Abbas ataka wafungwa wote wa Kipalestina waachiwe huru
Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ametaka kuachiwa huru wafungwa wote wa Kipalestina wanaoendelea kuteseka katika jela na magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Karibu Wapalestina 5,000 wanashikiliwa katika jela za utawala wa Kizayuni wa Israel, ambapo 160 kati yao ni watoto na 29 ni wanawake.
Abbas amenukuliwa akitoa mwito huo Jumamosi na shirika la habari la Palestina la SAMA na kuongeza kuwa, "Taifa la Palestina linakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zina mfungamano na uporaji na ukaliaji wa mabavu wa ardhi zao unaofanywa na Israel."
Mahmoud Abbas amesema Wapalestina mbali na kukabiliwa na matatizo ya kiuchumi, mfumuko wa bei na kupanda kwa bei za bidhaa, lakini pia wanakabiliwa na dhulma za kihistoria ambazo ni kizingiti kwenye njia ya matumaini ya taifa hilo.
Kadhalika amelaani vikali kimya cha jamii ya kimataifa na kutochukua kwake hatua yoyote ya maana kukabiliana na vitendo vya kinyama na jiinai za utawala ghasaibu wa Israel huko Palestina.
Amekosoa udhaifu wa jamii ya kimataifa na kushindwa kwake kuchukua hatua za kuulazimisha utawala ghasibu wa Israel ukubaliane na maamuzi ya walimwengu na kuheshimu maazimio ya kimataifa.
Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameeleza bayana kuwa: Haki za Wapalestina madhulumu zimekanyagwa na viatu vya kijeshi vya utawala wa Israel kwa miaka 70. Katika kipindi hicho, utawala ghasibu umetenda jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina.