dbeibah, baada ya kufichuka habari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo kuonana kwa siri na waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni, Eli Cohen nchini Italia.
Khalid al-Mishri, Mwenyekiti wa zamani wa Baraza Kuu la Uongozi la Libya amelaani mkutano baina ya wawili hao ambao anasisitiza kuwa, yumkini si wa kwanza kufanyika.
Amebainisha hayo katika ujumbe aliouchapisha katika ukurasa wake wa Facebook na kuongeza kuwa, "Serikali ya Dbeibah imevuka mistari yote myekundu na inapasa kuondolewa mamlakani."
Wakati huo huo, mgombea wa urais wa Libya, Suleiman Al-Bayoudi ameishutumu serikali ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo kwa kuendeleza kampeni ya kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, akitaka kuondolewa madarakani serikali hiyo katika uchaguzi ujao.
Katika kuonyesha hasira zao dhidi ya serikali baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya kuonana na waziri huyo Mzayuni, wananchi wenye hasira wa Libya wameandamana na kuchoma moto bendera ya Israel na kulaani kitendo chochote cha kuwa karibu na utawala katili wa Israel.
Huku hayo yakiarifiwa, Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Libya amekimbilia Uturuki baada ya Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya kumsimamisha kazi kwa kosa la kuonana na waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni nchini Italia.
Al-Mangoush amekiri kuwa alifanya mazungumzo na Eli Cohen kwa uratibu wa waziri wa mambo ya nje wa Italia, Antonio Tajani, lakini amedai kuwa mazungumzo hayo hayakuwa rasmi na hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa.