Maandamano ya kutaka kufukuzwa askari wa Ufaransa yashtadi Niger
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i101772-maandamano_ya_kutaka_kufukuzwa_askari_wa_ufaransa_yashtadi_niger
Maelfu ya wananchi wa Niger wamefanya maandamano katika mji mkuu Niamey, kuonyesha uungaji mkono wao kwa serikali ya kijeshi inayotawala hivi sasa, na kutaka kufukuzwa nchini humo wanajeshi na wanadiplomasia wa Ufaransa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 02, 2023 11:09 UTC
  • Maandamano ya kutaka kufukuzwa askari wa Ufaransa yashtadi Niger

Maelfu ya wananchi wa Niger wamefanya maandamano katika mji mkuu Niamey, kuonyesha uungaji mkono wao kwa serikali ya kijeshi inayotawala hivi sasa, na kutaka kufukuzwa nchini humo wanajeshi na wanadiplomasia wa Ufaransa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Waandamanaji hao jana Ijumaa walikusanyika nje ya uwanja wa ndege wa kijeshi wa Kikosi cha 101 cha Ufaransa mjini Niamey, ambapo walisikika wakipiga nara za kulaani ubeberu wa Ufaransa, na uwepo wa wanajeshi wa Kifaransa katika nchi hiyo huru.

Viongozi wa Kiislamu nchini humo ni miongoni mwa shakhsia walioshiriki maandamano hayo ya kutaka kutimuliwa nchini humo wanajeshi na mabalozi wa Ufaransa.

Issaka Hassane Karanta, Rais wa Baraza la Waislamu la Niger (CSN) ameikosoa vikali Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS kwa kuiwekea Niger vikwazo, na kutishia kuishambulia kijeshi nchi hiyo mwanachama wake, kwa mashinikizo ya Wamagharibi.

Wakati huo huo, serikali ya kijeshi ya Niger imelaani kauli aliyotoa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa usiku wa kuamkia leo na kutangaza kuwa, lengo la Macron ni kuzusha machafuko katika eneo la Afrika Magharibi na kuwatia hofu viongozi wa eneo hilo.

Wananchi wa Niger katika maandamano dhidi ya Ufaransa

Sambamba na mivutano iliyozuka wiki kadhaa baada ya kuondolewa madarakani rais wa Niger, Mohamed Bazoum, Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali ya kijeshi ya Niger wiki iliyopita ilimpa balozi wa Ufaransa, Sylvin Yette, saa 48 kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo.

Balozi huyo wa Ufaransa alikaidi agizo hilo na kutangaza kuwa ataendelea kusimamia wadhifa wake, uamuzi ambao ulisifiwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Polisi nchini Niger wanaendelea kuzingira majengo ya ubalozi huo mjini Niamey, huku Baraza la Kijeshi linalotawala nchi hiyo likichukua uamuzi wa kupiga marufuku shughuli za mashirika ya kimataifa na yasiyo ya kiserikali.