Aug 29, 2023 11:51 UTC
  • Al Sisi akimpokea al Burhan
    Al Sisi akimpokea al Burhan

Mkuu wa Baraza la Utawala wa Sudan, Abdel Fattah Al-Burhan, leo Jumanne amewasili nchini Misri, katika ziara yake ya kwanza ya kigeni tangu kuanza mapigano ya ndani nchini Sudan yapata miezi 5 iliyopita, huku mapigano yakiendelea kati ya Jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) katika mji wa Khartoum na maeneo mengine.

Shirika la Habari la Middle East News Agency limeripoti kuwa Al-Sisi amempokea Al-Burhan katika Uwanja wa Ndege wa El Alamein.  

Baraza la Utawala wa Sudan limesema - katika taarifa yake - kwamba, katika ziara hiyo, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan anafanya mazungumzo na Rais wa Misri kuhusu hali ya Sudan, uhusiano kati ya nchi hizo mbili, na njia za kuimarisha na kustawisha uhusiano huo.

Katika safari hiyo, Kamanda wa Jeshi la Sudan Abdel Fattah Al-Burhan, anafuatana na kaimu Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Ali Al-Sadiq, Mkurugenzi wa Idara ya Ujasusi, Luteni Jenerali  Ahmed Ibrahim Mufaddal, na Mkurugenzi Mkuu wa Viwanda vya Ulinzi, Luteni Jenerali Mirghani Idris Suleiman.

Abdel Fattah al-Burhan, alisema hapo awali kwamba hakuna nuwezekano wa kufanya mazungumzo na wale aliowaita waasi na wasaliti, na amekanusha kuwepo kwa makubaliano yoyote ya kuondoka kwake Khartoum. 

Wakati huo huo Shirika la Habari la Ufaransa limewanukuu walioshuhudia na chanzo cha matibabu leo ​​Jumanne, kwamba takriban watu 39 wameuawa katika mashambulizi ya makombora yaliyolenga nyumba za raia katika kitongoji cha Sikkah Al-Hadid katika mji wa Nyala, mji mkuu wa Darfur Kusini (magharibi mwa Sudan), wakati wa mapigano kati ya Jeshi la Sudan na vikosi vya RSF.

Sudan

Shirika hilo limesema kuwa wengi kati ya waliouawa ni wanawake na watoto, ikiwa ni pamoja na familia ambayo watu wake wote wameuawa.

Tags