Jeshi la Kenya laua wanachama 4 wa al-Shabaab, Lamu
Askari wa Kenya wamewaangamiza wanamgambo wanne wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika kaunti ya Lamu.
Kanali David Obonyo, Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Kenya amesema wanachama hao wa al-Shabaab waliuawa jana Jumatano baada ya kujiri mapigano makali kati yao na askari wa KDF, katika eneo la Milimani, karibu na mji wa Baure kaunti ya Lamu.
Amesema askari wa KDF waliwavizia wanachama zaidi ya 30 wa al-Shabaab waliokuwa wanapanga kushambulia kambi ya jeshi ya Mangai; na baada ya makabiliano makali na jeshi la Kenya, wanne waliuawa huku makumi ya wengine wakikimbilia msitu wa Boni ulioko katika kaunti hiyo. Msemaji wa Jeshi la Ulinzi nchini Kenya amesema askari mmoja wa KDF amejeruhiwa katika makabiliano hayo na kuongeza kuwa wamefanikiwa kunasa silaha kadhaa za wanamgambo wa al-Shabaab, yakiwemo maroketi, maguruneti, mada za miripuko na bunduki 4 aina ya AK-47. Aidha amesisitiza kuwa operesheni ya kuwafurusha wanachama wa al-Shabaab kutoka msitu wa Boni maarufu kama 'Operation Linda Boni' itaendelea hadi watakapohakikisha kuwa wameusafisha msitu huo. Mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu, kundi la al-Shabaab lilidai kuwa limeua askari wapatao 200 wa Jeshi la Ulinzi la Kenya KDF katika kambi ya El-Adde nchini Somalia.