Libya yaagiza kukamatwa maafisa 8 katika uchunguzi wa kuporomoka kwa bwawa
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Libya imesema, Mwendesha Mashtaka Mkuu huyo ameamuru kukamatwa maafisa wanane kama sehemu ya uchunguzi wake kuhusu maafa ya hivi majuzi ya mafuriko ambayo yalisababisha vifo vya maelfu ya watu.
Taarifa iliyotolewwa na ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali ya Libya imeeleza kuwa, maafisa husika wa idara ya vyanzo vya maji na usimamizi wa mabwawa ya Libya wanashukiwa kwa uongozi mbovu na upuuzaji.
Makundi ya Misaada ya Kimatafa yalisema katika ripoti yao ya Jumamosi iliyopita kuwa hadi sasa watu walioaga dunia kwa mafuriko huko Libya imepindukia 3,800 na kwamba watu 10,000 au zaidi hawajulikani walipo.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali ya Libya Al Seddik- al Sur alisema zaidi ya wiki moja iliyopita baada ya kuanza uchunguzi kuhusu janga la mafuriko lililoikumba nchi hiyo kuwa mabwawa mawili katika mji wa Derna yalipasuka tangu mwaka 1998.
Ukarabati uliokuwa umeanza kufanywa kwenye mabwawa hayo na kampuni ya Uturuki mwaka 2010 ulisimamishwa baada ya miezi kadhaa wakati yalipopamba moto mapinduzi ya Libya mwaka 2011; na kazi hiyo haikuanza tena.
Bwawa la kwanza kuporomoka katika maafa hayo lilikuwa bwawa la Abu Mansur, lililoko umbali wa kilomita 13 kutoka Derna, ambalo hifadhi yake ilikuwa na mita za ujazo milioni 22.5, kisha mafuriko yakapasua bwawa la al Bilad lililokuwa na uwezo kuhifadhi mita za ujazo milioni 1.5.