Umoja wa Mataifa walaani shambulizi la kigaidi na mauaji ya waziri Mogadishu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10168-umoja_wa_mataifa_walaani_shambulizi_la_kigaidi_na_mauaji_ya_waziri_mogadishu
Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Michael Keating, amelaani vikali shambulizi la kigaidi lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya hoteli ya Naso Hablod kusini mwa Mogadishu, ambako watu 25 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 28, 2016 09:39 UTC
  • Umoja wa Mataifa walaani shambulizi la kigaidi na mauaji ya waziri Mogadishu

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Michael Keating, amelaani vikali shambulizi la kigaidi lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya hoteli ya Naso Hablod kusini mwa Mogadishu, ambako watu 25 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Mmoja kati ya waliouawa katika shambulizi hilo alikuwa Bwana Buri Mohamed Hamza, Waziri wa Mazingira katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

Keating amesema amechukizwa mno na shambulio hilo lililopelekea watu wengi kupoteza maisha na kuongeza kuwa, kifo cha Waziri Hamza kinatia huzuni zaidi kwani alikuwa mtu mwenye hamasa kubwa katika kupigania mazingira nchini Somalia.

Kundi la magaidi wakufurishaji wa Al-Shabaab lilidai kutekeleza shambulizi hilo dhidi ya hoteli ya Naso Hablod, ambayo aghalabu hutumiwa na wanasiasa na watalii.

Katika shambulio hilo la Jumamosi iliyopita, gaidi mmoja wa ash-Shabab aliyekuwa kwenye gari lililokuwa na mada za milipuko alitekeleza shambulio kwenye mlango wa kuingilia hotelini hapo. Baada ya mlipuko huo wanachama wengine wa genge hilo waliokuwa wamejizatiti kwa silaha waliingia katika hoteli hiyo ya Nasa Hablod na kuwateka nyara watu kadhaa.